HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 9, 2018

VIGODORO NA NGOMA ZA USIKU KWA WATOTO NI MARUFUKU!!

Katibu tawala mkoani Pwani, Zuberi Samataba akitembelea baadhi ya mabanda ya maonyesho ya kielimu yaliyoandaliwa na baadhi ya wanafunzi Chalinze Mkoani Pwani wakati wa maadhimisho ya Juma la elimu kimkoa yaliyofanyika Chalinze mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali Chalinze Mkoani Pwani wakionyesha mabango katika maadhimisho ya Juma la elimu kimkoa yaliyofanyika Chalinze.

NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE

SERIKALI Mkoani Pwani, imekemea tabia inayofanywa na baadhi ya wazazi ya kuwahusisha watoto wao kwenda katika vigodoro,  kudhurula nyakati za usiku na badala yake wawasimamie katika suala la elimu ili kuinua taaluma zao. Aidha imewaonya wazazi wanaowakataza watoto wao kwenda shule na wengine kuwashawishi watoto hao kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya kumaliza darasa la saba na kidato cha nne.

Akitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani, Katibu tawala wa mkoa huo, Zuberi Samataba alisema, wapo wazazi na walezi ambao ndio chanzo cha kudidimiza suala la elimu. Alieleza, endapo watambaini mzazi ama mlezi akimwachia mtoto kuzurula na kumhusisha kwenye vigidoro na ngoma za usiku atakiona.

"Serikali haiwezi kukubali mzazi akaachia mtoto kiholela, watoto ni wa serikali, mzazi atakaebainika kufanya hayo hatutamvumilia, hii inasababisha kudumaza elimu mkoani kwetu"

Alizielekeza halmashauri kuwachukulia hatua wazazi wanaowaachia huru watoto wao kwani wanahatarisha maisha ya watoto hao hasa kusababisha mimba za utotoni. Samataba alikemea mimba za utotoni, na amesisitiza kuchukuliwa hatua kali kwa wanaosababisha mimba hizo.
Alisema, zipo taarifa zilizokuwa zikidai wapo wazazi wanaojua watoto wao wanafanya vizuri darasani ambapo wanawakataza kufanya vizuri kwenye taaluma zao.

Nae kaimu afisa elimu mkoa ,Hedegald Makundi alieleza uandikishaji katika elimu ya awali  bado upo  chini  tofauti na wanaoandikishwa darasa la  kwanza.

"Elimu ya awali lengo lilikuwa ni kuandikisha  wanafunzi 35,418 walioandikishwa ni 26,997 sawa na asilimia 76 ambapo uandikishaji darasa la kwanza lengo ilikuwa 47,686 walioandikishwa ni 52,551 sawa na asilimia 110" alieleza Hedegald.

Mwenyekiti wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Pwani, Ramadhani Maneno alisema ili kuhakikisha elimu inaboreshwa ni  lazima kushirikiana wadau, wazazi na walimu kutatua changamoto za kielimu bila kuiachia serikali pekee.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad