HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 11 June 2018

WAZIRI PROF. MBARAWA ATOA MAAGIZO KWA BODI MPYA YA WAKURUGENZI TRC

Ni baada ya RAHCO, TRL kuunganishwa, 
azindua bodi ya wakurugenzi TRC 

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi mpya ya Wakurugezi wa Shirika la Reli Tanzania(TRC) kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge).
Amesisitiza ujenzi wa reli hiyo ni wa kihistoria nchini na baada ya kukamilika kwake itachukua miaka 100 kushuhudia tena ujenzi wa reli ya aina hiyo , hivyo ni fursa kwa TRC kuhakikisha wanapeleka wataalam wa kada mbalimbali kujifunza na kupata uzoefu.
Pia amesema ni wakati muafaka kwa bodi hiyo kuanza kuandaa watalaamu kabla ya kukamilika kwa ujenzi huo Novemba mwaka 2019 ikiwa ni pamoja waendeshaji wa mitambo.
Profesa Mbarawa amesema hayo leo Dar es Salaam wakati anazindua rasmi Bodi mpya ya TRC ambayo Mwenyekiti wake ni Profesa John Kondoro. 

Akizungumza na wajumbe wa bodi hiyo, Profesa Mbarawa amesema anatambua majukumu ambayo bodi hiyo wanayo katika kuhakikisha wanatekeleza vema majukumu waliyonayo hasa kipindi hiki ambacho ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea.
Hivyo ameitaka bodi hiyo kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo kwa karibu zaidi badala ya kuacha wajenzi peke yako.

Amesema siku za karibuni alifanya ziara saa sita usiku ya kwenda kuangalia ujenzi huo.Alifanya hivyo baada ya kupata taarifa hakuna usimamizi wa kutosha unaofanywa na TRC.
"Wakati naenda kwenye ile ziara kuna mtu alikuwa na taarifa hivyo akawaambia, bila hivyo nisengewakuta kule usiku.Hakikisheni mnausimamia ule mradi badala ya kukaa kando na kuacha wakandarasi peke yao,"amesema Profesa Mbarawa.
Pia amewasisitiza umuhimu wa kuanza kuandaa waendesha mitambo mapema kabla ya kukamilika kwa ujenzi.
"Haitakuwa vema mradi unakamilika halafu wanapewa watu wengine kuuendesha wakati Watanzania wapo na wakiandaliwa mapema wanaweza kuendesha mitambo kwa ufanisi mkubwa,"amesema.

Pia amesema maandalizi hayo yaende sambamba na upatikanaji wa vipuri ili isiwe kila kitu kinapoharibika kinaagizwa nje ya nchi.

Wakati huohuo ameitaka TRC kuhakikisha idadi ya mizigo na abiria inaongezeka kutokana na uwekezaji unaendelea kufanyika hasa kwa kuzingatia wamepewa vichwa vipya vya treni.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TRC Masanja Kadogosa amemuelezea Waziri changamoto na mafanikio ya shirika hilo huku akiahidi kuwa wataendelea kutoa huduma bora na kuongeza idadi ya abiria na mizigo inayosafiri kwa treni. Serikali imeamua kuziunganisha Shirika Hodhi la Reli(RAHCO) na Shirika la Reli Tanzania(TRL) na kupata TRC.

Kutokana na muunganiko huo wajumbe wa bodi hiyo wamehimizwa kufanya kazi kwa ushirikiano hasa kwa kuzingatia kabla ya hapo kila mmoja alikuwa na utamaduni wake wa kutekeleza majukumu yao.
 Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza wakati  akizindua bodi ya wakurugezi wa shirika la reli Tanzania (TRC) iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad