HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 7 May 2018

MJANE KARIAKOO AMUOMBA RAIS MAGUFULI AMSAIDIE KUPATA NYUMBA YAKE


*Adai nguvu ya fedha imesababisha adhulumiwe, sheria kupindishwa

Na Ripota Wetu,Globu ya jamii
MKAZI wa Kariakoo jijini Dar es Salaam Rafika Hawa Sadick ambaye ni Mjane amemuomba Rais John Magufuli kumsaidia ili apate haki baada ya kudai kuna kundi la watu wamepora nyumba Plot 3 block 19 nyumba namba 41 iliyopo Mtaa wa Uhuru na Kongo jijini.

Amesema nguvu ya fedha inayotumiwa na watu ambao wamempora nyumba yake imesababisha hata sheria za nchi zisiheshimiwe na hata baadhi ya maofisa wa Wizara ya Ardhi nao wanashiriki kumkandamiza.

Hivyo amesema imani yake imebaki kwa Rais Magufuli ambaye amekuwa akisaidia wananchi wanyonge kwa kuhakikisha haki inatendeka.
Akizungumza leo kuhusu nyumba hiyo Mama Rafika amesema huu ni mwaka wa 26 amekuwa akipigania haki yake bila mafanikio lakini kupitia Rais Magufuli anaamini haki itapatikana kwani Serikali yake iko makini na haitaki dhuluma

"Walionipora nyumba yangu ni watu wenye fedha, hivyo wanatumia nguvu hiyo ya kifedha kufanya wanachotoka. Haki inapindishwa na hakuna anayejali.

"Nina kila kitu kuhusu nyumba yangu na hata kesi nilishinda lakini bado walipora wanaimiliki kwa nguvu na wanasema sina cha kufanya hata nikienda wapi,"amesema.

Amefafanua nyumba hiyo awali kabla ya kuinunua mwaka 1989 alikuwa mpangaji ndipo mwenye nyumba hiyo kwa wakati huo Amina Amri Husein na Abass Amri Hussein wakatangaza kuiuza kwake.

Amefafanua baada ya kununua alifuata sheria zote za umiliki kwa kupewa hati na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na vibali vya ujenzi.Pamoja na kuimiliki kihalali bado wenye fedha wamempora nyumba yake.

"Nina imani na Rais wangu Magufuli kwani tangu ameingia madarakani nimekuwa nikimfuatilia namna ambavyo anawasaidia waliokata tamaa.Hivyo nami naomba anisaidie nipate haki yangu.Naamini sauti hii ninayoipaza leo hii itafika kwa Rais na haki yangu itapatikana.

"Chonde chonde Rais wangu sikia kilio changu, nisaidie kuipata nyumba yangu ambayo imeporwa irudi kwenye mikono yangu.Kutokana na kuporwa kwa nyumba yangu mwaka 1994 nilipeleka barua Ikulu kutaka kujua nyumba ni yangu au laa kwa kupeleka ushahidi wote.

"Ikulu wakanijibu kwa barua(hii hapa, akaionesha).Ukiisoma utabaini Ikulu wamethibitisha nyumba ni mali yangu lakini cha kushangaza aliyenipora kwa kutumia fedha zake nyumba bado haiko mikononi mwangu,"amesema.

Amesisitiza kuwa "inaumiza hata pale Ikulu inapotoa haki wengine wanaendelea kuipindisha.Ila naamini Ikulu ya Rais Maguguli haiwezi kunyamazia jambo kama hili na ndio maana naomba Rais anisaidie,"amesema.
Amefafanua nchi hii ilikuwa imefika pabaya mno lakini anamshukuru Mungu kwa kumleta  Rais Magufuli kwani ni mtenda haki.
 Mjane Rafika Hawa Sadick akionesha barua ya Ikulu ya mwaka 1994 kwa waandishi wa habari inayothibitisha nyumba namba 41 iliyopo mtaa wa Uhuru na Kongo kuwa ni mali yake halali lakini wenye fedha wameidhulumu, hivyo anamuomba Rais Dk John Magufuli amsaidie apate haki yake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad