Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Anne Makinda akisalimiana na mmoja
wa wananchi waliokuwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Na Grace Michael, Dodoma
WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kuwa na bima ya afya
kabla ya kuugua ili kuepukana na usumbufu wa kutafuta au kutumia
gharama kubwa za matibabu wakati wanapopatwa na magonjwa.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa
Taifa wa Bima (NHIF), Anne Makinda wakati akizungumza na wadau
kutoka Wizara zote Jijini Dodoma.
Amesema kuwa mwananchi anapokuwa na bima ya afya anakuwa na
uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote bila kujali kama
ana fedha ama hana ikilinganishwa na mwananchi ambaye hana bima ya
afya ambapo akiugua ni lazima aanze kutafuta fedha za kujitibia.
Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Anne Makinda akizungumza na Wadau wa Mfuko kutoka Wizara mbalimbali jijini Dodoma.
“Ni lazima ifike mahali watanzania tujenge utamaduni wa kuwa na bima ya
afya kabla ya kuugua, tunashuhudia namna wananchi wanavyopata shida
wakati wakiwa wamefikwa na maradhi hali inayosababisha wengine hata
kulazimisha kutumia njia za mkato au udanganyifu hivyo ili kuepukana na
matatizo haya ni vyema tukawa na huu utamaduni wa kukata bima ya afya
mapema,”alisema Mama Makinda.
Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John
Pombe Magufuli imewekeza fedha nyingi katika sekta ya afya kwa
kuhakikisha dawa, vifaa tiba na mahitaji yote katika vituo vya kutolea
huduma vinakuwepo ili mwananchi apate huduma kamilifu.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga akieleza mikakati ya Mfuko katika kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi wengi zaidi.
Kutokana na hayo, aliwataka wadau hao kushirikiana na Mfuko kwa karibu
kwa kutoa maoni ama ushauri wao kwa uwazi ili kuleta mabadiliko chanya
ya kihuduma kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea afya bora kwa wote.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema,
Mfuko umejipanga katika uboreshaji wa huduma zake ikiwemo taratibu
zinazowawezesha wananchi kujiunga na huduma zake.
Alisema kuwa, kwa sasa mfuko unaangalia uwezekano wa kumwezesha
mwananchi mmoja mmoja kujiunga na mfuko lakini pia utaratibu wa kulipa
fedha kidogo kidogo, taratibu ambao zitawawezesha wananchi wengi zaidi
kunufaika na huduma za mfuko.
“Tumejipanga na tumedhamiria kufikia mwaka 2020 ni lazima tuhudumie
wananchi wengi zaidi na kwa sasa tunajipanga kuzindua huduma
mbalimbali ambazo zinalenga kumnufaisha mwananchi wa kawaida
kabisa,”alisema.
Sehemu ya wadau wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi Mama Anne Makinda.
Akizungumzia suala la huduma bora, alisema mfuko umeweka mazingira
rafiki kwa watoa huduma kupata mikopo rahisi kwa ajili ya uboreshaji wa
huduma zao hususan vifaa tiba na uimarishaji wa miundombinu hatua
ambayo imewezesha upatikanaji wa huduma nyingi na bora kupatikana
nchini.
Alitumia mwanya huo pia kukemea tabia ya baadhi ya watoa huduma na
wanachama wasio waaminifu ambao kwa namna moja ama nyingine
wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya udanganyifu ambapo alisema
Mfuko hauko tayari kuona vitendo hivyo vikiendelea na badala yake hatua
kali zitachukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo.
Kwa upande wa wadau ambao ni Maofisa Waandamizi kutoka wizara zote,
waliupongeza mfuko kwa kazi kubwa ambayo umefanya ya utoaji wa
huduma na uwekezaji katika sekta ya afya ambao umesaidia huduma
nyingi za kitaalam ambazo awali hazikupatikana nchini kupatikana.
No comments:
Post a Comment