HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 20 July 2018

SSRA YAHIMIZA VIJANA KUJENGA DESTURI YA KUJIWEKEA AKIBA

“Kesho ya Mtu hujengwa leo na Tofali la kujengea kesho hufyatuliwa leo” hii ni kauli ya Sarah Kibonde Msika, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii – SSRA akizungumza na vijana waliotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya 13 ya Elimu ya Juu na Taasisi za Kitafiti na wadau wa elimu ya juu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Akifanunua kauli hiyo, Mkuu huyo wa Kitengo kutoka SSRA anasema, Taifa linakabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini wa kipato hasa kwa baadhi ya makundi kama ya wazee, jambo linalotokana na watu wengi kutokuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba na maandalizi ya kufikia uzee, hivyo kuwahimiza vijana wenye nafasi ya kurekebisha hali hiyo kuanza maandalizi mapema kwa kujiwekea akiba kwa njia mbalimbali ikiwemo Mifumo ya Hifadhi ya Jamii .

Kwa kutambua changamoto hiyo ya umaskini wa kipato hasa wakati wa uzee, SSRA inajukumu la kuhakikisha watanzania wanapata kinga kwa ajili ya kuwalinda dhidi ya majanga ya kiuchumi na kijamii. Mpaka sasa imefanya juhudi ya kuanzisha mipango ya kupambana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo utakaoruhusu kila kundi katika jamii kufaidika na huduma za Hifadhi ya Jamii. Miongoni mwa mipango hiyo ni pamoja na mfumo wa hiari/ziada (Supplementary Schemes), wenye lengo la kukabiliana na mahitaji mahususi ya nguvukazi katika sekta isiyo rasmi ambayo kwa hakika inajumuisha sehemu kubwa zaidi ya nguvukazi nchini, anasema Sarah Kibonde.

Akifafanua kuhusu Mpango huo, Sarah anasema chini ya usimamizi wa SSRA, nguvukazi kutoka katika wa sekta isiyo rasmi na hata wanafunzi wa vyuo vikuu sasa ina fursa ya kuchagua na kuchangia kiasi chochote wanachomudu kila mwezi au kila mara kadiri watakavyoweza. Katika mfumo huo inahimizwa zaidi kuwa fao litakalopatikana litategemea kiasi cha michango kitakachotolewa.

Kiasi cha michango kinavyokuwa kikubwa zaidi ndivyo fao linavyokuwa kubwa zaidi. Kuhusu utaratibu na namna ya kujiunga na mfumo huu wa hiari, Sarah anawashauri vijana kutembelea katika ofisi za Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii.

Hivyo basi, SSRA inatumia maonesho haya ya Elimu ya Juu kuelimisha Umma juu ya masuala ya Hifadhi ya Jamii hususani kukutana na vijana waliopo vyuoni na wanaotarajiwa kuingia vyuoni, lengo likiwa ni kuwaelimisha na kuwaimiza kuweka akiba jambo litakalowajengea tabia ya kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadae na kuwaepusha na changamoto ya umaskini wa kipato wakati wa uzee. “Majuto ya kesho huandaliwa leo” anasisitiza Bibi. Sarah Kibonde
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Uhamasishaji wa SSRA, Sarah Kibonde Msika akifafanua jambo wakati kwa wadau waliotembelea banda la SSRA wakati wa Maonyesho ya Taasisi za Elimu ya Juu yanaendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Afisa Matekelezo wa SSRA, David Lyanga akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la SSRA lililoko kwenye Maonyesho ya Taasisi za Elimu ya Juu yanaendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye banda la SSRA wakati wa Maonyesho ya Taasisi za Elimu ya Juu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijni Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad