HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 7 July 2018

WAZIRI MKUU: SERIKALI HAITANUNUA MADENI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haina mpango wa kununua madeni yaliyosababishwa na mikopo ya kibenki kwenye vyama vikuu vya ushirika nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Julai 7, 2018) wakati akizungumza na wanaushirika na mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Furahisha, jijini humo.

“Serikali ya awamu ya tano hatuna biashara ya kununua madeni ya vyama vikuu, kulikuwa na tabia ya watu wa ushirika kukopa na hali ikiwa mbaya wanakimbilia Serikalini. Serikali hii hatuna biashara hiyo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema anazo taarifa kwamba Chama Kikuu cha mkoa wa Kagera (KCU) kimekopa fedha Benki ili kiweze kulipa deni la mwaka 2014. “Nimeambiwa KCU wamekopa fedha benki ili kulipa deni la mwaka 2014, hii inaingia akilini kweli? Mnakopa fedha kulipa deni la zamani, ni kwa nini msiwatafute waliosababisha deni na kuwachukulia hatua?,” alihoji.

“Ninyi mlikuwa watu sita ambao mlikubaliana kama viongozi, mlienda kukopa kuzidi uwezo mlionao. Leo hii ni kwa nini serikali ije kulipa wakati mmetumia ninyi?,” aliuliza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tatno inasisitiza masuala ya ushirika kwa sababu imeamua kuwahudumia wananchi kuanzia ngazi ya chini kuanzia pembejeo, dawa hadi masoko.

“Tunataka tuondoe utaratibu wa chama kikuu kukopa fedha benki ili kikanunue mazao. Vyama vingi vimetengeneza hasara, leo hii vyama vikuu vina madeni. Hii ni kwa sababu mlikopa fedha benki wakati hata hamjui mna kilo ngapi ambazo zimevunwa.

“Fedha mnachukua nyingi na hata ikibaki hamrudishi benki. Riba anadaiwa mkulima kupitia kilo anazouza, deni anapelekewa mkulima na kuanza kukatwa kwa kila kilo. Hatutaki tena utaratibu huu. Kuanzia sasa, AMCO ndiyo itaratibu na kukusanya mazao ya kila mwanachama kwa sababu yenyewe inajua ina wanachama wangapi, wana ekari ngapi na wanatarajia kuvuna kilo ngapi,” amesema.

Amesema ili kuondokana na utaratibu wa vyama vikuu kukopa benki, Serikali imepiga marufuku utaratibu huo na badala yake wanunuzi wataenda kununua mazao kwenye vyama vya msingi kupitia minada na watatakiwa kuwa wameingiza fedha kwenye vyama vya msingi (AMCOS) ndani ya siku tatu.

“Tulishasema mwisho uwe ni msimu huu, yasijirudie tena haya mambo ya kukopa benki.  Mnunuzi akipata mnada, ndani ya siku tatu, anatakiwa awe amehamisha fedha kwenda kwenye akaunti ya AMCOS husika,” alisema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema mfumo wa ushirika bado unakabiliwa na changamoto ya upotoshaji na maewagiza maafisa ushirika wakasimamie suala hilo kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakulima.

“Leo hii tunakabiliwa na changamoto kubwa kupitia uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi za Mazao Ghalani, Kuna watu wanapita wakipotosha kwamba serikali inawakopa wakulima mazao yao.”

“Nendeni mkawaelimishe wakulima kwamba mtu akipeleka mazao yake ghalani siyo kwamba anakuwa tayari ameuza, bali anayaweka pale na kujua ana kilo ngapi, amapewa risiti na kusubiri bei iwe nzuri wakati wanunuzi wakibishana. Hela ikilipwa, anapewa hela yote kulingana na mzigo wake,” alisema.

Siku ya Ushirika Duniani huadhimishwa Jumamosi ya kwanza ya Julai kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Ushirika kwa ulaji wa uzalishaji endelevu wa bidhaa na huduma.” 
 Waziri Mkuu, Kassim  Majalawa akizungumza katika Maadhimisho ya siku ya ushirika dunianiyaliyofanyika kitaifa  kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, Julai 7, 2018.
 Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba akizungumza wakati alipomkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhutubia katika Maadhimisho ya siku ya Ushirika duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa  Furahisha jijini Mwanza, Julai 7, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Ushirika nchini, Bibi Renata Mwageni (kushoto) Tuzo ya  Rais John Pombe Magufuli iliyotolewa na Wanaushirika nchini  ili kutambua mchango wa Rais  katika kuendeleza sekta ya ushirika na kuinua uchumi wa wananchi wa Tanzani ya 2018 . Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye  Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye  uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Juni 7, 2018.  Wapili kushotoi ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba na kulia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab  Telack.
 Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika Maadhimisho ya  Siku ya Ushirika duniani  wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua mizani ya Kielektroniki ya kupima uzito wa pamba wakati alipotembelea banda la Chama Kikuu  cha Ushirika cha Nyanza katika maonyesho ya siku ya Ushirika duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa  Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018. Wapili kulia ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba na watatu kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwaanjelwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama pamba iliyostawi vizuri wakati alipotembelea banda la Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza  baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018.  Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitazama pamba iliyostawi vizuri wakati alipotembelea banda la Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza  baada ya kuhutubia katika maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018.  Wanne kulia  ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack. Wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Magu  Khadija Nyembo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama samaki waliokaushwa  wakati alipotembelea banda la Vyma vya Ushirika katika Soko la Kimataifa la Kirumba – Mwaloni wilayani Ilemela baada ya kuhutubia katika Maadhimisho ya siku ya Ushirika duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Zainab Telack na watatu kushoto ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela .
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa TANESCO wakati alipotembelea banda lao katika maonyesho ya siku ya Ushirika duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa furahisha jijini Mwanza  Julai 7, 2018.  Wapili kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack na watatu kushoto ni Naibu Waziri wa Kilimo, Dkt. Mary Mwanjelwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama pamba  na mafuta yanayotokana na mbegu za pamba wakati alipotembelea banda la Ushirika wa wilaya ya Chato katika monyesho ya Ushirika yaliyofanyika kitaifa  kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza Julai 7, 2018,.


 Msanii wa kikundi cha sanaa cha Buyegi, John Riziki akicheza ngoma ya nyoka katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, Julai 7, 2018.  Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad