HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 31 May 2018

WIZARA, TAASISI ZA SERIKALI ZITUMIE NISHATI MBADALA – WAZIRI MKUU

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuzindua Maadhisho ya Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es salaam, Kate Kamba wakati alipowasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam kuzindua Wiki ya Mazingira, Mei 31, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na watatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhandisi Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu mkaa uliotengenezwa kutokana na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. katikati ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Kampuni ya  Space Engineering Limited, Bw. Philip Mtui kuhusu  mkaa uliotengenezwa kutoka na takataka na kufungashwa kwenye kiroba tayari kwa kuuzwa wakati alipotembelea banda la Kampuni hiyo kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Kulia kwake ni Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi, Evarest Ndikilo na kushoto ni Meneja Mauzo wa kampuni hiyo, Neema Matemba.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata Maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Edosama Hardware Limited, Edward Maduhu kuhusu bidhaa mbalimbali zinazotokana na miti ambazo zinatengenezwa na kampuni hiyo wakati alipotembelea mabada ya maonyesho kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Bibi Nimwagile Mwaijumba wakati alipotembelea banda la Kituo cha Utengenezaji magari cha Nyumbu  na kujionea mashine ya kutengeneza mkaa bora kwa kutumia takataka iliyobuniwa na kutengenezwa na kituo hicho. Waziri Mkuu alitembelea mabanda ya maonyesho  kabla ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Watatu kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba na wapili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Opwani Mhandisi, Evarest Ndikilo. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya JHS , David Mwendapole  wakati alipotoa maelezo kuhusu majiko makubwa yanayotumia  gesi kidogo  katika maonyesho ya Wiki ya Mazingira kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. Wanne kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam Mei 31, 2018. 
 Baadhi ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipowahutubia kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 31, 2018. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagana na viongozi baada ya kuzindua Wiki ya Mazingira kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mei 30, 2018. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala, Mwenyekiti wa CC wa Mkoa wa Dar es alaam, Kate Kamba,Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Matiku Makori  na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


*Aagiza viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wabadilike
*Ataka wasimamie wananchi waachane na matumizi ya mkaa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.

“Wizara, taasisi na mashirika yote ya Serikali na binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati mbadala ili matumizi ya mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”

Waziri Mkuu amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Ili kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.

“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.

“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”

“Meya ametoa fursa na amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni bajeti kupitia Mabaraza ya Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa teknolojia hii kwenye maeneo yenu. Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe watengeneze mashine nyingi zaidi na zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze kutumia teknonolojia hiyo kupikia,” alisisitiza.

Amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam wafuatilie kwa karibu usambazaji wa teknolojia hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali ya mazingira hapa nchini ni mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu waishio mijini.

“Hali ya mazingira nchini mwetu ni mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa sababu mahitaji yao yote wanayapata sokoni na madukani,” alisema.

“Wenzetu wa mikoani na vijijii wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba wanataabika kwa sababu kipato chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.  

Alisema mazingira yanafungamana na utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na kwamba maendeleo ya nchi pia yamefungamana moja kwa moja na mazingira. “Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini Tanzania, unatumika jijini Dar es Salaam,” alisema.

Waziri Makamba alisema taasisi za Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na shule zinaongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.

Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu kila siku.

“Chuo hiki kina migahawa tisa, kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna mgahawa mmoja mdogo unatumia magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo mkubwa unatumia magunia mangapi?” alihoji.

Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni siku ya kilele. Pia wiki nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na mjadala wa kitaifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad