HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 13 May 2018

KUWAIT NA TAASISI YA WAMA ZATIA SAINI MKATABA WA KUWASAIDIA WALEMAVU

Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Jasem Al-Najem na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, Jumamosi Mei 12 2018, walitiliana saini mkataba wa ushirikiano kwa ajili ya kuwasaidia walemavu na albino nchini. 

Kwa mujibu wa mkataba huo uliosainiwa katika makao makuu ya Taasisi ya WAMA, Kawe jijini Dar es Salam, Ubalozi wa Kuwait utaipatia Taasisi hiyo dola elfu 50 sawa na takriban shilingi milioni 112  kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa vya walemavu ambavyo vitasambazwa katika vituo husika kama vile Shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko na kituo Maalum cha Usonji (Autism) kilichopo Sinza.
Baada ya zoezi la kutia saini, Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete ameushukuru Ubalozi wa Kuwait kwa msaada huo huku akiahidi kuufikisha kwa walengwa, Mama Salma amefafanua kuwa Taasisi yake inajishughulisha zaidi katika mambo matatu makuu ambayo ni Elimu kwa kuwapa kipaombele watoto mayatima na wanaotoka katika mazingira magumu, afya na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Kwa upande wake Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Al-Najem amesema kuwa Ubalozi umeamua kutia saini mkataba huo ikiwa ni kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli wakati wa uzinduzi rasmi wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete JKMF wiki chache zilizipota uliofanyika Ikulu ambapo Rais Magufuli alitoa wito wa kuzisadida Taasisi zinazoshirikiana na Serikali katika kuwaletea watanzania maendeleo.

Al-Najem amefafanua kuwa Ubalozi utaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania na asasi zisizokuwa za kiserikali ili kuwasaidia walemavu huku akisema kuwa siku ya Jumanne ijayo Ubalozi utakabidhi vifaa vya kisasa katika chumba cha upasuaji cha watoto wenye vichwa vikubwa katika Taasisi ya Mifupa MOI Muhimbili ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamo wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Hafla ya Utiaji saini ilishuhudiwa na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya WAMA ambao Bi. Zakia Meghji, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar pamoja na Daud Nasib.
Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al-Najem na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakisaini mkataba wa ushirikiano katika program ya kuwasaidia walemavu na albino wenye thamani ya dola za Marekani elfu 50 (sawa na shilingi milioni 112) ambazo zitatumika kununulia vifaa kwa ajili ya vituo mbali mbali chini ya Taasisi hiyo.
Balozi wa Kuwait nchini, Jasem Al-Najem akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete (katikati) pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo, Zakia Meghji, baada ya kusaini mkataba wa makubalio.
Picha ya pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad