HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 4, 2018

IGP Sirro awataka Wakufunzi wa Vyuo vya Polisi vya Dar na Zanzibar kuwafundisha Askari Polisi Wanafunzi

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewataka Wakufunzi wa Vyuo vya Polisi vya Dar es Salaam na Zanzibar kuhakikisha wanawafundisha Askari Polisi Wanafunzi waliopo katika vyuo hivyo kwa kuzingatia mitaala iliyotolewa ili wanapotoka waweze kuwatumikia Wananchi na kupunguza uhalifu hapa nchini.

IGP Sirro ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake katika vyuo hivyo ambapo alizungumza na Wakufunzi pamoja na Askari wanafunzi wanaosomea vyeo mbalimbali ambapo lengo la ziara hiyo ni kukagua muenendo wa mafunzo katika vyuo vya Polisi.

Amesema lengo la mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivyo yanapaswa kutolewa kwa weledi ili kila Askari anayehitimu aweze kupata maarifa ambayo yatawezesha kufanya kazi za Polisi vyema jambo ambalo litaendelea kupunguza uhalifu hapa nchini.

“Kila mkufunzi anapaswa ahakikishe lile somo analolifundisha wanafunzi wake wanalielewa ili kusudi kama ni Ofisa, Mkaguzi na Kiongozi mdogo ndani ya Jeshi la Polisi anafanya kazi kwa kufuata ile misingi iliyopo” Alisema Sirro.

Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Anthony Rutta amesema lengo la mafunzo katika Chuo hicho ni kuhakikisha kila Askari anayatambua majukumu yake ili kupunguza uhalifu hapa nchini na watahakikisha ukakamavu na nidhamu inazingatiwa ili kuwa na Jeshi lenye kufuata kanuni na taratibu zilizopo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Polisi Zanzibar Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Geofrey Kamwela amesema Chuo hicho kinakabiliwa na Changamoto mbalimbali zikiwemo za uchakavu wa miundombinu yakiwemo majengo na bwalo la Chakula ambapo IGP Sirro aliahidi kutuma fedha za awali kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la kulia chakula chuoni hapo.

Kamwela alisema hivi sasa wanaendelea kutekeleza mradi wa kuweka mfumo wa Tehama ambao utawezesha wanafunzi kujisomea na kupata matokeo yao kwa njia ya mtandao jambo ambalo litawafanya kwenda kisasa katika utoaji wa elimu chuoni hapo.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini yupo katika ziara ya kukagua mafunzo yanayoendelea katika vyuo vya Polisi hapa nchini ili kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanawajenga Maofisa na Askari kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kupunguza uhalifu hapa nchini.
 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akisalimiana na Maofisa wa Polisi Kamisheni ya Zanzibar wakati wa Ziara yake inayoendelea katika Vyuo vya Polisi hapa nchini kwa lengo la kuboresha elimu inayotolewa na vyuo hivyo
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akiimba wimbo pamoja na Askari wakati wa kikao chake na Askari wanafunzi katika Chuo cha Polisi Zanzibar wakati wa ziara yake. Kulia kwake ni Kamishna wa Polisi Zanzibar Mohamed Hassan Haji na kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha Kamisheni ya Polisi Zanzibar Faustine Shilogile.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro akizungumza na Mafundi wa Nguo za Polisi waliopo katika Kiwanda cha Polisi cha kushona nguo Kamisheni ya Polisi Zanzibar wakati wa Ziara yake inayoendelea katika Vyuo vya Polisi hapa nchini kwa lengo la kuboresha elimu inayotolewa na vyuo hivyo (Picha na Jeshi la Polisi).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad