HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 1 June 2018

RC TABORA : WATENDAJI KUANZA ZOEZI LA UHAKIKI WA WATOTO WA KIKE WALIOHAMIA MIKOA MINGINE

Na Tiganya Vincent
WAKUU wa Wilaya na  Watendaji mkoani Tabora wametakiwa kuanza uhakiki  wa uhamisho wa  wanafunzi wote wa kike waliohama kutoka mkoani humo kwenda kwingine ili kujiridhisha kama kweli wanaendelea na masomo au walihamishwa ili wakaolewe.
Hatua hiyo inalenga kupata taarifa sahihi za watoto wa kike waliohamisha wakiwa darasa la nne na kuendelea hadi sekondari  kama kweli wanaendelea na masomo yao au walihamishwa ili wakawe wake za watu.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwenye ziara yake katika maeneo mbalimbali mkoani humo wakati akiendelea na kampeni ya operesheni komesha utoro, mimba  na ndoa za utotoni.
Alisema baadhi ya wazazi wakiona mtoto wao ambaye yuko shuleni amechumbiwa wamekuwa wakitumia mbinu hiyo chafu ya kudai wanahamishia mikoa mingine kwa ndugu zao ili wamuoze na kumkatisha masomo yake.
 “Nawaagiza anzeni kufuatilia watoto wote wa kike waliohama kuanzia mwaka 2015 walipokwenda kama kweli wanasomo…kama hawasomi warudisheni hapa ili nianze kufutilia nani aliyepata mpango huo ili nipambane naye…kama kuna mtumishi au mzazi alihusika nitamsomba mzima ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye kutaka kupanga mbinu hizo chafu” alisema Mwanri.
Alisema kuna wazazi au walezi kwa sababu wanajua kuwa hawawezi kwenda shule kusema kuwa wanamuomba mtoto wao akaolewe kwa sababu amepata mchumba wanachodai anahamia Kahama au Katavi kwa Shangazi yake au baba yake mtoto ili kuhalalisha uhamisho kumbe anaishia hapa katikati.
Mwanri aliwataka kutumia mifumo ya kiserikali iliyopo kuwasiliana na watendaji wa Mikoa au maeneo mengine ambayo wazazi wa watoto hao wanadai wamehamia ili kujua ukweli wa uhamisho huo isije ikiwa ni udanganyifu.
“Wewe Ofisa Elimu au Mkuu wa Shule unajua ni shule gani ambayo mzazi au mlezi wa mtoto alidai anamuhamishia mtoto wake…piga simu kwa Ofisa mwezako au Mkuu wa Shule ambayo mtoto alidaiwa kuhamisha ili kujua kama kweli yuko shuleni…kama hayupo peleka taarifa kwa Mtendaji wa Kata au Mkuu wa Wilaya ili mhusika akamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake” alisema.
Alisema anataka ifikapo mwakani Mkoa wa Tabora uwe wa kwanza kwa watoto ambao wanahudhuria shuleni na sio kwa utoro.
 Baadhi ya wakazi wa Miguwa wilayani Nzega wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora ( hayupo katika picha) jana wakati akiendelea na kampeni yake ya kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya na kukomesha utoro shuleni.
  Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoa wa Tabora Vedastus Kalungwani akitoa maelezo kwa wanaushurika wa Miguwa wilayani Nzega jana jinsi ya kujiunga na aina ya Bima ijulikanayo Ushirika Afya.
 Mkuu wa Wilaya ya Nzega Godfrey Ngupula akitoa maelezo jana wakati wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kupambana na utoro ambayo inaoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiendesha kampeni katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Nzega juu ya kupambana na utoro mashuleni na kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya. Picha na Tiganya Vincent

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad