HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 18, 2018

KONGAMANO LA BIASHARA NA UWEKEZAJI LAFANYIKA JIJINI SEOUL, KUHAMASISHA WADAU WA MADAWA NA VIFAA TIBA KUWEKEZA NCHINI TANZANIA

Katika kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ubalozi wa Tanzania Seoul kwa kushirikiana na “Korea-Africa Foundation” na “Korea Chamber of Commerce and Industry” uliandaa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kwa wadau wa sekta ya Afya lililofanyika Seoul, Jamhuri ya Korea. Kongamano hilo la aina yake, lilijumuisha Wizara na Taasisi za kuitendaji katika eneo husika ambazo ni: Wizara ya Afya; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Kituo cha Uwekezaji (TIC); MSD; TFDA, na TAPI (Tanzania Association Pharmaceutical Industries).

Aidha, Kongamano hilo lililolenga kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya madawa na vifaa tiba nchini Tanzania, lilihudhuriwa pia na makampuni zaidi ya 100, kutoka pande zote mbili ikijumuisha: Makampuni ya utengenezaji madawa na vifaa tiba; Vyuo Vikuu; Taasisi za utafiti; Hospitali; Vyama vya watengenezaji wa madawa na vifaa tiba; Makampuni kutoka katika sekta binafsi; na Diaspora wetu waliopo Seoul.

Katika Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa zikijumuisha: Fursa zilizopo Tanzania katika sekta ya utengenezaji wa madawa na vifaa tiba, mazingira ya ufanyaji biashara na vivutio “incentives” vinavyotolewa na Serikali; Hali ya soko na uhitaji (Market Potentiality); Taratibu za kufuatwa katika uingizwaji wa bidhaa za madawa na uanzishwaji wa viwanda husika; na utayari wa sekta binafsi katika kushirikiana na wenzao wa Korea katika biashara na ubia katika viwanda vya madawa na vifaa tiba. Upande wa Korea pia ukiwakilishwa na Vyama vya watengenezaji wa madawa na vifaa tiba walitoa mada iliyokuwa na lengo la kubadilishana uzoefu na upande wa Tanzania. Kongamano lilihitimishwa kwa B2B, ambapo makampuni na Taasisi zilikutana kujadiliana zaidi fursa, maeneo ya ushirikiano, na kupata ufafanuzi wa kina katika maeneo mbalimbali; na baadaye kutembelea Makampuni ya Madawa.
Mgeni Rasmi katika Kongamano la kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya madawa na vifaa tiba, Bw. Geoffrey Mwambe, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) akitoa Hotuba ya Ufunguzi, kwa niaba ya Mhe. Ummy Ally Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Mhe. Matilda Swilla Masuka akitoa neno la ukaribisho katika Kongamano hilo.
Rais wa “Korea-Africa Foundation” waandaaji wenza wa Kongamano hilo, Balozi CHOI, Yeon-ho, akitoa neno katika hafla ya ufunguzi.
Sehemu ya washiriki katika Kongamano la kuhamasisha wawekezaji wa viwanda vya Madawa na vifaa tiba Seoul, Jamhuri ya Korea, August 13, 2018.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Geoffrey Mwambe, ulipotembelea Kampuni ya kutengeneza Madawa ya Celltrion, na kujionea shughuli mbalimbali za kampuni hiyo. Celltrion ni kampuni maarufu na inashika Na.1 nchini Korea katika “ sekta ya Bio-pharmacy”. Wakati za ziara hiyo ujumbe wa Tanzania uliambatana na Balozi wa Tanzania Korea, Mhe. Matilda Swilla Masuka, na Rais wa “Korea-Afrika Foundation”, Balozi Yeon-ho CHOI.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Bw. Geoffrey Mwambe ulipokutana na Kampuni ya LS watengenezaji wakubwa wa Matrekta na vifaa vya kilimo nchini Korea Kusini wenye lengo la kupanua wigo wa biashara kwa kuwa na uwakilishi na pia kuwekeza kwenye kiwanda “Assembly Plant”.
Ujumbe huo ulikutana pia na makampuni ya Hyundai yenye nia ya kuwekeza kwenye kiwanda cha kuunganisha magari “Assembly Plant”; na KT Telecoms yenye lengo la kufanya kazi na makampuni ya Kitanzania kwenye miradi ya TEHAMA.
Ujumbe kutoka Tanzania ukiwa katika picha ya pamoja na Wana Diaspora ambao walishiriki kikamilifu katika Kongamano hilo la kuhamasisha wawekezaji katika viwanda vya madawa na vifaa tiba.
Sehemu ya ujumbe kutoka Tanzania wakiwa na mwenyeji wao Balozi Matilda Swilla Masuka, baada ya kufanikisha Kongamano hilo la aina yake na lililovutia makampuni ya madawa na vifaa tiba zaidi ya 100.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad