HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 20 July 2018

WAZIRI WA MAJI AMTUMBUA MENEJA WA DAWASCO ILALA

*Amtaka Mtendaji Mkuu wa DAWASCO kumpangia kituo kingine cha kazi.
*Awaagiza DAWASCO kupeleka maji Kiwanda cha Bia TBL ndani ya wiki moja.


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa amemuagiza Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam (DAWASCO) Mhandisi Cyprian Luhemeja kumbadilisha kituo cha kazi Meneja wa Mkoa Ilala Chris Kaoneka kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Prof Mbarawa ametoa agizo hilo leo Jijini Dar es Salaam alipotembelea kiwanda cha Bia cha TBL na SBL katika ziara ya kushtukiza kwa ajili ya kuangalia miundo mbinu ya DAWASCO na kuona watendaji wa Shirika hilo kutokuwa makini kulinda rasilimali zao.

Akizungumza baada ya kumaliza kutembelea Kiwanda cha TBL, Prof Mbarawa amesema kuwa kiwanda hicho kina mahitaji ya maji Lita Milioni 60 kwa mwezi ila mtendaji mkuu wa DAWASCO pamoja na wasaidizi wake wameshindwa kukidhi mahitaji ya mteja na badala yake anapata lita milioni 17 hadi 20 kwa mwezi.

"Nawaaagiza ndani ya wiki moja muwe mmewapatia maji wanayohitaji ya Lita Milioni 60 kwa mwezi kwani DAWASCO kuna maji ya kutosha na yakutosha ila nashangaa kwa nini suala hilo limeshindwa kufanyika muda wote," ameagiza Prof Mbarawa.


Amesema kuwa, DAWASCO mnatakiwa mfanye biashara lakini kama Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO hajawahi kwenda kuwatembelea wateja wake kujua nini wanahitaji na kwa muda basi suala hilo linasababisha kutokupatikana kwa mapato yanayostahili kutoka kwenye Viwanda vilivyopo Jijini Dar es Salaam.

"Kama Afisa Mtendaji Mkuu unashindwa kwenda kuwatembelea wateja wako hususani wakubwa kama hawa ina maana kuwa hauko makini, ni lazima ujue wateja wako wanahitaji nini na kwa wakati gani ili waweze kukidhi mahitaji yao na kwa hili nakulaumu wewe,"

Katika kutembelea kiwanda hicho Prof Mbarawa aliweza kutembelea palipo Mita ya maji ya DAWASCO na kuwataka waibadilishe na kuweka ya Kieletroniki  itakayokuwa inasoma Wizarani na Ofisini kwao wenyewe ikiwemo na kuiwekea seal, mbali na hilo amewataka wakate bomba moja liliopo ndani ya kiwanda cha TBL na kuliacha moja kutokana na maelezo yao kuwa wanatumia bomba moja kwa mahitaji yao.

 Akiwa katika kiwanda cha SBL, Prof Mbarawa ametembelea bomba la maji taka lililojengwa na kampuni hiyo na namna wanavyochakata maji yao na kuyasafirisha kwa njia ya mabomba na kwenda katika sehemu maalumu ya kuyahifadhi ya DAWASCO.

Waziri amewashauri SBL na makampuni mengine kutumia maji ya DAWASCO  kwakuwa yapo mengi na ya kutosha pia ni salama na safi kwa matumizi yote.

Waziri Prof Mbarawa amekuwa katika ziara maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam hususani katika viwanda kwa ajili ya kuangalia Miundo mbinu ya DAWASCO ya maji safi na maji taka pamoja na namna wanavyokuwa wanafuatilia usomaji wa mita zao na jinsi ulipaji unavyoenda kwa kila kiwanda.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kutembelea kiwanda cha bia cha TBL  na kuwaagiza watendaji wa Shirika la Maji safi na Maji taka (DAWASCO) kupelekea maji ya kiasi cha lita Milioni 60 kwa mwezi ndani ya wiki moja. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu DAWASCO Mhandisi Cyprian Luhemeja.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa  akisikiliza maelekezo kutoka kwa Meneja wa Mkoa wa Ilala DAWASCO Chris Kaoneka alipotembea kiwanda cha Bia cha TBL  leo Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa akiuliza jambo kwa DAWASCO baada ya kukagua mita ya maji ya Kiwanda cha bia cha  TBL na kuonekana kuna mapungufu ikiwemo kukosekana kwa seal kwenye bomba hilo.
  Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa akiwa anatembelea kiwanda cha bia cha Serengeti SBL na akionyeshwa visima wanavyovitumia kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya Kiwanda hicho.
 Mkurugenzi wa Mahusiano wa kiwanda cha bia cha SBL John Wanyancha akitoa maelezo kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof Makame Mbarawa alipotembelea kiwanda hicho leo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad