HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 18, 2018

USHAHIDI KESI MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA INAYOMKABILI TIDO MHANDO KUSIKILIZWA JUNI 8

Na Karama Kenyunko, Blogu ya jamii

USHAHIDI dhidi ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando  utaendelea kusikikizwa Juni 8,mwaka huu.

Kesi hiyo ambayo ilikuwa iendelee kusikilizwa kwa shahidi wa nne wa upande wa mashtaka kutoa ushahidi wao, imeahirishwa sababu shahidi waliyemtarajia kutoa ushahidi Katika kesi hiyo anaudhuru.

Hayo yameelezwa na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai,  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu , Huruma Shaidi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 8 mwaka huu ambao mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi.

Katika kesi hiyo tayari mashahidi watatu  wamekwishatoa ushahidi wao ambao ni Afisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Clement Mshana.

Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.milioni 887. 
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Juni 16, 2008,   akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido aliyekuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBCli hasara ya Sh.887,122,219.19.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad