HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 29 April 2018

WAZIRI WA NISHATI DKT KALEMANI AZINDUA KIWANDA CHA KUTENGENEZA MITA ZA LUKU JIJINI DAR.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani sambamba na wabia wa kampuni ya Baobao Energy System akikata utepe kuashiria kufunguliwa rasmi kwa kiwanda hicho.

Na Leandra Gabriel,  ya jamii
KATIKA kuelekea uchumi wa kati wa viwanda kampuni ya Baobao Energy Systems Tanzania (BEST) imefungua kiwanda cha kutengeneza mita za umeme za luku na hii ni kwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda na kufikia uchumi wa kati kufikia 2025.

Akizungumza katika uzinduzi huo mgeni rasmi ambaye pia Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameeleza kufurahishwa  na kufarijika kwa kupata mwaliko wa kuzindua kiwanda hicho kwani mita za luku zinategemewa na wadau wengi nchini na amewapongeza na kuwataka TANESCO kujipanga katika kukabiliana changamoto za kukidhi mahitaji ya kutoa huduma za umeme kwa wananchi.

Aidha Dkt Kalemani ameeleza kuwa Julai mosi mwaka huu hakuna mita za luku zitakazoagizwa kutoka nje na hii ni baada ya kufanya tathimini kwa miezi mitatu na kujiridhisha na uzalishwaji wa mita hizo hapa nchini na kuanzia Mei mwaka huu mita za luku zitanunuliwa kutoka Baobab.

Pia Dkt Kalemani amewataka wamiliki wa kiwanda hiki kuzingatia uharaka wa utengenezaji, wingi wa mita hizo, ubora na upatikanaji wake kirahisi, Na ameeleza umuhimu wa mita hizi ikiwa pamoja na matengenezo pindi zinapoharibika, gharama nafuu na uharaka tofauti na zile zinazoagizwa nje na amewataka TANESCO kuunganisha umeme kwa siku zisizozidi 7.

Mwakilishi wa Wizara ya viwanda, biashara na uwekezaji Aristides Mbwasi amewapongeza wamiliki na kiwanda hicho na kuahidi ushirikiano pale watakapohitaji kwani kwa sasa taifa lipo katika malengo ya kuijenga Tanzania mpya kama Serikali ya awamu ya tano ilivyoazimia.

Naye Meneja mkuu wa kampuni ya Baobab Energy Systems Tanzania, Mhandisi Hashim Ibrahim amemshukuru waziri wa nishati kwa kuja kufungua kiwanda hicho na kueleza kuwa kampuni hiyo ni ya ubia baina ya kampuni ya Comfix Engineering Ltd ya Tanzania inayomiliki hisa kwa asilimia 51 na hii ni kwa kutoa mchango wa fedha, majengo, rasilimali watu na fedha na kampuni ya EDMI ya nchini Singapore inayomiliki hisa kwa asilimia 49 
na kuchangia mtaji kupitia mitambo na teknolojia kwa ujumla.

Hashim ameeleza kuwa hawaogopi ushindani na kampuni za nje ila tatizo lao ni pale kampuni hizo zinapopewa unafuu wa gharama na uzalishaji na ameiomba serikali kutoa ushirikiano ili kuweza kujenga Tanzania ya viwanda na ameeleza kuwa wana mpango wa kutengeneza mita za gesi na maji hapo baadaye.

Kuhusu uzalishaji wa mita katika kiwanda hicho Hashim ameeleza kuwa mita zitakazotengenezwa na kuuzwa nje na ndani ya nchi zitaliongezea taifa mapato yanayotarajiwa kufikia shilingi Bilioni 97 kwa mwaka.

Pia Mkurugenzi mkuu mauzo wa Kampuni ya EDMI ya nchini Singapore Lam Wee Chee ameeleza kuwa kwa miaka 10 kampuni ya EDMI imefanya kazi na Shirika la Umeme (TANESCO) hasa kwa kusambaza mita hizo na zaidi ya mita 100000 zimenunuliwa na TANESCO kutoka EDMI na kwa sasa watawapa mfumo utakaowasaidia kusoma taarifa zote na kudhibiti wizi wa umeme.

Aidha ameeleza juhudi zao katika kuunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano na kuahidi kutoa huduma bora kwa wateja wao kupitia TANESCO ambao ndio wasambazaji wa mita hizo.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na baadhi wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali za kiserikali na wafanyakazi wa kiwanda cha Baobao Energy System Tanzania wakati wa kuzindua kiwanda hicho kinachojihusisha na utengenezaji wa mita la LUKU, tukio lililofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
 Meneja Mkuu wa  kampuni ya Baobao Energy System Mhandisi Hashim Ibrahim akizungumzia kiwanda hicho kitakachokuwa kinatengeneza mita za LUKU hapahapa nchini wakati wa uzinduzi kilichozindukiwa na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani.
 Mkurugenzi wa Mkuu wa Mauzo wa EDMI Lam Wee Chee akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Baobao Energy System jana Jijini Dar es Salaam.

 Waziri wa Nishati akizindua kiwanda cha Baobao Energy System jana Jijini Dar es Salaam.
 Meneja Mkuu wa Baobao Energy System Hashim Ibrahim akimuelezea jambo Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alipokua akikagua chumba kinachotumika kutengeneza mita za LUKU wakati wa uzinduzi wa Kiwanda hicho.
 Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akikagua mitambo inayotumika kwa ajili ya utengenezeaji wa mita za LUKU wakati wa uzinduzi wa Kiwanda hicho jana Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akipata maelezo mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho namna wanavyoweza kutengeneza mita za LUKU zenye ubora.Picha zote na Zainab Nyamka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad