HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 22 May 2018

UBA YAJIVUNIA MAFANIKIO YAKE, YAAHIDI HUDUMA BORA ZA KIBENKI NCHINI

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
UONGOZI wa United Bank for Africa(UBA) umesema umejipanga kuendelea kutoa huduma bora za kifedha kwa Watanzania huku ukifafanua kukua kwa teknolojia kumeifanya benki yao kutoa huduma zake kwa njia ya mtandao na kuwafikia wateja wengi zaidi.

Pia umeeleza mikakati yao katika kuhakikisha wanashiriki kuleta maendeleo nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano.Pia umewahimiza wananchi umuhimu wa kuwa na Kitambulisho cha Taifa kwani vinarahisisha kwa wanaohitahi kufungua akaunti benki.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na uongozi wa UBA wakati wanazungumza na waandishi wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio, malengo na mikakati yao katika utoaji wa huduma za kibenki nchini. Pia UBA umekutana na wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM).

Mtendaji Mkuu wa UBA nchini Tanzania Chris Byaruhanga ,amesema tangu kuanzishwa kwa benki hiyo miaka 75 iliyopita nchini Nigeria na kufungua matawi katika nchini mbalimbali ikiwemo Tanzania wamepata mafanikio makubwa na benki hiyo imekuwa chachu ya maendeleo katika Bara la Afrika.

Amefafanua kwa Tanzania UBA imeendelea kujiimarisha katika kutoa huduma bora za kibenki na imekuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za kimaendeleo na kubwa zaidi uwepo wa benki hiyo umesaidia kutoa ajira kwa Watanzania.

"Hivi karibuni tunatarajia kwenda kufungua tawi Mjini Dodoma, tunatambua Makao Makuu ya Serikali yamehamia huko nasi lazima twende kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.Hivyo tawi hilo litakapofunguliwa litahitaji watu wa kuwaajiri ambao nao watakuwa Watanzania,"amesema.

Kwa upande wa Mkuu wa Mahusiano ya ndani wa UBA Kanda ya Afrika Nasir Ramon, amesema UBA inatoa huduma zake katika nchi 20 za Bara la Afrika na ndio benki pekee ya Afrika ambayo ipo Marekani, Uingereza na Ufaransa.

Amesema UBA ina mtaji wa Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 12, na hivyo kujidhatiti katika utoaji wake wa huduma katika nchi yoyote. Amesema malengo mengine ya benki hiyo nchini ni kuhakikisha inaongoza kwa wateja huku akisisitiza usalama wa fedha za wateja wao ni mkubwa.

Amehimiza Watanzania kuchangamkia fursa zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo ya utoaji mikopo yenye riba nafuu na kupongeza jitihada za Serikali zinazozungumzia kuwa na benki imara na zenye tija kwa wateja.

Wakati huo huo Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Brendansia Kileo, amewataka wananchi kujitokeza na kujiunga na benki hiyo ili wanufaike na huduma za kifedha wanazotoa.

Wakiwa IFM uongozi wa UBA umetumia nafasi hiyo kuzungumza mambo mbalimbali yanayohusu benki yao ambapo wanafunzi hao waliwapata nafasi ya kuuliza maswali na kupata majibu.
Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Brendansia Kileo (kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumzia mipango mbalimbali ya UBA. Wengine ni Mkuu wa Mahusiano ya ndani na nje wa UBA Nasir Ramon(kushoto) na Mtendaji Mkuu wa UBA nchini Tanzania Chris Byaruhanga(katikati).
Mtendaji Mkuu wa UBA nchini Tanzania Chris Byaruhanga (katikati) akizungumzia mafanikio ya benki hiyo kwa waandishi wa habari nchini.Kulia ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Brendansia Kileo na Mkuu wa Mahusiano ya ndani na nje wa UBA Nasir Ramon(kushoto)
Mkuu wa Mahusiano ya ndani na nje wa UBA Nasir Ramon (kushoto)akizungumzia mchango wa benki hiyo katika kuchangia maendeleo ya nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.Kati kati ni Mtendaji Mkuu wa UBA nchini Tanzania Chris Byaruhanga na kulia ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki hiyo Brendansia Kileo
Mmoja ya maofisa wa UBA akielezea ubora wa kadi ya benki hiyo kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM) leo jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad