HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 19, 2018

Astashahada, Stashahada Msizipe Kisogo: Waziri Jafo

Na Atley Kuni OR TAMISEMI
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema kuanza kwa kozi za ngazi ya Shahada katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kisiwe kigezo cha kuondosha kozi za Astashahada na Stashahada katika chuo hicho.
Waziri Jafo alikuwa akizundua rasmi Bustani ya  Magufuli katika chuo hicho ambapo Bustani hiyo itatumika kuishi na kuenzi mchango wa kiongozi huyo wa Nchi kwasasa ambao ni uzalendo, kujituma pamoja na uadilifu katika kuwatumikia wananchi.
“Nimesikia maombi yenu yakutaka Kuanzishwa kwa kozi za Ngazi ya Shahada kusudi mtu anapo hitimu masomo yake ya ngazi za awali aweze kuendelea, naomba niwambie, tutajitahidi lifanikiwe, lakini angalizo langu kwenu, tutakapo anzisha Degree isiwe sababu yakusitisha kozi zinazoendelea kwa sasa, ikiwepo Astashahada (Certificate) na Stashahada (Diploma) ya kozi mnazo endelea nazo” amesema Jafo.
Waziri Jafo amesema, vyuo vingi vilipo anzisha ngazi ya Shahada na kusahau wataalam wa kada za kati vilichochea kukosekana kwa wataalam wakutosha katika ngazi ya kati hususan mafundi mchundo ambao walikuwa wakizalishwa katika vyuo hivyo.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewahakikishia Wakurufunzi hao wa chuo cha Hombolo uhakika wa kuajiriwa na Serikali kwa wale watakao fikia vigezo vinavyo hitajika katika nafasi mbali mbali ambazo serikali itatangaza.
“Tumebaini Wataalam wa chuo cha Hombolo  tunaowaajiri katika kada za Maafisa Watendaji wa Vijiji, Kata na hata Tarafa wanauelewa mpana wa Masuala ya jamii za watanzania hususan ni wale waishio vijijini, hivyo basi tunapotangaza ajira kipaumbele tutakitoa kwa  wanafunzi wa chuo hiki” amesema Waziri Jafo.
Mhe. Jafo hakusita kuonesha furaha yake kwa jinsi chuo hicho kilivyo jizatiti katika suala la utunzaji wa mazingira, hatua ambayo ameitaja ni  kumuunga mkono Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye kupitia Wizara ya Mazingira na Muungano amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watanzania wanantunza mazingira.
Mbali ya pongezi hizo Waziri  ametoa maelekezo kwa uongozi wa Manispaa ya Dodoma kuanza kampeni ya upandaji wa miti ya Matunda. “Tunataka Dodoma iwe Fruit City” amenukuliwa Waziri
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi inayomaliza Muda wake Prof. Suleiman Ngware, yeye alisema lengo la kujenga Bustani ya  Magufuli nikuunga mkono juhudi za Mhe. Rais katika kusimamia rasilimali za nchi kwa moyo uzalendo na uadilifu wa dhati.
“Mhe. Waziri Shabaha yakuwa na Bustani ya aina hii yenye Mnara wa Magufuli nikutambua mchango mkubwa na moyo wa kizalendo alionao Rais wetu, sasa tunachotaka nini hapa, kila mtu atakaye uangalia mnara huu aweze kujitathmini mwenyewe bila yakusukumwa na mtu, Je! Mimi kama Mkufunzi ninatimiza wajibu wangu? Mimi kama Mwanafunzi nafanya matendo sawa na Rais wangu? Mimi kama Mwenyekiti wa Bodi au Mkuu wa Shule sifanyi manyanyaso kwa watu sibagui watu nk, nk". Amesema Mwenyekiti huyo.
Kila Mwaka ifikapo Aprili 18, Bodi, Uongozi, Wanafunzi na Wananchi wanaozunguka eneo la chuo watakuwa wakikutana kwa pamoja na kujitathmini kwa mienendo na matendo yao ya utendaji wa mwaka mzima, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo kwa sasa kinawanafunzi zaidi ya 3000.
 Waziri wa Nchi OR TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo (Mb), akizungumza  wakati wa uzunduzi wa mnara wa kuenzi uzalendo wa Mhe. Rais wa awamu ya tano wa Tanzania katika chuo cha Hombolo.




Baadhi ya watendaji wa Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo wakati wa zoezi la uzinduzi wa mnara wa fikra za kizalendo za Mhe. Rais Magufu
 Kikundi cha Ngoma za asili cha Swala kitoa borudani wakati wa  wa uzunduzi wa mnara wa kuenzi uzalendo wa Mhe. Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, kikundi hicho kinachopatikana katika Kijiji cha Nkoyo, Hombolo ambacho ni maarufu katika mkoa wa Dodoma hususani kudumisha utamaduni wa mtanzania.
Mwonekano wa Mnara wa Magufuli Square, Sehemu iliyojengwa mahususi kwa ajili ya kuenzi uzalendo wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa vitendo
 Bodi ya Chuo cha Hombolo iliyo maliza muda wake wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa mnara wa fikra za kizalendo za Mhe. Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad