HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 3 July 2018

DAKTARI BINGWA WA MAGONJWA YA MOYO WA HEAMEDA MEDICAL CLINIC ATOA USHAURI NAMNA YA KUEPUKA MAGONJWA YA MOYO

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
DAKTARI Bingwa wa magonjwa ya moyo nchini kutoka Heamedia Medical Clinic Dk. Hery Mwandolela amesema kuna umuhimu mkubwa wa kila mmoja wetu kuhakikisha anapima afya yake mara kwa mara huku akitaja sababu zinazosababisha ugonjwa wa moyo.

Pia amesema ni vema kila mtu akafahamu namba saba muhimu kwa afya yako na kusisitiza kitendo cha kuchelewa kutambua ugonjwa mapema kunasababisha gharama kubwa zaidi ya ungetambua mapema na kukika ugonjwa husika.

Dk. Hery Mwandolela amesema hayo leo kwenye mahojiano maalum wakati anazungumza na Michuzi Blog kwenye banda lake lililopo katika Maonesho ya Bishara ya kimataifa yanayoendelea viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Amesema lengo la uwepo wake kwenye banda hilo kwanza unalenga kuwakumbusha wananchi mbalimbali kutambua umuhimu wa kupima afya mara kwa mara kwani inasaidia kupunguza gharama za matibabu.

Pia amesema yupo kwenye maonesho hayo kwasababu anataka kuwafahamisha Watanzania huduma bora na za kiwango cha juu katika kutibu magonjwa ya moyo ambayo yaafanywa na madaktari wabobezi waliopo Heameda Medical Clinic iliyopo mtaa wa Fubu maeneo ya Bunju B jijini.

Dk.Mwakandolela amesema pamoja na kutoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu wameweka gharama nafuu ambazo kila mmoja anaweza kumudu ukilinganisha na maeneo mengine.

Akifafanua zaidi kuhusu kupima afya mara kwa mara amesema magonjwa kama ya kupanda kwa shinikizo la damu na kisukari huweza kuja bila dalili yeyote na wakati mwingine yanagundulika baada ya mhusika kupata madhara makubwa.

"Njia pekee ya kukabiliana na magonjwa haya ni kujenga tabia ya kupima afya zetu hata kama hatusikii dalili zozote za ugonjwa, kwani hii itsaidia kugundua tatizo mapema na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana nalo.

"Ugonjwa kama kupanda kwa shinikizo la damu hupewa jina muuaji kimya kimya kutokana na tabia yake ya kuwepo bila kuonesha dalili zozote za ugonjwa wakati ukiharibu viungo kama moyo, macho, figo na hata ubongo,"amesema Dk.Mwandolela.

Ameongeza unaweza kuwa na tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu bila kuwa na dalili zozote na njia pekee ni kupima shinikizo la damu.

Amesema kupanda kwa shinikizo la damu bila kudhibitiwa huweza kusababisha madhara makubwa katika moyo, mishipa ya ya damu, macho, figo na ubongo.

"Hivyo tupo hapa katika maonesho pamoja na kutoa ushauri wa masuala ya afya tunaenelimisha Watanzania umuhimu wa kupima afya zao.Ukipima afya mapema ni rahisi kutatatua tatizo kwa kupata dawa za kukinga ambazo gharama yake ni nafuu kuliko dawa za kutibu.

"Ukigundua tatizo mapema ni rahisi kwenda kwa hospitali ukiwa mwenyewe na hivyo hata gharama ya usafiri itakuwa ya kawaida lakini ukichelewa hadi tatizo litokee maana yake itabidi ubebwe na hautaweza kupanda hata daladala, hivyo gharama zitaongezeka.Ndio maana tunashauri upimaji wa afya wa mara kwa mara,"amesema Dk.Mwandolela.

Kuhusu afya ya moyo wako , Dk.Mwakandolela amesema ni vema ukaonana na daktari ili kufanya vipimo vitakavyosaidia kufahamu hali halisi ya moyo wako.Endapo huna tatizo lolote ni vizuri kufanya vipimo vinavyokutaarifu kuhusu afya ya moyo na mishipa ya damu angalau kila baada ya miaka miwili.

Akizungumzia namna ya kufahamu namba saba muhimu kwa afya yako , amesema mhusika anatakiwa kufahamu uzito unaokubalika kwa afya bora, kufahamu shinikizo la damu , kufahamu ukubwa wa mzunguko wa kiuno chak na kiwango cha sukari katika damu.

Pia kufahamu kiwango cha mafuta katika damu na kufahamu kiwango cha mapigo ya moyo wako.

Amezungumzia umuhimu wa kufanya mazoezi angalau nusu saa kwa siku, au mara tano kwa juma na kwamba mazoezi hayo yanaweza kuwa ni kwa kutembea, kukimbia ,kuendesha baiskeli, kufanya kazi zinazotumia nguvu na kushiriki katika michezo.

Ametoa rai kwa Watanzania ni vema wakapata muda wa kupumzika, kukabiliana na msongo wa mawazo, kujumuika na unawapenda na kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula. 
Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo nchini kutoka Heamedia Medical Clinic Dk. Hery Mwandolela akimuelezea mwandishi wa habari Said Mwishehe wa Michuzi Media mambo mbalimbali yanayosababisha watu kukumbwa na magonjwa ya moyo katika banda la Kliniki hiyo lililopo kwenye viwanja vya maonyesho vya Sabasaba Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Daktari  Bingwa wa magonjwa ya moyo nchini kutoka Heamedia Medical Clinic Dk. Hery Mwandolela akionyesha mfano wa moyo wa binadamu. 
Daktari  Bingwa wa magonjwa ya moyo nchini kutoka Heamedia Medical Clinic Dk.Hery Mwandolela akizungumza na mmoja wa wananchi waliotaka kupata ufafanuazi wa magonjwa ya moyo alipotembelea katika banda hilo.

1 comment:

  1. Naifahamu Clinic hii,ni Clinic Bora hapa Tanzania.Dr Mwandolela ni Daktari mstaarabu sana na ni mwelewa sana anapoongea na wagonjwa.Namfahamu vizuri maana ndiye aliyekuwa anamtibu baba yangu na ndiye anayeendelea kuwatibu ndugu zangu zaidi ya watano akiwemo MAMA YANGU MZAZI.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad