HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 25, 2018

TCRA WATOA LESENI KWA WATOA HUDUMA ZA HABARI MTANDAONI

*Mkurugenzi TCRA asema 45 ndio wamekidhi vigezo kati ya waombaji 262
*Asema mchakato bado unaendelea, atoa sababu kuweke gharama za usajili

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MAMLAKA ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania(TCRA)imesema leo ni siku muhimu katika tasnia ya habari na utangazaji kutokana na kushuhudiwa wadau wa habari wakiwa wamekamilisha hatua za usajili ili watambulike na kutumia fursa hiyo ya utoaji na upashaji habari kupitia mtandao wa intanenti.

Kutokana na kukamilisha mchakato huo TCRA imetoa leseni kwa watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao wa intanenti 45 kati ya watoa huduma 262 walioomba na kushindwa kutimiza vigezo vilivyowekwa.Miongoni mwa waliopewa leseni baada ya kukamilisha taratibu hizo ni pamoja na Michuzi Media Group(MMG)

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandisi James Kilaba wakati akikabidhi cheti cha usajili kwa wamiliki 45 wa Blogs, Redio na televisheni za mtandaoni na kusema kuwa zipo faida nyingi za habari na utangazaji kwa njia ya mtandao ambazo zinafahamika kwa wengi.

"Kama tunavyofahamu kwa miongo mingi sasa sekta ya habari na utangazaji imekuwa ikipata habari kwa njia ya redio na televisheni kupitia majukwaa mbalimbali kama mitambo iliyojengwa ardhini,Satellite na Cable.

"Baadae kwenye miaka 2000 teknolojia ya intaenti iliingia ingawa matumizi yake yalikuwa kwa ajili ya mawasiliano ya kawaida kama vile barua pepe bila kujumuisha matumizi ya vyombo vya habari (online media service),"amesema.

Ameongeza ujenzi wa mkongo wa Taifa nchini unaotumia "optic fiber" na matumizi ya teknolojia ya 4G vimechangia ongezeko la kasi ya usafirishaji wa taarifa ya vyombo vya habari (broadband) na kuwezesha matumizi ya habari mitandaoni.

Ameeleza kuanzia mwaka 2013 Watanzania wameshuhudia kuongezeka kwa kasi kwa vyombo vya habari mtandaoni hata kuleta mvuto wa pekee kwa wananchi wengi na kupelekea fursa kwa kila mmoja na kuleta mapinduzi chanya kwenye sekta ya habari na utangazaji hasa kwa wanaoitumia vema.

"Zipo faida nyingi za habari na utangazaji kwa njia ya mtandao ambazo zinafahamika.Mojawapo kubwa ni kutoa fursa ya ajira kwa wengi hasa vijana. ambapo baadhi yenu hii imekuwa chanzo cha mapato kwa ajili ya kurahisisha maisha.Faida nyingine ni upatikanaji wa habari kwa haraka hasa za matukio mbalimbali yanayotokea miongoni mwa jamii,"amesema.

Amefafanua matumizi bora au mabaya ya mawasiliano yanaweza kufanyika kwenye majukwaa hayo ikiwa hayatakuwa na utaratibu mzuri uliowekwa kuhusu maudhui. Hivyo ni kwa ajili hiyo Serikali imeendelea kuwa na sheria na kanuniz zinazosimamia majukwaa hayo ambayo yamekuwa yakitumika na yanayoendelea kutumika ili kuhakikisha kuna matumizi bora na salama kwenye tasnia ya habari na utangazaji kwa watoa huduma na watumiaji.

"Hali kadhalika kwasababu zile zile mawasiliano kwa njia ya mtandao kwa vyombo vya habari nayo yanatakiwa kuwa yanatumika vema ili kuwa na matumizi bora na salama. "Ni matumaini yangu wote tunakiri na kuona haja ya majukwaa haya yanakuwa na utaratibu mzuri kupitia sheria na kanuni .Hivyo usimamizi wa matumizi bora ya majukwaa haya ni muhimu bila kubagua kwa vile yote yanabeba maudhui kwa ajili ya mawasiliano,"amesema.

Amefafanua kwa kuzingatia umuhimu huo Serikali ikaandaa kanuni za maudhui mtandaoni za mwaka 2018 zilizoanza kutumika Machi mwaka 2018 na kuongeza kanuni nne inaipa uwezo TCRA kufanya mambo muhimu matatu. Ameyataja ni kutuza rajis ya wanablogu , majukwaa ya habari mtandaoni , redio na televisheni mtandaoni.Pia kuchukua hatua dhidi ya wakiukaji wa kanuni hizo ikiwemo kuagizwa kuondolewa kwa maudhui yaliyokatazwa na kuelimisha umma kuhusu salama ya maudhui mtandaoni.

Mhandisi Kilaba amesema katika kutekeleza matakwa ya kanuni hizo za maudhui mtandaoni za 2018 wamekamilisha taratibu rahisi za kuwasilisha maombi ya usajili tangu Aprili 21 mwaka huu na hivyo kuwezesha mwanzo wa kuwa na rajis endelevu ya wanablogu, majukwaa ya habari mtandaoni ,redio na televisheni mtandaoni. Amesema kuongezeka kwa orodha ya wanaotambulika itakuwa chachu kubwa katika ushirikiano wa kuhabarisha na kuelimisha umma. Pia amesema usimamizi wowote wa sekta una gharama zake ili kuhakikisha kuwa huduma inayotolewa inakidhi matarajio ya watanzania wengi.

Amesema gharama zilizopo zinalenga kuzuia uanzishwaji holela wa vyombo vya habari mtandaoni usiokidhi viwango vinavyotakiwa, kuleta ushindani sawa wa vyombo vya habari na kutambua watu wenye nia safi ya kutoa huduma hiyo ya maudhui mtandaoni kwa jamii. "Naomba nitumie fursa hii kuwakumbusha kwamba si nchi yetu ya Tanzania pekee iliyokumbwa na changamoto za matumizi na habari salama mitandaoni kisha kuchukua hatua.Huko duniani hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa kulingana na tamaduni, mila ,desturi na mahitaji ya nchi husika.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akizungumza wakati wa utoaji wa leseni kwa watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao , iliyofanyika leo  katika ukumbu wa TCRA jijini Dar es Salaam.
 Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Blogers , Krants Mwantepele akizungumza kuhusiana na mwitikio ulionyeshwa kwa wamiliki kujisajili TCRA iliyofanyika , jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akikabidhi  leseni kwa  watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao kwa Mmoja wa Wakurugenzi wa Michuzi Media Group (MMG), Ainde Ndanshau katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa TCRA , jijini Dar es  Salaam.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akikabidhi  leseni kwa  watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao kwa Mkurugenzi wa Blogu ya Wananchi , William Malecela ‘LE MUTUZ ‘ Vkatika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa TCRA , jijini Dar es  Salaam
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akikabidhi  leseni kwa  watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao kwa Mwakilishi wa  Mtandao wa Bongo 5, Yassin Ng’itu katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa TCRA , jijini Dar es  Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akikabidhi  leseni kwa  watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao kwa Mmiliki wa Habari Mseto , Francis Dande katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa TCRA , jijini Dar es  Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA),  Mhandisi James Kilaba akikabidhi  leseni kwa  watoa huduma wa maudhui kwa njia ya mtandao kwa  Mmiliki wa Radio Seven ya Mtandaoni,  Atu Mandoza katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa TCRA , jijini Dar es  Salaam.
 Baadhi ya waandishi na wamiliki wa watoa huduma kwa njia ya mtandao

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad