HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 19 August 2018

Maugo amchapa Mmalawi, Class amnyamazisha Mazola kwa TKO

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo wa Tanzania amemchapa kwa pointi, mpinzani wake, Charles Misanjo wa Malawi katika pambano la kimataifa la uzito wa Super Middleweight kwenye ukumbi wa PTA jijini. Wakati Maugo anashinda kwa pointi, bondia nyota nchini,Ibrahim Class alidhihirisha ubora wake baada ya kushinda kwa Technical knockout (TKO) raundi ya tano katika uzito wa Super Feather.

Pambano hayo yaliandaliwa kwa lengo la kutafuta mataulo ya kike kwa wanafunzi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa kushirikiana na taasisi ya She Can Foundation. Katika pambano hilo lililoandaliwa na promota wa kwanza wa kike nchini, Sophia Mwakagenda wa kampuni ya Lady In Red Promotion, Maugo alipata pointi 77-75 kutoka kwa jaji, Mwinyi Milla,  78-74 (Modesti Rashid) na 76-76 kutoka kwa jaji, Chaurembo Palasa.
Bondia Mada Maugo (kulia) akirusha konde kwa Charles Misanjo wa Malawi katika pambano la kimataifa la uzito wa Super Middle lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA juzi. Maugo alishinda kwa pointi.

Pamoja na ushindi huo ulilalamikiwa na Misanjo na baadhi ya mashabiki wa ngumi za kulipwa, Maugo alisema kuwa Mmalawi alikuwa anapiga makofi baadala ya ngumi ndiyo maana ameonekana kushambulia sana.

“Mimi nimekuwa nikipigana kwa kutafuta pointi kwa kupiga ngumi, yeye alikuwa anapiga makofi muda wote na kusukuma, hao mashabiki na bondia inaonekana hawajui ngumi, sijapendelewa kwa sababu ya Utanzania, hapana,” alisema Maugo.

Misanjo alisema kuwa haikuwa ngumi za kawaidi bali ni vita. “Matokeo sikubaliani nayo, yanaua mchezo wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, itatufanya tusiwe tunakuja kupigana kutokana na maamuzi kama haya,” alisema Misanjo. Pambano kati ya Ibrahim Class na Baina Mazola ndilo lilikuwa na msisimko mkubwa ambapo mabondia hao walionyesha uwezo mkubwa. Class alianza pambano kwa kasi na kutawala raundi mbili za mwanzoni huku Mazola alikitawala raundi ya tatu.
Bondia Ibrahim Class (kushoto) akimchapa ngumi mpinzani wake, Baina Mazola katika pambano la uzito wa Super Feather kwenye ukumbi wa PTA juzi.Class alishinda kwa technical knockout (TKO) raundi ya tano.

Mabondia hao walipigana kwa visasi na kuleta burudani ya aina yake. Class alionekana kutumia uzoefu zaidi na kufanikiwa kumchana jicho Mazola katika dakika ya 1.47 ya raundi ya tano na kuibuka mshindi.

“Nimepoteza kwa kuumia, hata hivyo nitamtafuta tena Class ili kuonyesha kuwa mimi ni bora zaidi yake,” alisema Mazola. Class alisema kuwa mpinzani wake ni mzuri na ushindi ni jambo la kawaida sana kwake.

“Mimi ni bondia bora, hilo halina ubishi,Mazola bado sana kwangu, afanyekazi ya zaida kunifikia na kunishinda,” alitamba Class.

Bondia Flora Machela alifanikiwa kushinda kwa TKO raundi ya tano dhidi ya Sarafina Julius katika pambano la uzito wa bantam wakati Asha Ngedere na Happy Daudi wakitoka sare kwa katika pambano la  uzito wa Super Light.

Akizungumza baada ya pambano hilo, promota Mwakagenda aliwapongeza wadau na makampuni yaliyochangia kufanikisha tukio hilo japo lengo la kukusanya mataulo 40,000 halijafanikiwa.

“Huu ni mwanzo na jambo hili ni geni kwangu, ndiyo kwanza nimeandaa ngumi za kulipwa na nimeona changamoto zake, nimejifunza na nitaendelea kuandaa kwa malengo maalum,” alisema Mwakagenda.
Mabondia wa kike, Asha Ngedere (kushoto) na Happy Daudi wakipambana uliongoni. Mabondia hao walitoka sare.
Bondia Flora Machela akimchapa konde mpinzani wake, Sarafina Julius katika pambano la uzito wa bantam kwenye ukumbi wa PTA. Flora alishinda kwa TKO raundi ya tano.
Ngumi ni mchezo, lakini ni hatari sana! Bondia Baina Mazola akiuguliwa baada ya kuchanwa na Ibrahim Class katika pambano la uzito wa Super Feather. Class hakutumia kisu wala kiwembe, ila ni nguvu ya mikono yake ndani ya glovu.
Mheshimiwa mbunge Sophia Mwakagenda akiwa na waheshimiwa wenzake na mabondia wa kike wakati wa pambano la kutafuta fedha za kununua mataulo ya kike kwa wanafunzi wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa mbunge Sophia Mwakagenda (wapili kulia) akizungumza wakati wa pambano la kutafuta fedha za kununua mataulo ya kike kwa wanafunzi wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad