HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 22, 2018

HOSPITALI MLOGANZILA WAJIANDAA KUTIBU SELIMUNDU KWA KUPANDIKIZA UTE WA MIFUPA

*Wazungumzia namna wanavyofanya tafiti, kutoa huduma bora

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MKUU wa Idara ya Hematolojia, Uwekaji wa Damu na Mtafiti Mkuu wa Program ya Selimundu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS) Profesa Jullie Makani amesema wapo katika mchakato wa kutoa huduma ya kutibu Selimundu kwa Kupandikiza ute wa Mifupa

Prof.Makani amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Selimundu Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Mlaganzila ambapo amesema kwa sasa wapo katika mchakato wa mazungumzo na yakikamilika wanatarajia kuanza kutibu Selimundu kwa kutumia tiba ya Kupandikiza Ute wa mifupa kwa mgonjwa.

"Zipo njia mbili zinazotumika kutibu Selimundu.Njia ya kwanza ni kwa kutumia Hydroxyurea na ndio ambayo tunaitumia hapa nchini.Njia ya pili ni ya kutibu kwa kupandikiza ute wa mifupa ambayo kitalaam inafahamika Bone Marrow Transplant,"amefafanua.

Alipoulizwa ni lini wataanza kupandikiza ute wa mifupa kwa mgonjwa wa Selimundu katika hospitali hiyo amejibu wanatarajia kuanza mwakani iwapo mchakato utakwenda vizuri hata.Pia amesema haijafahamika gharama ya kutibu kwa kupandikiza ute wa mifupa itakuwa kiasi gani na ndio mazungumzo ambayo wanaendelea nayo kufanya.

Amefafanua nchini India wanatibu Selimundu kwa njia ya kupandikiza ute wa mifupa kwa gharama ya Dola 60,000 na hivyo moja ya jambo ambalo wanalifanya ni kuzungumza na wadau mbalimbali ili watakapoanza kuitoa huduma hiyo gharama iwe yenye unafuu.

Alipoulizwa iwapo mgonjwa wa Selimundu anaweza kutibiwa na kupona kabisa Profesa Makani amejibu inawezekana kwa njia ya kupandikiza ute wa mifuko kwa mgonjwa huku akielezea jitihada mbalimbali zinazofanywa katka kutafiti ugonjwa huo na kutafuta tiba yake.

Kuhusu ugonjwa huo nchini amesema watoto 11000 kila mwaka wanazaliwa wakiwa na Selimundu na nchini kwa takwimu za Dunia zinaonesha watoto 300,000 kwa mwaka.Tanzania inashika nafasi ya nne kwa ugonjwa huo.

Ameeleza kuna tafiti nyingi ambazo zinafanywa na zinaendelea kufanywa na MUHAS katika kutafuta tiba ya ugonjwa huo.Pia wamekuwa wakiendelea kufanya tafiti kwa wanaougua ugonjwa huo.

Profesa Makani alipoulizwa mgonjwa mwenye Selimundu nini ambacho anakabiliana nacho, amejibu kuwa mgonjwa wa Selimundu anakabiliwa na maumivu makali ya mwili na kupungukiwa damu mara kwa mara.

Wakati huohuo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS)Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema pamoja na kufanya tafiti za Selimundu pia wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali huku akieleza kuwa wameamua Hospitali ya Mlongazila kuwa eneo la tafiti za magonjwa.

"Pamoja na kutoa taaluma ya tiba ya afya, tumekuwa tukijikita kufanya tafiti za magonjwa mbalimbali  na sasa Hospitali ya Mloganzila ni eneo ambalo litatumika kufanya tafiti hizo,"amesema.

Amefafanua wamejikita katika kutoa mafunzo, kuhudumia wagonjwa na kufanya tafiti , hivyo wanajivunia kwani wamekuwa wakifanya tafiti nyingi na zimeleta matokeo chanya.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Huduma za Hospitali Profesa Said Aboud ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kufika kwenye hospitali hiyo kupata huduma bora ambazo zinatolewa na madaktari bingwa na wabobezi.

Amesema wanatoa huduma ya kutibu magonjwa mbalimbali na wanayo maabara ya kisasa pamoja na vifaa tiba vya kutibu magonjwa mbalimbali.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MuHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Ugonjwa wa Seli Mundu yaliyofanyika kwenye Chuo Kikuu hicho Kampasi ya Mloganzila leo na kushirikisha Madaktari Bingwa, Watafiti wa Magonjwa na Tiba mbalimbali na wauguzi, Profesa Kamuhabwa amesema chuo hicho mpaka sasa ina miradi ya utafiti wa magonjwa mbalimbali pamoja na tiba inayofikia 92.
Profesa Julie Makani Mkuu wa Idara ya Hematolojia , Uwekaji wa Damu na Mtafiti Mkuu wa Programu ya Seli Mundu (MuHAS)akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Seli Mundu yaliyofanyika katika Chuo hicho Kampasi ya Moganzila leo.Profesa Julie Makani Mkuu wa Idara ya Hematolojia , Uwekaji wa Damu na Mtafiti Mkuu wa Programu ya Seli Mundu (MuHAS) akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Seli Mundu yaliyofanyika katika Chuo hicho Kampasi ya Moganzila leo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MuHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa katikati ,Profesa Julie Makani Mkuu wa Idara ya Hematolojia , Uwekaji wa Damu na Mtafiti Mkuu wa Programu ya Seli Mundu (MuHAS) kushoto na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Huduma za Hospitali Profesa Said Aboud wakifuatilia baadhi ya taarifa za tafiti zilizokuwa zikionyeshwa kwenye Projekta. 
Baadhi ya wataalamu na madaktari mbalimbali wakiwa katika maadhimisho hayo. 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Huduma za Hospitali Profesa Said Aboud akitoa shukurani zake wakati wa maadhimisho hayo mara baada ya kutolewa kwa taarifa mbalimbali za kiutafiti katika chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MuHAS) Profesa Appolinary Kamuhabwa katikati ,Profesa Julie Makani Mkuu wa Idara ya Hematolojia , Uwekaji wa Damu na Mtafiti Mkuu wa Programu ya Seli Mundu (MuHAS) kushoto na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Huduma za Hospitali Profesa Said Aboud wa pili kutoka kushoto pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Uzamivu (MuHAS) Emmanuel Balondya kushoto wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Madaktari Bingwa, Wataalam na Watafiti wa chuo hicho.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad