HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 31, 2018

SPIKA NDUGAI AFUNGUA MAONESHO YA MADINI BUNGENI DODOMA

Na Veronica Simba
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, leo Mei 30, amefungua rasmi maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma na kuipongeza Wizara ya Madini kwa kuyaandaa.
Akitoa hotuba ya ufunguzi, Ndugai alimpongeza Waziri mwenye dhamana, Angellah Kairuki pamoja na watendaji wa Wizara, kwa juhudi kubwa za kutangaza na kulinda rasilimali ya madini hapa nchini. Alisisitiza kuwa, anatumaini juhudi hizo zitaendelezwa ili kuiwezesha sekta husika kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa letu.
Alisema kwamba Wizara ya Madini inalo jukumu kubwa la kuufahamisha umma kuhusu sekta husika kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari na maonesho mbalimbali.
“Maonesho haya yamekuja wakati muafaka kwa sababu kipindi hiki nchi yetu iko katika mageuzi makubwa katika sekta ya madini; na ninyi wizara mnawajibika kuifanikisha azma hii kwa njia mbalimbali, hususan vyombo vya habari na maonesho kama haya.”
Aidha, Spika aliwataka wadau mbalimbali wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ikiwa ni pamoja na usalama wa wafanyakazi wao na kulipa kodi za Serikali.
Kuhusu suala la uongezaji thamani madini kabla ya kuyauza, Ndugai alisema kwamba hilo ni suala muhimu sana kwa kuzingatia sera ya nchi ya kuwezesha uchumi wa viwanda. “Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tutajenga viwanda ambavyo vitatoa fursa ya ajira kwa watanzania na kuinua uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.
Akizungumzia mchango wa Bunge katika kukuza sekta ya madini, alisema Bunge limekuwa makini katika kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta husika unakuwa wenye tija na manufaa kwa pande zote; yaani Serikali, Taifa na wawekezaji.
“Tuliunda Kamati mbalimbali za ufuatiliaji wa sekta ya madini. Nafurahi kuwaambia kwamba mambo yamekuwa yakiboreka siku hadi siku. Nawasihi tuendelee hivyohivyo kwa manufaa ya pande zote.”
Awali, akimkaribisha Spika kufungua maonesho husika; Waziri Kairuki alisema kuwa, Wizara imeandaa maonesho hayo kwa kuzingatia kuwa ni Wizara mpya hivyo inahitaji kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake; yakijumuisha dhima na dira.
“Baada ya Bunge lako tukufu kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini Namba 14 ya Mwaka 2010, kupitia marekebisho ya Sheria Namba 7 ya Mwaka 2017, Wizara yangu imekuwa na jukumu kubwa la kutekeleza maelekezo ya Sheria hiyo.”
Maonesho hayo ya siku tatu, yaliyoanza Mei 30 na kutarajiwa kuhitimishwa Juni Mosi; yameshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Wachimbaji Wakubwa (TCME) na Kampuni zinazojishughulisha na uchimbaji na uongezaji thamani madini.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akitoa hotuba ya ufunguzi rasmi wa maonesho ya madini katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Wengine pichani (kutoka kulia), ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai (katikati), akiangalia aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini, alipotembelea Banda la Chuo cha Madini (MRI) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu.
 Mjasiriamali anayejishughulisha na uongezaji thamani madini kwa kutengeneza na kuuza bidhaa mbalimbali za urembo, Susie Kennedy (mwenye blauzi nyeupe), akimwonesha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, moja ya bidhaa anazotengeneza kutokana na madini; wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Kushoto ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, akiangali bidhaa zinazozalishwa na Kampuni ya Tancoal, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya madini kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Mei 31 mwaka huu. Pamoja naye pichani ni Waziri wa Madini Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof Simon Msanjila na Kamishna wa Madini Prof Shukrani Manya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad