HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 31 May 2018

WALIOKAIDI KUHAMA KWENYE MAENEO YENYE MAFURIKO SAME SASA KUKAMATWA

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii,Kanda ya Kaskazini.


SERIKALI imetoa siku mbili kwa wananchi waliosalia katika Vijiji vya Ruvu Mferejini na Ruvu Marwa wilayani Same ,Mkoani Kilimanjaro vilivyozingirwa na maji kuondoka mara moja na kwamba watakao kaidi wataondolewa kwa kutumia nguvu na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Zaidi ya watu wapatao 2000 wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya kufikwa mafuriko kutokana na mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha huku eneo lililoathirika zaidi na mvua hizo ni ukanda wa tambarare wa wilaya ya Same unaopakana na Bwawa la Nyumba ya Mungu.

Licha ya Idadi hiyo ya watu kuyahama makazi yao lakini bado wapo waliokaidi kuondokana na hapa Serikali kupitia Mkuu wa wilaya ya Same ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya hiyo ,Rosemerry Senyamule ,ikatoa agizo.

Serikali imetenga maeneo kando ya milima iliyopo katika kitongoji cha Mferejini kwa ajili ya Kambi za Muda kwa watu waliokosa Makazi ,Clouds Habari imefika katika Kambi hizo na kujionea maisha mapya ya wahanga wa mafuriko huku misaada ya kibinadamu ikihitajika zaidi .
Licha ya kukosekana kwa baadhi ya huduma katika eneo hili bado wananchi hawa wanahitaji msaada wa hali na mali ili angalau kuweza kunusuru Maisha yao kutokana na Baridi kali ,Mbu na hata wanyama wakali wakiwemo Nyoka.

Katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi ,Aisha Amour ni miongoni mwa baadhi ya viongozi waliowatembelea wahanga wa mafuriko kwa ajili ya kutoa pole . 

Mafuriko katika vijiji hivi yanatajwa kuwa hutokea kila baada ya Miaka 10 na kwamba mara ya mwisho yalitokea mwaka 2008 huku chanzo kikitajwa kuwa ni kujaa kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu ambapo ujazo ulifikia Mita za ujazo 689.88 ambazo kwa sasa zimeanza kupungua hadi kufikia mita za ujazo 689.80 baada ya maji kuanza kuelekea kwenye maeneo ya makazi kwa kupitia mto Pangani.
Wananchi Jamii ya Massai pia ni miongoni mwa waathirika wa Mafuriko hayo.
 Eneo la Kitongoji cha Mferejini lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kuanzisha kambi kwa ajili ya Wahanga wa Mafuriko .
Wahanga wa Mafuriko wakianza ujenzi wa nyumba za Miti kwa ajili ya kujisitiri katika eneo la Ruvu Mferejini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad