HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 20 April 2018

WIZARA YAHAMSHA ARI YA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Wizara ya Afya, Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imedhamiria kuendelea na kampeni ya kuamsha ari ya Wananchi kushiriki katika Miradi ya Maendeleo na katika kipindi cha Julai 2017 hadi Machi 2018, Wizara imefanya uhamasishaji katika Mikoa 11 ya Iringa, Dodoma, Mwanza, Pwani, Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Kagera na Shinyanga.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2017/2018 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Bungeni Mjini Dodoma.

Waziri Ummy ameeleza kuwa uhamasishaji huu umewezesha ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya Mondo, Wilaya ya Misungwi (Mwanza); ujenzi wa bwawa la maji Maghangu Mpwapwa (Dodoma); ujenzi wa Zahanati Ufyambe (Iringa); ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Uvinza (Kigoma); ujenzi wa shule ya sekondari na kituo cha afya – Mpanda (Katavi); ujenzi wa kituo cha afya –  Sumbawanga (Rukwa); ujenzi wa kituo cha afya – Mbozi (Songwe); ujenzi wa shule ya sekondari – Manispaa ya Mbeya (Mbeya).

Pia amesema kuwa Kampeni hii ya Kuamsha Ari ya Wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo imesaidia  kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa Makazi ya wazee (Kagera); kuzindua Kituo cha Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) cha wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto Wilaya ya Kahama (Shinyanga) na ujenzi wa madarasa mawili katika Kijiji cha Chambasi, Kisarawe (Pwani).

Aidha Mhe. Ummy Mwalimu ameongeza kuwa Wizara imeendelea kushirikiana na Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika kutekelza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa Huduma kwa jamii na kwa kipindi cha kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Machi, 2018, jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali192 yalisajiliwa.

Mhe.Ummy Mwalimu alisema pia imeongeza Ustawi wa watoto wazee na jamii nchini kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22). Katika mwaka 2017/18, Kazi zilizofanyika chini ya mpango huu ni kutoa elimu kuhusu athari za mila na desturi zenye madhara kwa jamii ikiwemo ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kwa makundi mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wao baadhi ya wabunge waliochangia Hotuba wameipongeza Wizara kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma kwa wananchi.

Naye Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Mandeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba ameiomba Wizara kuajiri Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini ili kuondokana na upungufu uliopo kwani Maafisa hawa ni watu muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Zanzibar Mhe. Najma Giga amesema kuwa Wizara inatakiwa kukaa na wadau ili kupata namna bora ya kutokomeza tatizo la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwani limekuwa ni tatizo linalosumbua katika sehemu nyingi hapa nchini.

“Naomba suala hili la Ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto tuondokane nalo maana tatizo hilo linalowakumba na kuwasababishia ukatili mkubwa watoto na wanawake wenzetu” alisisitiza Mhe. Najma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiwasilisha Utekelezaji wa Bajeti ya kwa Mwakawa fedha  2017/2018 na makadirio ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa fedha 2018/2019 Bungeni Mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad