HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 30 August 2018

HAKI MADINI WAJENGEA UWEZO JAMII WA ARDHI NA MADINI

SHIRIKA la Haki Madini la jijini Arusha, limewajengea uwezo viongozi wa serikalini, wa kimila na baadhi ya wananchi wa mikoa ya kanda ya kaskazini, juu ya utambuzi wa uthamini wa fidia ya ardhi na madini. 

Mwanasheria wa shirika la Haki Madini, Erick Luwogo akizungumza mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro,  alisema kupitia mafunzo waliyotoa, elimu ya fidia ya ardhi na madini itaifikia jamii ipasavyo. 

Luwogo alisema wanataka kuona changamoto ya ucheleweshaji wa fidia, isiyo sahihi na kukatazwa kufanya maendelezo zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka. 

"Tumekutanisha wadau wengi wakiwemo wanasheria, wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji, viongozi wa kimila, jamii na lengo hasa ni kupata majawabu ili serikali inapotoa fidia iwe inafanya kwa wakati," alisema. 

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Anthony Mavili alisema miradi mingi mikubwa ya eneo hilo imefanyika lakini wananchi ambao waliathirika kwa namna moja au nyingine hawakufidiwa. 

"Kuna barabara ya lami ya Kia-Mirerani wananchi waliovunjiwa nyumba zao hawakufidiwa na pia ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite kuna makazi, maboma ya wafugaji na njia za mifugo ilipitiwa ndani ya ukuta lakini jamii haikufidiwa," alisema Mavili. 

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Mundarara Wilayani Longido Mkoani Arusha, Yohana Muyase alisema tatizo la muda mrefu wa kulipwa fidia linawatatiza wananchi. 

Muyase alisema fidia ni suala lililopo kisheria hivyo linapaswa kutekelezwa mara baada ya kufanyika kwa tathimini tofauti na ilivyo hivi sasa. 

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Godbless Mollel amesema kupitia elimu hiyo ataenda kuwasaidia wananchi juu ya elimu ya fidia. 

Mthamini mkuu wa Halmashauri ya jiji la Arusha, Rosemary Kirenga alisema pamoja na manufaa ya elimu hiyo bado tatizo la kulipwa fidia kwa wakati baada ya kufanyika tathimini ni changamoto na watalifanyia kazi. 

Kirenga alisema ofisi ya mthamini imeona changamoto hizo hivyo wanaendelea kutoa elimu ya fidia ili jamii itambue kuwa serikali ipo pamoja nao katika kuwatekelezea kwa wakati. 

Alisema kupitia sheria mpya ya wathamini iliyopitishwa na bunge ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake zitawawezesha wananchi walipwe fidia zao kwa wakati. 
 Baadhi ya walioshiriki warsha hiyo mwanasheria wa TLS Linda Shamba (kushoto) na mhandisi wa madini Ernest Sanka.
 Baadhi ya viongozi wa serikali, wanasheria na wananchi walioshiriki kwenye warsha ya sheria ya fidia ya ardhi na madini iliyoandaliwa na shirika la Haki Madini, mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. 
 Mmoja kati ya wawezeshaji wa warsha hiyo, mthamini mkuu wa Halmashauri ya jiji la Arusha, Rosemary Kirenga (kushoto) na mwanasheria wa shirika la Haki Madini, Erick Luwogo wakizungumza na washiriki wa warsha hiyo. 
Mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Anthony Mavili akizungumza juu ya fidia kwenye warsha ya sheria ya fidia ya ardhi na madini iliyoandaliwa na shirika la Haki Madini mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro. 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad