HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 4 June 2018

Wizara yazindua mradi wa VVU na Ukimwi kwa Wasichana Balehe na Wanawake Vijana Nchini

Na Anthony Ishengoma Singida.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani Singida kwa lengo la kuutambulisha kwa jamii kuhusu wasichana na wanawake vijana walio shuleni na walio nje mfumo wa Elimu.

Mradi huu unatekelezwa na  Wizara pamoja na wadau wa Maendeleo kutoka AMREF, TAYOA, TASAF, TACAIDS na Mfuko wa Kimataifa wa Global Fund na wakati huu mradi uko katika hatua ya majaribio katika mikoa mitatu ya Tanzania ambayo ni Singida, Dodoma na Morogoro.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mradi huu mapema leo mjini Singida Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Marcel Katemba amesema kimsingi Wizara yake imepewa jukumu la kuandaa mazingira rafiki na wezeshi ya utekelezaji wa Mradi huu na ndiyo maana hatua ya awali ya maandalizi inaanzia kwa kujenga uwezo kwa wataalamu wa maendeleo ya Jamii kutoka mikoa ya majaribio ya mradi.

Aidha Bw. Katemba amesema Serikali ya Tanzania imepata ruzuku kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Global Fund kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya mapambano dhidi ya Maambukizi ya Virusi vya  Ukimwi Nchini  kwa kipindi cha January 2018 mpaka Desemba 2020.

‘’Maambukizi ya Ukimwi pamoja na mambo mengine yanachangiwa na tabia za Wasichana balehe na Wanawake vijana wenye umri wa miaka 10-24 kwa kujaribu kufanya mambo yanayotokana na mabadiliko ya miemko ya miili yao ambayo yanasababisha kujamiina na mahusiano ya kimapenzi yasiyokuwa salama.’’Alisema Kaimu Katibu Mkuu Marcel Katemba.

Aidha ameongeza kuwa mradi huu wa VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na Wanawake Vijana ambao utatekelezwa kwa Halmashauri 10 kutoka mikoa mitatu ya majaribio ambayo ni Manispaa ya Singida, Iramba, Halmashauri ya Singida, Dodoma, Bahi, Mpwapwa,Kongwa na Kondoa na kwa mkoa wa Morogoro mradi huu utaendelea kwa Halmashauri za Ulanga, Malinyi na Ifakara.

Wakati huo huo Naibu Meya wa Mkoa wa Singida Bi. Yagi Kiaratu amesema maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika Mkoa Singida bado ni Changamoto kubwa na kusema kuwa ujio wa mradi huu mkoani kwake utachangia kupunguza kuenea kwa virusi hivyo kwa wasichana balehe na wanawake vijana kwa kupunguza au kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Bi. Yagi ameongeza kuwa tatizo kwa wasichana wengi walio katika rika hili wanaingia katika janga la ukimwi kwasababu bado wanakuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu janga hili lakini pia wanakuwa hawajaanza kujitambua kama wako katika hatari ya kupata maambukizi ya ukimwi.

Jitihada za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi zimekuwa zikiendelea kwa kipindi cha miongo mitano lakini kwa kuwa tatizo hili changamoto kwa maendeleo ya Familia na Taifa serikali inaendelea kuokoa maisha ya watu hasa kwa vijana ambao ndio waathirika wakuu.
 Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Marcel Katemba  akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani Singida.
 Mkurugenzi wa Idara ya watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai akizungumza na wajumbe wa Mkutano wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani Singida.
 Naibu Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akitoa neno la shukrani kwa viongozi wa Wizara hawako pichani wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani Singida.
Uongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Taasisi za TASAF na TACAIDS na wadau wa maendeleo kutoka Amref na TAYOA wakiwa katika picha ya pamoja  wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani Singida. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad