HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 4, 2018

Njombe, Ruvuma kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, Septemba

Na Greyson Mwase, Makambako
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa amefurahishwa na utekelezaji wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako kilichopo mkoani Njombe.
Kalemani aliyasema hayo leo tarehe 03 Juni, 2018 mara baada ya kukamilika kwa ziara yake katika kituo ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Njombe na Ruvuma kwa ajili ya kukagua miradi ya usambazaji wa umeme nchini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Alisema kuwa, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea mapema mwezi Septemba mikoa ya Njombe na Ruvuma itaunganishwa rasmi na Gridi ya Taifa na kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Aliendelea kufafanua kuwa, kuingizwa kwa mikoa husika kwenye Gridi ya Taifa kutalipunguzia Shirika la TANESCO gharama kubwa inayotokana na matumizi ya mitambo ya mafuta mazito. 
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alielekeza kampuni  inayojihusisha na usambazaji wa umeme mkoani Njombe na Ruvuma ya Isolux kutoka Spain kuongeza kasi ya usambazaji ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika.
“ Haiwezekani wananchi wanakosa huduma ya nishati ya umeme wa uhakika kutokana na kusuasua kwa ukamilishwaji wa miradi ya umeme,” alisema Waziri Kalemani.
Awali akielezea utekelezaji wa mradi wa umeme wa Makambako – Songea, Meneja wa Mradi huo Mhandisi Didas Lyamuya alisema  lengo la mradi lilikuwa ni kujenga njia kuu ya usafirishaji  umeme wa msongo wa kV 220, yenye urefu wa kilomita 245 kutoka Makambako hadi Songea kupitia Madaba.
Alisema kazi nyingine zilizopo ndani ya mradi ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kupozea umeme vya Madaba na Songea Mjini pamoja na upanuzi wa kituo cha kupozea umeme cha Makambako, utandazaji  wa nyaya za mawasiliano, ujenzi wa njia za usambazaji wa umeme wa msongo wa kV 33 zenye urefu wa kilomita 900 na kuunganisha wateja 22,700 katika wilaya za Njombe na Ludewa na mji wa Makambako katika mkoa wa Njombe, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na Mbinga katika mkoa wa Ruvuma.
Mhandisi Lyamuya alifafanua kuwa, mradi ulianza rasmi upande wa usambazaji  umeme Desemba 2015 na unatarajiwa  kukamilika mwezi Desemba, 2018, mradi wa usafirishaji umeme ulianza Mei 2016 na kutarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu huku ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ulianza Septemba 2016 na kutarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Akielezea maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 220 Mhandisi Lyamuya alisema kazi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme imekamilika pamoja na ujenzi wa misingi yote 711 ya nguzo umekamilika.
Aliendelea kueleza kazi nyingine zilizokamilika kuwa ni pamoja na ufungaji wa nyaya kwa kilomita 238 kati ya kilomita 245 na kusisitiza kuwa kwa ujumla mradi umekamilika kwa asilimia 98.
Akielezea maendeleo ya ujenzi wa vituo vya kupoza umeme, Mhandisi Lyamuya alisema kuwa kazi za ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea zimekamilika kwa asilimia 85.
Akielezea hatua ya utekelezaji wa kazi ya usambazaji wa umeme katika mikoa ya Njombe na Ruvuma, Mhandisi Lyamuya alisema kuwa kazi  ya ujenzi wa njia za kusambaza umeme wa msongo wa kati wa kilovolti 33 na msongo mdogo wa kilovoti 0.4 mkoani Njombe  umekamilika kwa asilimia 61 ambapo jumla ya wateja 437 wameunganishiwa umeme kati ya lengo la kuwaunganishia umeme wateja 12,000.
Aliongeza kuwa jumla ya transfoma 43 zimefungwa na vijiji 16 vimepatiwa umeme kati ya 55 ambapo hatua mbalimbali za ujenzi zinaendelea.
Aliendelea kusema kuwa ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa kilovolti 33 katika mkoa wa Ruvuma umekamilika kwa asilimia 59 ambapo wateja 1210 wa awali wameunganishwa na huduma ya  umeme kati ya lengo la kuunganisha wateja 11,700 mradi utakapokamilika.
“Aidha ufungaji wa transfoma 37 umekamilika na vijiji 20 vimepatiwa huduma ya umeme kati ya vijiji 60 ambapo hatua mbalimbali za ujenzi zinaendelea, hivyo kwa ujumla ujenzi  kwa mikoa ya Njombe na Ruvuma umekamilika,” alisema Mhandisi Lyamuya.
Akielezea gharama za mradi, Mhandisi Lyamuya alisema mradi unatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida), Serikali ya Tanzania na Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO)
Alieleza kuwa, Serikali ya Sweden ilitoa jumla ya krona milioni 620 kati ya fedha hizo msaada ni  krona milioni 578 na za mkopo zikiwa krona milioni 42 huku Serikali ya Tanzania ikichangia jumla ya Dola za Marekani milioni 20 ambapo Tanesco ilichangia Dola za Marekani milioni saba na Serikali Dola za Marekani milioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa njia ya msongo wa kilovolti na vituo vitatu vya kupozea umeme.
Mhandisi Lyamuya aliongeza kuwa, Serikali ya Tanzania pia ilitoa kiasi cha shilingi bilioni saba kwa ajili ya ulipaji fidia kwenye laini kubwa ya msongo wa kilovolti 220
 Meneja Mradi wa Mradi wa Umeme wa Makambako-Songea, Mhandisi Didas Lyamuya (kulia mbele) akielezea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati mbele) mara alipofanya ziara katika kituo hicho Juni 03, 
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati mbele) akiendelea na ziara katika kituo cha kupoza umeme cha Makambako kilichopo mkoani Njombe Juni 03, 2018
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mbele) akiendelea na ziara ya ukaguzi wa kituo cha kupoza umeme cha Madaba kilichopo mkoani Ruvuma.
 Kituo cha Kupoza Umeme cha Makambako kama kinavyoonekana pichani

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad