HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 7 July 2018

Tanzania yasisitiza ushirikiano kutekeleza SDGs

SERIKALI ya Tanzania imeomba wadau wa maendeleo na taasisi mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Mataifa kuendelea kufanyakazi nayo kuhakikisha kwamba ajenda ya kimataifa ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 inaendelea kutekelezwa nchini.
Hayo yalisemwa katika kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa malengo hayo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk Augustine Mahiga.
Aidha alisema serikali imetengeneza mikakati kadhaa ya kuwezesha kutekelezwa kwa malengo hayo ya dunia.
Alisema wakati Tanzania imekaza nia ya kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda suala linalosisitizwa katika SDG 9 ni muhimu na kwamba serikali ya Tanzania inataka kuendeleza ushirikiano huo ili malengo ya dunia yafikiwe pia nchini Tanzania.
Alisema Tanzania chini ya uongozi wa Rais John Magufuli inaendelea kutekeleza mpango wa maendeleo endelevu wa Umoja wa Mataifa (SDGs) wenye lengo la kufikia ustawi kwa kila mkazi wa dunia hii.
Ili kutekeleza malengo hayo, mpango wa maendeleo wa miaka mitano umeingiza malengo ya SDGs.
“Kama nchi tangu tumeanza kutekeleza SDG kwenye  mwaka 2016, tumechambua na kuingiza vipengele vya SDGs kwenye mipango mbalimbali ya kitaifa ikiwamo mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano 2016/17-2020/21 (FYDP II) na mpango wa tatu wa kukuza uchumi wa Zanzibar na kupunguza umaskini (MKUZA III)” alisema.
Aidha alisema hatua kadhaa zimechukuliwa kuhakikisha kwamba malengo hayo yanatekelezwa ikiwamo uboreshaji wa vyanzo vya mapato ya ndani.
“ Tumeingia katika mifumo ya kisasa ya ukusanyaji  wa mapato, kutanua wigo wa kodi, kukabiliana na rushwa na kukabiliana na tabia zote zinazochochea upotevu wa mapato” alisema Dk Mahiga na kuongeza kuwa juhudi zilizofanyika zimefanya kuwepo na utekelezaji mzuri wa malengo hayo.
Pia alisema wameweka mikakati ya kuhakikisha kwamba malengo hayo yanapatiwa fedha na pia kushawishi ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma ili kufikia malengo hayo ambayo yametamkwa katika mpango wa maendeleo wa kitaifa.
Pamoja na kuhimiza uwekezaji, serikali pia imekuwa ikifanya juhudi na kuwa na soko la fedha lenye uhakika ambalo litachangia kupatikana kwa mitaji kwa ajili ya uwekezaji.
 Waziri Mahiga alisema pamoja na kuhakikisha mambo yanaenda vyema nchini, serikali pia imekuwa ikishirikiana na taasisi za kimataifa na mataifa mengine ili mitaji ya utekelezaji wa malengo hayo ya dunia ikiwamo ajenda 17 unafanikiwa.
Hata hivyo katika mkutano huo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema kwamba  kumekuwa na uchelewefu wa utekelezaji wa makubaliano ya misaada yenye lengo la kujazia utekelezaji wa SDGs.
Katika mazungumzo hayo alitaka wadau wa maendeleo kutekeleza ahadi zao kwa kuwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano unatekeleza makubaliano ya malengo ya dunia ya SDGs.
Alisema mafanikio ya mpango hayo yanategemea sana utekelezaji wa msingi katika siku 1000 za utekelezaji wa malengo hayo ya dunia.
Katika siku hizo imeelezwa ni lazima kuwepo na utashi wa kisiasa,uwajibikaji na ushirikiano.
Alisema yapo makubaliano miongoni mwa nchi za Afrika namna ya kutekeleza kwa kasi wa Agenda hiyo ya maendeleo.
 Alisema pamoja na serikali kufanikiwa kutoa elimu kwa watunga sera na sheria na wananchi kwa ujumla kuhusu SDGs na kuingiza ajenga hizo katika mipango ya kitaifa.
Alisema pamoja na mafanikio mengi yanaonekana kuhusu utekelezaji wa malengo hayo, Tanzania imekuwa na matatizo katika utekelezaji wake.
Miongoni mwa matatizo hayo ni ya kifedha, uwezo wa kiufundi, mawasiliano na uragibishi na changamoto zinazotokana na takwimu.
Aidha wadau wa maendeleo wamepunguza misaada yao na pia wakati mwingine wamekuwa wakichelewesha.
“Ukiangalia utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2017/18 inaonesha kuwa mikopo na ruzuku iliyopatikana kutoka kwa wadau wa maendeleo (DPs) inafikia Shilingi trilioni 1.87 sawa na asilimia 47 lengo la Shilingi trilioni 3.97 . “ alisema Dk Mpango na kusema hali hiyo inaathiri utekelezaji wa SDGs.
Wakati huo huo Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez amesema umoja huo utaendelea kufanyakazi na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kwamba malengo ya maendeleo endelevu yanafanikiwa.
Mratibu huyo amesema inafurahisha namna ambavyo serikali ya Tanzania inatekeleza malengo hayo kuanzia uhamasishaji na hadi sasa kuwekewa mikakati pamoja na kutumbikizwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
Rodriguez amesema Serikali ya Tanzania inapaswa kuungwa mkono na kupongezwa kwa kufanya juhudi za kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha zake.
Pia Mratibu huyoa amesema kwamba yapo mambo ambayo yanastahili kuzingatiwa hasa namna ya kuangalia utekelezaji na uratibu wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (kulia) akizungumza jambo na Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kushiriki kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu. Wengine katika picha Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (katikati), Mtaalam wa Programu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Amon Manyama (wa pili kulia) pamoja na Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada nchini, Sue Steffen (kushoto).
 Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad (kulia) akibadilishana mawazo na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk. Tausi Kida (wa pili kulia), Mtaalam wa Programu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Amon Manyama (katikati) pamoja na Mkuu wa Maendeleo kutoka Ubalozi wa Canada nchini, Sue Steffen (kushoto) wakati kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu (SDGs) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk Augustine Mahiga akisalimiana na  Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya (kushoto) mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kushiriki kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Augustine Mahiga akibadilishana mawazo na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Maniza Zaman wakati kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu (SDGs) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga (kulia)wakijidiliana jambo Ofisa anayeshughulikia mambo ya kigeni wa Wizara hiyo, Nguse Nyerere kabla ya kuanza kwa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu (SDGs) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
  Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez (kulia) akifurahi jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini (UNDP), Natalie Boucly wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiitambulisha meza kuu kutoka kushoto ni Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Augustine Mahiga, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolf Mkenda pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolf Mkenda akitoa neno la ukaribisho wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dk. Augustine Mahiga akitoa neno la ufunguzi wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akizungumza kwenye kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akitoa maelezo mafupi kuhusu mkutano wa mashauriano baina ya Serikali ya Tanzania na mashirika ya Umoja wa Mataifa wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Adolf Mkenda
Balozi wa Norway nchini Tanzania, Hanne-Marie Kaarstad akitoa maoni wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Malawi nchini Tanzania, Hawa Ndilowe akizungumza wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo akibadilishana mawazo na mmoja wa wadau wa maendeleo wakati wa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam Baadhi ya wadau wa maendeleo, viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na Waheshimiwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini walioshiriki kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam
Picha ya pamoja ya viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo kutoka mashirika mbalimbali na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wizara, wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, taasisi za serikali na meza kuu mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kupewa taarifa ya utekelezaji wa maendeleo endelevu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad