HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 12, 2018

RC MAKONDA AKABIDHI KADI 220 ZA BIMA YA AFYA KWA WATOTO YATIMA NA WAISHIO KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

Na Zainab Nyamka, Globu ya jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam  Paul Makonda amekabidhi kadi 220 za Bima ya Afya (Toto Afya Card) zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 11 kwa watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu ili wapate uhakika wa matibabu mwaka mzima ikiwa ni sehemu ya Mwezi mtukufu wa Ramadhan. 

Makonda amekabidhi kadi hizo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwa kawaida Mwezi wa Ramadhan watu wamekuwa wakifuturisha watoto yatima lakini inakuwa ni chakula cha siku moja kwa hiyo katika mwendelezo wa mwezi mtukufu ameona ni vyema aguse maisha ya watoto yatima kwa kuwapatia Bima ya Afya.
Aidha  Makonda amesema kadi hizo zitawawezesha watoto kupatiwa matibabu Bure kwa kipindi cha mwaka mmoja katika Hospital yoyote hapa nchini.
Makonda amesema watoto waliopatiwa kadi hizo hawahusiani na wale waliojitokeza kwenye mchakato wa kutafuta haki ya mtoto ambapo ameshukuru Hospital ya Regency na TMJ kwa kujitolea kutoa kadi hizo.

Pia Makonda amesema atakabidhi pia mabegi 400 yaliyosheheni vifaa vyote vya Shule kwa vituo vya watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu ili wawe na uhakika wa kupata masomo mwaka mzima na kuweza kutumia vyema fursa ya elimu bure.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospital ya Regency Dk. Kanabar Rajni na Mkurugenzi wa Hospital ya TMJ  Parul Chhaya wamesema wameguswa kutoa msaada huo Kama sehemu ya kuunga mkono hamasa anayoitoa RC Makonda kwa wazazi kuwa na kadi za bima za afya (Toto Afya Card).
Meneja Masoko na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Bima ya Afya Nchini Angela Mziray amesema kuwa ugonjwa hauna muda kwahiyo kupatikana kwa kadi hizi kutasaidia sana waotot hawa kuwa na uhakika wa tiba pindi pale wanapopata maradhi na watatibiwa katika hospitali yoyote nchini.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utoaji wa kadi za bima ya Afya ( Toto Afya Kadi) kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu katika vituo vya kulelea watoto yatima Jijini Dar es Salaam.

Meneja Masoko na Elimu kwa umma NHIF Angela Mziray akizungumza na waandishi wa habari na kuwashukuru hospitali ya Regency na TMJ kuweza kulipia kadi za bima ya Afya kwa watoto 220 wanaoishi kwenye mazingira magumu Jijini Dar es Salaam.
 Moja ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu akifurahi baada ya kupatiwa kadi yake ya Bima ya Afya leo Jijini Dar es Salaam.
 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akiwapatia kadi za bima ya Afya (Toto Afya Kadi) watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu  zilizotolewa na hospitali ya Regency na TMJ leo Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad