HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 22 May 2018

WATENDAJI WATATU KITUO CHA UWEKEZAJI NCHINI WAFARIKI DUNIA

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

WATENDAJI watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC)  wakiwamo Wakurugenzi wawili na Meneja mmoja wamefariki dunia baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kupata ajali ya kugongana uso kwa uso na Scania katika Kijiji cha Msoga Chalinze mkoani Pwani.

Akizungumza na Michuzi Blog kwa njia ya simu leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Jonathan Warioba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusababisha vifo hivyo ambapo amesema  Zacharia Kingu na Martin Masalu ambaye ni Meneja wa Utafiti walifariki papo hapo wakati Said Amir alifariki dunia baada ya kufikishwa 
hospitali kwa matibabu.

Amefafanua ajali hiyo imehusisha magari mawili ambayo ni gari namba STK 923 aina Toyota Landcruiser mali ya Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji iliyokuwa ikiendeshwa na Priscus Peter(23) mkazi wa Dar es Salaam kugongana na scania namba T 620AQV/ T 407DBY.

"Mei 21 mwaka huu saa 15:30 maeneo ya Msoga-Chalinze katika barabara ya Msoga/Msolwa Wilaya ya kipolisi Chalinze Mkoa wa Pwani, gari hizo ziligongana na kusababisha vifo na majeruhi,"amefafanua Kamanda Warioba.

Ameongeza majeruhi katika ajali hiyo ni Godfrey Kilolo(45) na dereva Priscus Peter ambao walipelekwa Hospitali ya Msoga kwa matibabu na tayari wameruhusiwa na miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani.

Eneo la ajali hiyo kwa mujibu wa taarifa limekaguliwa na na  ASP. Solla-Occid(W) akisaidiwa na INSP.MS Mkojera - DTO (W) Chkojera pamoja na F7704 PC Hamza ambaye ndiye mpelelezi wa tukio hilo.Hata hivyo juhudi za zinafanyika kumpata dereva wa Scania kwa mahojiano zaidi kwani alikimbia baada ya ajali kutokea.

Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha  ajali ni uzembe  wa dereva wa gari namba STK 5923 T ambaye alihama kutoka upande wake na kwenda kugongana na Scania hiyo.
Pichani ni  gari namba STK 5923 aina Toyota Landcruiser mali ya Wizara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji iliyokuwa ikiendeshwa na Priscus Peter(23) mkazi wa Dar es Salaam kugongana na scania namba T 620AQV/ T 407DBY na kupelekea vifo na majeruhi. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad