HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 8 April 2018

MWENYEKITI JUMUIYA YA WAZAZI CCM TAIFA AHIMIZA VIJANA KUWA NA NIDHAMU

Na Elissa Shunda
WAZAZI nchini wameombwa kudumisha nidhamu katika maisha wanayoishi ili vijana wao pia ambao ndiyo viongozi wajao katika ngazi mbalimbali waige mifano mizuri ya kitabia na kiuongozi kutoka kwao ili waje kuwa viongozi bora na si bora kiongozi.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa,Dk.Edmund Mndolwa wakati akizungumza na wanachama wa Jumuiya hiyo na wananchi waliohudhuria  Maadhimisho ya wiki ya wazazi.

Ambayo kitaifa yalifanyika katika ofisi kuu ya wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyopo wilayani Nzega mkoani Tabora na kuhudhuriwa na viongozi wengine wakuu wa jumuiya hiyo na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Serikali.

Katika maadhimisho hayo Dk.Edmund Mndolwa amewaambia wazazi,viongozi,wanachama na wanajumuiya hiyo kuwa ili kijana awe na tabia nzuri katika ukuaji wake na katika utawala wake akichaguliwa kuwa kiongozi mzazi ni mtu wa kwanza katika kumlea mtoto huyo akue katika maadili mazuri.

"Mzazi au mlezi hakikisha katika ukuaji wa kijana wako unamsimamia bega kwa bega kuhakikisha anazingatia maadili na haigi mambo ambayo hayana tija.

“Ndugu zangu wazazi wenzangu katika ukuaji wa mtoto mzazi awe baba na mama ndiyo watu wa kwanza katika kuhakikisha watoto wake wanakua katika maadili mazuri kwa kuwafundisha kila lililo jema na kuwaonyesha lililo baya kuanza tabia na mavazi ambayo kijana aliye mtiifu anapaswa kuyavaa.

"Haiwezekani mzazi anamuona mwanae anatoka usiku anaenda kucheza disko hamkanyi au mzazi unamuona mtoto anatembea na makundi ya vijana wenzake ambao hawana tabia nzuri wewe humkanyi unamnyamazia kwa kuogopa kumkera hapo kaa ukijua mwanao anaharibikiwa utakapotaka kumrekebisha utakuwa umechelewa," anasema.

Dk.Mndolwa amesema mzazi anapaswa kuwa na nidhamu kwa mzunguko wake wote wa maisha anayoishi kuanzia mtaani na nyumbani kwake ili vijana waige mfano wako.

"Lakini kwa jinsi utakavyojiweka ndivyo utakavyojipandisha heshima au kujishusha hadhi katika mtaa wako unaoishi na nyumbani kwako kwa ujumla.Ni jukumu letu sasa kujitathimini mienendo yetu kama kuna mapungufu tujirekebishe ili tutengeneze kizazi na viongozi bora wajao," amesema Dk.Mndolwa.

Aidha Mwenyekiti Dk.Mndolwa amewaonya wazazi ambao wana fedha nyingi za kutosha kuacha mara moja tabia ya kuwapatia watoto wao fedha nyingi za matumizi na kuwapeleka katika kumbi za starehe na sehemu za anasa badala yake watumie fedha hizo katika kuwaelimisha watoto wao.

“Wazazi ambao mwenyezi Mungu amewajalia kipato na kuwa na fedha ya kutosha niwaombe msiwapatie watoto wenu fedha nyingi na magari ya kifahari kwa ajili ya wao kwenda kwenye kumbi za starehe na kufanya anasa badala yake wafundisheni watoto mapema kutumia fedha hizo kupeleka misaada sehemu maalumu kama misikitini, makanisani na kusaidia watoto yatima wanaoishi katika vituo vya kulelewa.

"Wakati wa malezi ya watoto wangu nakumbuka mimi nikishirikiana na mke wangu tulikuwa tunawasimamia vizuri sana watoto wetu katika kuhakikisha wanakuwa na tabia njema na kuvaa nguo zenye heshima. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sasa wamekuwa kila mtu ana familia yake," amesema Dk.Mndolwa

Aidha Dk.Mndolwa ametoa agizo kwa viongozi na wanajumuiya wote ya wazazi kuhakikisha wanasimamia vya kutosha katika kuenzi dhumuni la kuwepo kwa jumuiya hiyo ambavyo ni malezi kwa vijana wao,utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kadri wawezavyo na kulinda uharibifu wa mazingira.

Pia kushiriki na jamii husika katika kuhakikisha huduma ya afya inaimarika kwa kuwajulia hali wagonjwa katika vituo vya afya,kutoa vifaa kwa ajili ya mahitaji ya vituo hivyo na kushiriki katika utatuzi wa changamoto zinazozunguka katika hospitali walizo karibu nazo.

Pia Mwenyekiti Dk.Mndolwa ameshauri vijana kutokubali kutumiwa kwa faida ya kikundi cha watu wachache wenye kutaka kunufaika peke yao na kuacha kuangalia maslahi mapana ya Tanzania na wananchi wake.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wengine wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora,Gullam Dewji amesema  wamepokea maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi huyo wa jumuiya ya wazazi taifa Dk.Edmund Mndolwa na kuahidi kuyachukua na kuyafanyia kazi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa mkoa huo,Aggrey Mwanri amemhakikishia mwenyekiti huyo wa mkoa kuwa ulinzi umeimarishwa na kuwaambia wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi.

“Katika mkoa huu mimi ni  Mwakilishi wa Rais Dk.John Magufuli,hivyo nitahakikisha  nikishirikiana na vyombo vya dola Tabora yetu ulinzi umeimarishwa.Serikali inawapenda wananchi wake sema ikitokea tofauti kidogo ila amani iwepo eneo husika hakuna budi serikali hiyo kutumia nguvu kidogo ili kuleta amani eneo husika,” amesema Mwanri.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa akizungumza katika maadhimisho ya wiki ya Wazazi Taifa ambayo yalifanyika katika wilayani Nzega Mkoa wa Tabora leo. Picha zote na Elisa Shunda.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa wa Pwani, Jackson kituka, Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo wa Mkoa huo, Gama J.Gama, Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa kutoka Mkoa wa Pwani, Dk.Zainab Gama na Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa Wilaya ya Kibaha Mjini, Edwin Shunda na wajumbe wengine wakimsikilza kwa makini Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Taifa Dk.Edmund Mndolwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza katika maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad