HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 12 July 2018

Wananchi Mtego wa Simba wafurahia kuwashiwa umeme

Na Veronica Simba – Morogoro
Wananchi wa Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, wameshindwa kuzuia furaha yao baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, kuzindua rasmi uwashaji wa umeme katika Kijiji hicho, kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA.)
Tukio hilo la kuwasha umeme, lilifanyika Jumatano, Julai 11, 2018 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, ambao muda wote walionesha bashasha, Mgumba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa kuendelea kutekeleza ahadi ya kuwapelekea wananchi, hususan walioko vijijini nishati ya umeme.
“Serikali iliahidi kwamba itasambaza umeme kwa vijiji vyote vilivyobaki, kwenye Awamu mbili za REA III. Tunatoa shukrani sana kwa kuja hapa leo kutekeleza ahadi hiyo kwa vitendo.”
Akizungumza katika Hafla hiyo, Naibu Waziri aliwaeleza wananchi kuwa baada ya uzinduzi huo, wataanza kuunganishiwa umeme katika nyumba zao kuanzia Ijumaa, Julai 13, mwaka huu.
“Nimeongea na Mkandarasi, kuanzia Ijumaa, zile nyumba za awali 62 zote zitawekewa umeme.”
Mbali ya uzinduzi huo wa uwashaji umeme, Naibu Waziri alitembelea Zahanati iliyopo katika Kijiji cha Towero, Kata ya Mlimani, Wilaya ya Morogoro Mjini, kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Machi 24 mwaka huu, kuiunganishia Zahanati hiyo umeme.
Naibu Waziri alikiri kufurahishwa na Uongozi wa TANESCO kwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati, ambapo mbali na kuiunganishia zahanati husika umeme, wameunganisha pia huduma hiyo muhimu kwa Shule ya Msingi iliyopo eneo hilo na kueleza kuwa wana mpango wa kupeleka umeme huo kwa Shule ya Sekondari ya mahala hapo.
“Kipekee niwapongeze TANESCO Mkoa na Makao Makuu kwa kuendelea kutekeleza maagizo ya viongozi wetu ya kupeleka miundombinu ya umeme kwenye huduma za kijamii ikiwemo zahanati, vituo vya afya, shule mbalimbali, miradi ya maji na nyinginezo.”
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kwa Naibu Waziri, Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrance Maro, alisema kuwa Transfoma iliyofungwa ili kuwezesha kuunganisha umeme huo ni yenye uwezo wa  kilovoti 50 na kwamba wamejenga njia ndogo ya kusafirisha umeme, yenye urefu wa kilomita 1.5.
Aidha, Naibu Waziri alitembelea Mtaa wa Mafisa, Kata ya Tungi, Wilaya ya Morogoro Mjini, ambapo aliridhishwa na hatua iliyofikiwa katika kutekeleza agizo alilolitoa Machi 24 mwaka huu, kuanza kazi ya kupeleka umeme katika eneo hilo.
“Namshukuru Mungu kazi imeanza na inaonekana. Tumeona njia ya umeme imeanza kujengwa na nguzo zimeanza kuchimbiwa. Kazi hii kwa awamu ya kwanza itagharimu shilingi milioni 107,” alisema.
Naibu Waziri Mgalu yuko katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme katika mikoa kadhaa nchini.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akifurahia baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa uwashaji umeme katika kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Jumatano, Julai 11, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo na wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza wakati wa Hafla ya uzinduzi rasmi wa uwashaji umeme katika kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Jumatano, Julai 11, 2018.
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) akiwasha taa ya umeme, katika moja ya vyumba vya Zahanati ya Kijiji cha Towero, Kata ya Mlimani, Wilaya ya Morogoro Mjini, Jumatano, Julai 11, 2018. Naibu Waziri alitembelea Zahanati hiyo kujiridhisha endapo agizo alilotoa kwa TANESCO kuiunganishia umeme limetekelezwa. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo na wa kwanza kulia ni Meneja wa TANESCO wa Kanda ya Kati, Mhandisi Athanas Nangali.
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (katikati), akicheza muziki na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wananchi, kusherehekea uzinduzi rasmi wa uwashaji umeme katika kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Jumatano, Julai 11, 2018. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo na wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba.
 Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Lawrance Maro (aliyesimama), akizungumza, wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (mwenye kilemba cha pinki) katika Zahanati ya Kijiji cha Towero, Kata ya Mlimani, Wilaya ya Morogoro Mjini, Jumatano, Julai 11, 2018.
 Naibu Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Omari Mgumba, akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, katika Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini; ambapo alizindua rasmi uwashaji wa huduma ya umeme. Hafla hiyo ilifanyika Jumatano, Julai 11, 2018.
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akiwaonesha wananchi wa Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, kifaa kitumikacho kuwasha umeme pasipo kutandaza nyaya katika nyumba, kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA). Alikuwa katika ziara ya kazi kijijini hapo ambapo alizindua rasmi uwashaji wa huduma ya umeme, Jumatano, Julai 11, 2018.
 Baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi, wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa uwashaji umeme katika Kijiji cha Mtego wa Simba, Kata ya Mikese, Wilaya ya Morogoro Vijijini, Jumatano, Julai 11, 2018.
 Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (wa pili kutoka kushoto), akizungumza jambo, wakati akiwa katika ziarani Mtaa wa Mafisa, Kata ya Tungi, Wilaya ya Morogoro Mjini, Jumatano, Julai 11, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi.
Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Regina Chonjo (wa tatu kutoka kushoto). Naibu Waziri alifika ofisini hapo kuelezea dhamira ya ziara yake wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Jumatano, Julai 11, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad