HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 29, 2018

SEKTA YA FEDHA YATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU KATIKA UTOAJI WA MIKOPO

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
SERIKALI imeitaka Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda na kilimo pamoja na wajasiriamali wadogo.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, katika Mkutano wa wadau wa Sekta ya Fedha uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu wa Taasisi za fedha na Wizara ya Fedha na Mipango.

Prof. Luoga alitoa wito huo kufuatia kuwepo kwa changamoto katika Sekta hiyo ikiwemo  ukosefu wa uwekezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo katika viwanda, kilimo na miundombinu pia  ukosefu wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

“Kuna kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo, gharama kubwa za huduma za fedha, mifumo hafifu ya kuwalinda  watumiaji wa huduma za fedha, ukosefu wa elimu ya fedha kwa wananchi na wananchi wengi kutofikiwa na huduma za fedha ambapo ni asilimia 8.6 tu ya nguvu kazi ya wananchi waishio vijijini wanapata huduma za benki ikilinganishwa na asilimia 32.1 ya nguvu kazi kwa wanaoishi mijini” alisisitiza Prof Luoga

Gavana huyo wa Benki Kuu alisema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali ilifanya maboresho ya Sekta ya Fedha  katika eneo la ubinafsishaji wa benki za Serikali kurekebisha na kutunga sera na sheria mbalimbali hadi kufikia Desemba, 2017 ili kuweka misingi imara ya kuwezesha ukuaji, ushindani na ufanisi katika sekta ya fedha.

“Maboresho ya Sekta ya Fedha yamesaidia ongezeko la idadi ya benki na taasisi za fedha kufikia 54, kampuni za bima 31, kampuni zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa 27, taasisi za huduma ndogo za fedha takriban 450, mifuko na program za Serikali 34, vikundi vya kifedha vya kijamii takribani 30,019 katika mikoa 18 ya Tanzania bara na uanzishwaji wa soko la bidhaa” alieleza Prof. Luoga.

Alisisitiza kuwa taasisi za fedha zikitimiza wajibu wake, sekta binafsi itakuwa na uwezo wa kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa na kupunguza umasikini wa kipato wa wananchi.

Aidha Serikali katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi, inaandaa Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha, unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha, kulinda watumiaji wa huduma za fedha, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, uthabiti wa sekta ya fedha, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya fedha, kudhibiti utakasishaji wa fedha haramu na kuweka mazingira wezeshi ya sheria, kanuni na taratibu katika sekta hiyo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Doto James, alisema kuwa  azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa nchi  unaongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. 

“Kuwepo kwa viwanda vingi italeta ongezeko la ajira kwa wananchi walio wengi pamoja na kuiongezea Serikali mapato” alieleza Dkt. Kazungu

Aidha, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo, ni lazima wapate rasilimali fedha kutoka kwenye taasisi  kama vile benki na masoko ya mitaji hivyo watoa huduma kwenye taasisi hizo wanapaswa kuongeza ubunifu kwenye utoaji wa huduma zinazokidhi mahitaji ya wapokeaji huduma kulingana na shughuli wanazofanya na kwa gharama nafuu. 

Alizitaka taasisi za fedha kuwekeza katika kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia taasisi hizo kwa kujiwekea akiba na kupata mitaji itakayowezesha kukuza biashara na shughuli zao za kiuchumi hivyo wadau wa sekta ya fedha wanapaswa kujiuliza ni kwa nini mikopo ya biashara kwenda kwenye sekta binafsi hairidhishi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora aliwataka wadau wa sekta ya fedha kuzungumzia mafanikio ya Sekta ya fedha kwa njia ya miamala ya Simu za mkononi kwa kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa Duniani katika eneo hilo na hivyo kuwa mfano kwa mataifa mbalimbali.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Elisante Ole Gabriel ameitaka Sekta binafsi inayonufaika na mikopo inayotolewa na taasisi za fedha kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kulipa mikopo yao kwa wakati pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa wanazozalisha na kuongeza kiwango cha mauzo ya bidhaa hizo nje ya nchi,
 Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maria Kangoye (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mkutano kati ya  wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga (katikati), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (kulia), na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora (kushoto), wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei, akisikiliza kwa makini wito wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga (hayupo pichani) kuhusu Sekta ndogo ya Benki kuongeza ubunifu kwa kutoa mikopo ya muda mfupi na mrefu ambayo itawezesha ukuaji wa sekta za viwanda, Jijini Dodoma.
 Baadhi ya wakurugenzi wa taasisi za fedha na maafisa waandamizi wa Serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakisikiliza maelezo ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (hayupo pichani) alipokua akieleza wajibu wa sekta ya fedha nchini katika kuwezesha viwanda vidogo vidogo, wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu akisisitiza kuhusu sekta ya fedha kuwa na mikakakati yenye tija katika kukuza uchumi wa viwanda wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga, akielezea kuwapo kwa changamoto ya kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma za bima za kilimo na   gharama kubwa za huduma za fedha wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Kaimu Kamishna wa Sera za Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Michael Nyagoga akielezea dhana ya Mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango  kuwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za kifedha za Sekta ya Viwanda nchini.
 Wakuu wa taasisi za fedha wakiwa katika majadiliano na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma kuhusu mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa viwanda nchini. 
 Wakuu wa taasisi za fedha wakiwa katika  picha ya pamoja na meza kuu wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma ulioangazia mchango wa sekta ya fedha katika ukuaji wa viwanda nchini.
Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango waliohusika katika uandaaji wa mkutano wa wadau wa sekta ya Fedha na Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizaya ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad