HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 24 May 2018

‘VITA’ SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI YAZINDULIWA DODOMA

Na Ramadhani Juma, Ofisi ya Mkurugenzi
ZOEZI la utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake limezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma huku wasichana waliopatiwa chanjo hiyo wakitoa wito kwa wenzao kujitokeza na kuhakikisha wanakingwa dhidi ya ugonjwa huo.
Uzinduzi huo umefanyika jana katika ukumbi wa Dodoma Sekondari ambapo mgeni rasmi katika hafla fupi ya uzinduzi huo alikuwa Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi huku Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea akimwakilisha Mkurugenzi Godwin Kunambi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya alisema uzinduzi huo ni kiashiria cha kuwafikia Wasichana wote wenye chini ya umri wa miaka 14 ndani ya Wilaya ya Dodoma.
Alisema zoezi hilo litaendeshwa na Halmashauri kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu, na litashirikisha viongozi wa ngazi zote ikiwemo Kata na Mitaa ili kuhakikisha kila msichana anayehusika anafikiwa na kupatiwa chanjo hiyo.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea alisema katika kipindi cha Mwaka mmoja ujao, jumla ya Wasichana 7,828 walio na umri wa chini ya miaka 14 wanatarajiwa kufikiwa na kupatiwa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma.
Alisema  baada ya miezi sita Wasichana wote waliopatiwa chanjo hiyo watapatiwa tena kwa awamu ya pili ili kukamilisha kinga yao dhidi ya virusi vinavyoeneza ugonjwa huo.
Alimweleza Mgeni rasmi na wajumbe kuwa, chanjo hiyo imethibitishwa na Shirika la AfyaDuniani (WHO) hivyo Wasichana na Wazazi wasiwe na mashaka badala yake watoe ushirikiano wa kutosha ili kufikia lengo la Serikali la kutokomeza ugonjwa huo kama ilivyofanya kwa magonjwa kama Polio.
 Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamadi Nyembea akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wasichana walio chini ya umri wa miaka 14 katika Wilaya ya Dodoma jana. Katikati ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi na wa kwanza ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dodoma palikofanyika uzinduzi huo Mwalimu Amani Mfaume.  
 Muhudumu wa Afya Ruth Azaliwa akimchoma Sindano ya chanjo dhidi ya Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake Mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash kuashiria uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma jana. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kushoto) na Mwalimu wa Afya wa Shule hiyo Caritas Burchard (kulia).
 Zoezi la utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wasichana walio chini ya umri wa miaka 14 likiendelea katika Sekondari ya Dodoma mara baada ya kuzinduliwa rasmi na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi.
 Mwanafunzi wa Kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash akionesha kadi yake aliyokabidhiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi (kushoto) kama ishara ya uzinduzi rasmi wa utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wanawake. Kadi hiyo itamuwezesha kupata chanjo hiyo kwa awamu ya pili baada ya miezi sita ili kukamilisha kinga yake dhidi ya ugonjwa huo. Wengine wanaoshuhudia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamadi Nyembea (mwenye miwani katikati nyuma)  na Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Amani Mfaume (mwenye miwani katikati mbele). Kushoto ni Mwalimu wa Afya wa Shule hiyo Caritas Burchard.
 Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi akimkabidhi kadi maalum kwa ajili kupata huduma ya chanjo awamu ya pili dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya kizazi kwa Wanawake Mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari ya Dodoma Huda Khalid Rabash kama ishara ya uzinduzi wa zoezi la utoaji wa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma jana katika ukumbi wa Shule hiyo.  
Sehemu ya Wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari ya Dodoma wakifuatilia shughuli ya uzinduzi wa utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi  uliofanyika katika Shule hiyo jana. Picha na Ramadhani Juma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad