HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 18, 2018

Serikali Yaandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa vitendo kwa Wahitimu wa Vyuo

Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Serikali imeandaa mwongozo wa Kitaifa wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo ili kuondoa pengo la ujuzi linalohitajika katika soko la ajira hapa nchini.

Hayo yamesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Antony Mavunde alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Zainab Athuman Katimba  juu ya Serikali haioni haja ya kutungwa sera ya mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu wa Elimu ya Juu na Vyuo vya Ufundi (Internship Policy for Higher Learning Institutions and Technical Colleges Graduates) ili vijana waweze kupata ujuzi utakaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

"Katika kuhakikisha pengo la ujuzi (skills gap/skills mismatch) kati ya ujuzi walionao wahitimu na ule unaohitajika katika soko la ajira, ni kweli Serikali imeona kuna haja ya kuwa na miongozo ya kisera ambapo kupitia Ofisi yangu tumeandaa mwongozo wa Kitaifa wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu (National Internship Guideline)," amesema Mhe. Mavunde.

Ameendelea kusema kuwa mwongozo huo ulizinduliwa rasmi Septemba, 2017 na kuanza kutumika rasmi ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 zaidi ya nafasi 750 zimetolewa na waajiri mbalimbali kuwezesha wahitimu kufanya mafunzo.

Aidha amesema, Serikali inafanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kuendana na mahitaji ya sasa ambapo sera mpya pamoja na mkakati wa utekelezaji wake iko katika hatua za mwisho na inatarajiwa kukamilika ifikapo Juni mwaka huu.

"Miongoni mwa matamko mahususi ya sera hii ni pamoja na kusisitiza kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu wa vyuo. Baada ya kupitishwa sera hii, suala la mafunzo ya vitendo kazini kwa wahitimu litawekwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.

Hata hivyo, Mhe. Mavunde ametoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa programu ya mafunzo kazini kwa wahitimu kwa kutoa fursa kwa vijana wahitimu kujifunza katika maeneo yao ya kazi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad