HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 30 June 2018

MWANAFUNZI CHUO CHA MAABARA SINGIDA AKIRI KUSAMBAZA ZA UONGO MATUMIZI YA PANADOL

*Ajisalimisha Mamlaka ya Chakula na dawa, awaomba radhi watanzania wote

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
MWANAFUNZI wa Chuo cha Maabara Singida, Elia Mhina amekiri kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu dawa aina ya Panadol kwamba si salama kwa matumizi ya binadamu.

Hatua ya mwanafunzi huyo ambaye aliambatana na mzazi wake Mchungaji Emmanuel Mhina jana katika Ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), ilitokana na jitihada za mamlaka hiyo za kumtafuta hadi walipomkamata.

Mhina ambaye anafanya mafunzo kwa vitendo Temeke, amesema alisambaza taarifa hizo alizozitafsiri kwa lugha ya kiswahili bila kufanya uchunguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mhina alisema alipokea taarifa za uvumi kutoka kwende video iliyotumwa kwenye kundi moja  la WhatsApp na kuifanya kuwa taarifa ya uhakika.

"Nilipokea video kweye kundi la Medical ambayo ilikuwa kwa lugha ya Kiingereza nami niliitafsiri kwa lugha ya Kiswahili na ndani ya siku tatu baada ya kuisambaza ilienea Tanzania nzima," alisema Mhina.

Pia alieleza kuwa aliamini taarifa hizo bila ya kufuatilia kitendo ambacho kimesababisha hofu kwa watumiaji wa dawa hiyo.

"Niwaombe radhi watanzania kwa ujumla, taasis na Kampuni ya Paracetamol kwa makosa niliyofanya ambayo kimsingi sio mazuri.

"Hivyo naahidi hata nikipata ajira nitakuwa mwaminifu pia niwasihi vijana wenzangu watumie vyema mitandao tusisambaze taarifa bila kujua ukweli wake," alisema.

Kwa upande wa Baba mzazi wa mwanafunzi huyo, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Avest Kibaha, Emmanuel Mhina alisema alipewa taarifa kuwa mtoto wake amefanya makosa ya mtandao kwakusambaza taarifa zisizo na ukweli na alikiri kufanya hivyo.

Alisema ni lazima watumiaji wa mitandao wawe makini na waangalifu kwani sio kila taarifa inatakiwa kusambazwa.

"Nawaomba vijana wajitawale na kuwa na mopaka katika kutumia mitandao ya kijamii kwani inaweza kubadili taswira ya kitu chochote. 

"Pia wazazi tunapaswa kuwafuatilia watoto wetu ili kujua viashiria vyovyote vinavyoweza kusababisha taharuki kwa jamii," alieleza Mchungaji Mhina.

Wakati  huo huo Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Fute alisema kitendo cha kusambaza uvumi ni kosa kisheria na kwamba likithibitishwa zipo adhabu mbalimbali ikiwemo kifungo jela au kulipa faini.

Fute alisema kwa mtu atakayebainika kutenda kosa hilo atatozwa faini ya kuanzia Sh laki moja hadi Sh milioni 10 au kifungo kisichopungua chini ya wiki mbili na kuendelea.

"Sayansi ya jinai inaelekeza kuwa mtu akikiri au kutambua kosa lake mbele ya umma inamaanisha kwamba kitu alichokifanya hakikuwa na nia ovu. Tumeangalia kitendo na nia ya kufanya kitendo hiki tumeona kuwahakuwa na nia ovu," alisema  Fute.

Pia aliwataka vijana kutumia somo hilo kuhakikisha wanatumia vyema mitandao ya kijamii na kwamba taarifa zozote zinathibitishwa na mamlaka husika.
 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Agnes Kijo akizungumza na waandishi habari kuhusiana na kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusu dawa aina ya Paracetamol inayojulikana kama Panadol kwamba si salama kwa matumizi ya binadamu uliofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
 Mwanafunzi wa Chuo cha Maabara Singida, Elia Mhina akizungumza na kuhusiana na kuhusika kusambaza taarifa za uongo za dawa aina ya Panado na kukiri kosa hilo kwa kuombaza msamaha kwa kile alicho kifanya katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria Mshauri wa TFDA, Iskari Fute akizungumza kuhusiana na sheria za kwa mtu anayesambaza taarifa za uongo katika masuala ya dawa na chakula Panado  katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad