HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 2, 2018

KAMATI YA MIUNDOMBINU YATAKA THAMANI YA FEDHA KATIKA MIRADI YA RELI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeutaka uongozi wa Kampuni ya Reli (TRC), kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya reli zinatumika kwa miradi iliyotengewa ili ikamilike kwa wakati na viwango.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Seleman Kakoso, ameyazungumza hayo mwishoni mwa wiki mkoani Kilimanjaro, mara baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa reli ya kaskazini kuanzia Tanga-Moshi-Arusha, na kusisitiza kuwa reli hiyo ni muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa.

“Hakikisheni mnatumia fedha za miradi kwa maeneo husika kwani Serikali imejikita katika kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa kwenye miradi zinatumika vizuri bila kubadilishwa matumizi ”, amesisitiza Mhe Kakoso.

Aidha Mhe. Kakoso, amesema kuwa ni wakati sasa kurudisha nguvu kwenye reli ya kati ili kusafirisha mizigo mikubwa na kuufikisha kwa watumiaji kwa wakati na hivyo kunusuru uharibifu wa barabara unaoendelea kujitokeza.

Ameongeza kuwa kazi za ukarabati zinazofanywa zifanyike kwa wakati mmoja sambamba na utoaji wa elimu kwa maeneo yote ya hifadhi ya reli ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa wananchi waliovamia maeneo ya reli nchini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt Leonard Chamuriho, amesema kwa sasa Serikali imeamua kuwekeza kwenye uboreshaji wa reli iliyopo na Reli ya Kisasa ya Standard Gauge ambao ujenzi wake unaendelea kwa awamu ya kwanza inayotoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na ile awamu ya pili inayoanzia Morogoro mpaka Makutupora, Dodoma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Bw. Masanja Kadogosa, amewaeleza wajumbe wa Kamati kuwa kazi zinazoendelea ni ukarabati wa njia kuanzia Mombo mpaka Moshi na sehemu ya ukarabati kuanzia Tanga mpaka Mombo umeshakamilika.

Ameongeza kuwa kazi zitakazofuata baada ya kukarabati njia ni kukarabati madaraja yaliyo katika njia hiyo na hatua ya mwisho sasa itakuwa kupitisha treni ya mizigo ili kupima uimara wa reli hiyo kabla haijaanza kutumika kwa treni za abiria.

Kuhusu suala la ajira, Bw. Kadogosa amefafanua kuwa kampuni inafanya ukarabati kwa kuwatumia wananchi ambao wanaishi maeneo jirani na reli inapopita na kuahidi kuwaajiri mara ya ukarabati huo kukamilika ili waweze kuitunza reli hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Moshi Seleman Kakoso, akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, wakikagua jengo la Stesheni ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), wakati kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ukarabati wa reli ya Tanga-Moshi-Arusha, mkoani Kilimanjaro.
Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Dkt Leonard Chamuriho, akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu tofauti kati ya reli ya kati (Meter Gauge) na Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati kamati hiyo ikikagua maendeleo ya ukarabati wa reli ya Tanga-Moshi-Arusha, jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu maendeleo ya ukarabati wa wa reli ya Tanga-Moshi-Arusha katika stesheni ya Kisanigilo, wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo kuona maendeleo ya ukarabati wake.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu maendeleo ya ukarabati wa wa reli ya Tanga-Moshi-Arusha katika eneo la KIA, Mkoani Kilimajaro wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo kuona maendeleo ya ukarabati wake, jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad