HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 25 June 2018

Pacha walioungana Muhimbili kupelekwa Saudi Arabia kwa matibabu zaidi

Watoto pacha Maryness Benatus Bernado na Anisia Benatus Bernado waliozaliwa wakiwa wameungana ambao kwa sasa wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) tangu mwezi Februari mwaka huu, wanatarajiwa kupelekwa nchini Saudia Arabia ndani ya wiki mbili kuanzia sasa kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwemo kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha.

Hayo yameelezwa leo na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al-Hazzan alipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili kuangalia watoto hao. Watoto hawa wameungana kuanzia sehemu ya tumboni hadi chini.“Tumekuwa na uzoefu mkubwa sana wa kuwatenganisha watoto pacha waliozaliwa wakiwa wameungana kuanzia miaka ya 1990 ambapo hadi hivi sasa watoto zaidi 35 kutoka nchi mbalimbali duniani waliozaliwa wakiwa wameungana tulifanikiwa kuwatenganisha,” alisema Kaimu Balozi Al-Hazzan

Amesema kwamba kutokana na uzoefu mkubwa walionao, nchi yake kupitia Mfalme wa nchi hiyo ameagiza watoto hao wapelekwe Saudi Arabia kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya ubingwa wa juu.Mbali na hayo Serikali ya Saudi Arabia imesema itagharamia usafiri, malazi pamoja na matibabu hivyo wamemuhakikishia mama wa pacha hao kwamba matibabu yatakwenda vizuri na watarejea nchini wakiwa salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amemshukuru Mfalme wa Saudi Arabia na Serikali yake kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Serikali ya Tanzania hususani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.Prof. Museru ameiomba Serikali ya Saudi Arabia kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta ya Afya katika kuangalia maeneo yenye upungufu wa wataalamu pamoja na maeneo mengine zikiwamo huduma za upasuaji.

Kwa upande wake Mama wa watoto hao, Bi. Jonesia Jovitus amemshukuru Mfalme wa Saudia Arabia kupitia Ubalozi wake hapa nchini Tanzania kwa msaada alioupata kwani anaamini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu watoto wake watapata huduma ya matibabu kulingana na uzoefu ulipo nchini humo. Watoto hao kwa pamoja wana uzito wa kilo 7 na gramu 40, walizaliwa Wilayani Misenyi, Mkoani Kagera tarehe 29 Januari, 2018.
 Kaimu Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al-Hazzan akiwa na watoto pacha waliungana, Maryness Benatus Bernado na Anisia Benatus Bernado ambao wamebebwa na mama yao, Jonesia Jovitus. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru.Watoto hao wanatarajiwa kupelekwa nchini Saudia Arabia ndani ya wiki mbili kuanzia sasa kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwemo kuangalia uwezekano wa kuwatenganisha.
  Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru akimsikiliza balozi huyo kabla ya kuwatembelea wodini watoto pacha leo tarehe 25 Juni, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi wa ubalozi huo, Fahad Ali Al Qahtani.
 Kaimu Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al-Hazzan na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru wakielekea wodini kuwaona watoto pacha walioungana leo tarehe 25 Juni, 2018.
Kaimu Balozi wa Saudia Arabia nchini Tanzania, Bandar Abdullah Al-Hazzan na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Museru wakiwa katika picha ya pamoja leo tarehe 25 Juni, 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad