HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 14, 2018

MTENDAJI MKUU TFS ALEZEA JITIHADA WANAZOFANYA KWA KUSHIRIKIANA NA WADAU KULINDA NA KUHIFADHI MISITU

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo ameelezea jitihada mbalimbali zinazofanyika nchini katika kulinda na kuhifadhi uoto wa misitu asili nchini.

Amesema hayo akiwa eneo la Msitu wa Kazimzumbwi wilayani Kisarawe mkoani Pwani wakati wa uzinduzi wa jitihada za Tanzania kuungana na nchi nyingine za Afrika katika kuhifadhi na kuendeleza hifadhi za misitu

Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Japhet Hasunga pamoja na mwenyeji wao Mkuu wa wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo ambaye alitumia nafasi hiyo kuelezea jitihada zinazofanyika kulinda misitu iliyopo wilayani kwake.

Akizungumza kwenye tukio hilo Profesa Silayo amefafanua Tanzania ni mwanachama wa Afrika katika juhudi hizo za kuhifadhi na kuendeleza hifadhi za Misitu African Forest Landscape Restoration Initiatives (AFR100).

Amesema lengo kuu la juhudi hizo ni kurejesha Uoto wa Asili kwa bara la Africa kwa hekta millioni 100 ifikapo mwaka 2030 na kwamba mkakati huo ulijadiliwa na kukubalika katika mkutano wa 14 wa Misitu uliofanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2015.

Ambapo uliliona suala hili na kuanzisha mkakati huu wa Nchi za Afrika. Pia mkatati huo wa Afrika ni kwa ajili ya kuchangia mkatati wa Dunia (Bonn Challenge) wenye lengo la kurejesha uoto wa asili kwa hekta milioni 150 ifikapo mwaka 2020 na hekta milioni 350 ifikapo mwaka 2030.

“Kidunia mkakati huu ulizinduliwa mwaka 2011 huko Ujeruman na baadaye kujadiliwa tena mwaka 2014 katika mkutano wa dunia wa mabadiliko ya tabianchi (UN Climate Summit),”amesema.

Amesema Januari mwaka huu Tanzania iliungana na nchi nyingine kwa kuwasilishwa barua kwenye Secretariat  inayojukikana kama New Partnership for Africas Development (NEPAD) Agency.

Aidha, Mratibu wa mkakati huo ni Ofisi anayoisimamia ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na inaendelea kuratibu shughuli zote zinazolenga mkakati.

Pia amesema maboresho ya usimamizi wa misitu na jitihada za kuhuisha (restore) maeneo ya misitu ni sehemu ya jitihada za kitaifa na dunia kwa jumla ambazo zinalenga kutimiza malengo ya mikataba au maazimio mbalimbali.

Ametaja baadhi ya maazimio hayo ni  malengo endelevu kimataifa hasa lengo la 13 kuhusu hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko, lengo 15 kuhusu kulinda, kurejesha na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali asilia.

Pia usimamizi endelevu wa misitu, kupambana na kunenea kwa hali ya jangwa na ukame, kuongoa ardhi iliyohabirika, kupunguza upoteaji wa bioanui.

Profesa Silayo amesema pia malengo namba 1 na 2 yanayolenga kumaliza umasikini, njaa na kilimo endelevu, mkataba wa Hifadhi ya Bioanuai,

Mkataba wa Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame na mkataba wa Kimataifa wa mabadiliko ya Tabianchi.

Amesema kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na nchi za Afrika, Kabla ya kuandaa mkakati wa Kitaifa wa utekelezaji kila nchi inatakiwa kuahidi ukubwa wa eneo (hekta) la misitu/ hifadhi ambazo inakusudia kuzihuisha.

“Ahadi hiyo hutakiwa kutangazwa rasmi katika vyombo vya habari hatua ambayo tunaifanya leo hii. Ifahamike tu kuwa malengo haya tunayoyatangaza leo yalifikiwa kufuatia vikao vya wataalam mbalimbali,”amesema.

Hivyo kwa kuanzia, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania iliandaa mikutano kadhaa baina ya  wadau wa sekta mbalimbali Bara na Visiwani kwa kushirikiana na Shirika la WWF kwa ajili ya kutathimini na kukubaliana ukubwa wa hekta za misitu ambazo Tanzania itatangaza kwa ajili ya uhifadhi.

Amesema katika mkakati huo utahusisha pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kutokana na vikao hivyo vya kitaalam, makubaliano yalifikiwa  baina ya wadau wote kuhusu ukubwa wa eneo la  misitu ambalo tunaweza kuahidi kuhifadhi kama Taifa.

Hivyo, kulingana na umuhimu wa mkakati huo wakaona ni vyema waende maeneo ambayo wanaweza kutamka lakini pia kuonyesha mfano na kufanya Sherehe za utangazaji katika msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbwi.

“Uamuzi wa kuja Kazimzumbwi umetokana na umuhimu wa kuliweka jambo hili katika uhalisia wake. Pia kuenzi jitihada zinazofanywa na wadau na viongozi katika ngazi zote katika kusimamia rasilimali za misitu na nyuki nchini,”amesema.

Ameelezea kutambua kwake mchango wa Mkuu wa wilaya ya Kisarwe Mwegelo na mtangulizi wake Happiness Saneda ambao wameonesha njia katika kusimamia misitu yetu kwa kufanya operesheni maalumu ya kuwaondoa wavamizi kwenye misitu ya wilaya hiyo.

Wakati huo huo TFS na WWF wameweka masaini makubaliano yenye lengo la kuhakiksha msitu wa Kazimzumbwi, Ruvu Kusini na Vikindu inaendelezwa, kulindwa na kuhifadhiwa pamoja na kuhakiiisha inawekea mazingira mazuri ili iwe sehemu ya utalii ambapo watu mbalimbali watapata nafsi ya kutembelea.

Waliosaini makubaliano hayo ni Profesa Silayo pamoja na Mkurugenzi Mkaazi wa WWF  Tanzania Dk.Amani Ngusaru.

Akizungumzia mkataba huo Dk.Ngusaru amesema lengo ni kuona misitu iliyopo nchini inalindwa na kuhifadhiwa na kubwa zaidi kuwekewa mazingira ambayo yatafanya iwe vivutio kwa ajili ya utalii na wamekuwa wakishirikiana na Serikali kwa muda mrefu na wamefanya hivyo katika misitu mbalimbali nchini. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Does Santos Silayo(kulia) pamoja na Mkurugenzi mkazi wa WWF Tanzania Dk.Amani Ngusaru(kushoto) wakisaini mkataba wenye lengo la kulinda na kuhifadhi msitu wa Kazimzumbwi ,Ruvu Kusini na Vikindu wilayani Kisarawe.Wanaoahuhudia ni Mkuu wa Wilaya Kisarawe Jokate Mwegelo na Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Japhet Hasunga.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Does Santos Silayo(kulia) akiwa ameshikana mkono na Mkurugenzi mkazi wa WWF Tanzania Dk.Amani Ngusaru baada ya kusaini mkataba wenye lengo la kulinda na kuhifadhi msitu wa Kazimzumbwi ,Ruvu Kusini na Vikindu wilayani Kisarawe.Wanaoahuhudia ni Mkuu wa Wilaya Kisarawe Jokate Mwegelo na Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Japhet Hasunga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Profesa Does Santos Silayo(kulia) pamoja na Mkurugenzi mkazi wa WWF Tanzania Dk.Amani Ngusaru wakiwa wameshika mikataba mara baada ya kusaini mkataba wenye lengo la kulinda na kuhifadhi msitu wa Kazimzumbwi ,Ruvu Kusini na Vikindu wilayani Kisarawe.Wanaoahuhudia ni Mkuu wa Wilaya Kisarawe Jokate Mwegelo na Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii Japhet Hasunga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad