HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 15, 2018

WAKALA WA MISITU TANZANIA WAZUNGUMZIA UMUHIMU WANANCHI KUTUNZA MITI YA MIKOKO

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) Profesa Dos Santos Silayo amesema ipo haja kwa Watanzania kuhakikisha wanatunza mikoko na kufafanua kuwa mikoko imekuwa ikichukua hewa ukaa mara 10 zaidi ya mimea mingine.

Ametoa kauli hiyo leo wakati wa upandaji miti ya mikoko katika eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam na kufafanua Wakala wa Misitu Tanzania wataangalia namna ya kufanya kwa kushirikiana na wadau wengine ili kwenye maeneo ya mikoko wananchi ambao wamekuwa wakiipanda na kuitunza mikoko kujipatia kipato kwa kufuga nyuki.

Pia Prof.Silayo amesema katika Taifa la Tanzania wanatoa msukumo wa kuifanya nchi kuwa kijani kwa kuendelea kuhifadhi maeneo ambayo yamehifadhiwa yaendelee kutunzwa, kupanda miti maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na miti na maeneo ambayo yalikuwa na miti na ikaharibiwa basi ni kupanda miti mingine huku akielezea pia kuitunza miti iliyopo.

"Kwa kufanya hivyo nchi itaendelea kuwa ya kijani kama ambavyo ilivyo kauli mbiu ya kuifanya dunia kuwa ya kijani ambapo kwa Tanzania kupitia Wakala wa Misitu Tanzania tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali ikiwamo ya kuhifadhi misitu iliyopo,"amesema.

Akizungumzia mikoko Prof.Silayo amefafanua ni furaha yake kwamba misitu ya mikoko ndio ya kwanza kuhifadhiwa ambapo ametoa historia kuwa ilianza kuhifadhiwa mwaka 1920 na kwa Tanzania ikaanza kuhifadhi miaka nane baadae.

Amesema nchi 121 duniani ndizo zenye mikoko na Tanzania ni ya tisa kwa kuwa na mikoko mingi ikitanguliwa na nchi ya Nigeria.

"Miti ya mikoko ina faida nyingi ikiwamo ya kusaidia kuzuia mmomonyoko kati ya bahari na nchi kavu. Robo ya watu duniani wanaishi karibu na bahari na hivyo mikoko husaidia kuepusha jamii hiyo kutoathirika na mawimbi ya mvua,"amesema Profesa Silayo.

Pia amesema faida nyingine ya mikoko inachukua hewa ukaa tofauti na misiti mingine na kuongeza asilimia 60 ya mizizi ya mikoko ipo aridhini , hivyo huifadhi Cabon nyingi.Pia asilimia 80 ya maeneo ya mikoko ndiko wanakopatikana samaki wengi.

"Mikoko iendelee kuihifadhiwa, pia kuhifadhi maeneo ambayo haijahifadhiwa,kupanda miti maeneo ambayo hajawahi kupandwa miti. Lazima tufahamu hifadhi ya mikoko ni mali ya Serikali.Pia Mawazo mazuri ya kusaidia kikundi hiki ni tukawasiliana hasa kwa kuizngatia hifadhi ya mikoko na misitu mingine ni mali ya Serikali,"amesema Prof.Silayo.

Kwa upande wa Rais wa Rotary Klabu ya Mlimani City jijini Dar es Salaam Dk.Eugene Kafanabo amesema moja ya shughuli wanazifanya ni kuisaidia jamii katika maeneo mbalimbali na hivyo wao wameamua wameamua kushiriki katika upandaji wa mikoko kwa lengo la kutunza mazingira.

"Kwetu sisi tumeamua kuchagua eneo la mikoko kwa kuungana na wananchi wa Mbweni kupanda mikoko na tutaendelea na utaratibu huu kwa kuwa tumejikita katika kusaidia shughuli za jamii,"amesisitiza.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake na Mazingira Mbweni jijini Dar es Salaam Husna Hussein amesema wamekuwa wakijishughulisha na upandaji na utunzaji mikoko kuanzia mwaka 1998 na wameona faida yake ambayo kubwa ni kutunza mazingira ya maeneo hayo ambayo yamepakana na fukwe ya Bahari ya Hindi.

Ametoa mwito kwa jamii kutunza mikoko kokote ilipo na kueleza kwa upande wao wameweka sheria ndogondogo kuwadhibiti waharibifu na atakayekamatwa hutozwa faini ya Sh.50,000.

Ameiomba Serikali kuunga mkono jitihada zao na kufafanua wamekuwa wakijitolea kwa kupanda miti hiyo wakiamini faida yake ni kwa jamii ya Watanzania wote hasa kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine mikoko huzuia mmomonyo wa ardhi.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Aqua-Farms Organization Jerry Mang'ena amesema wameamua kujikita katika upadaji mikoko kutokana na kutambua faida zake na kuiomba jamii ya Watanzania kuhakikisha wanatunza miti hiyo huku akielezea kwa Tanzania inaelekea kweye ujenzi wa viwanda,hvyo uwepo wa mikoko ni muhimu zaidi.

Pia amesema kutokana na juhudi za kupanda mikoko wanaangalia namna ya kuanza kuvuna hewa ukaa na kuiuza kwa kampuni kubwa zenye viwanda na kusisitiza wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakimo Wakala wa Misitu Tanzania katika kupanda mikoko na kuitunza.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo akizungumza leo wakati wa upandaji miti uliofanyika katika eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka , Globu ya jamii)
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu, Profesa Dos Santos  Silayo (wakwanza kulia alievaa kofia)  pamoja na wadau mbalimbali  wa Mazingira wakipanda miti katika eneo la Mbweni jijini Dar es Salaam.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu, Profesa Dos Santosa Silayo akimsikiliza Mwenyekiti wa Kikundi cha Wanawake na Mazingira Mbweni, Husna Hussein wakati akielezea upandaji wa miti ya mikoko ambayo wamekuwa wakipanda tangu mwaka 1998.
 Upandaji wa miti ya mikoko ukiendelea katika eneo la Mbweni Jijini Dar Es Salaam
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad