HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 21, 2018

WIZARA YA AFYA YATHIBITISHA UWEPO WA HOMA YA DANGUE, YAWATOA HOFU WANANCHI

Na Said Mwishehe,Globu  ya jamii

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa kumebainika uwepo wa virusi vya homa ya Dangue nchini huku ikiwata hofu wananchi na tayari imeanza kuchukua hutua mbalimbali kukabiliana nao.

Akitoa tamko la Serikali kuhusu uwepo wa ugonjwa hu, Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kutokana na vipimo vilivyofanya katika maabara ya Taifa International kupelekewa sampuli za wagonjwa kutoka katika Hospitali ya Intarnetional School of Tanganyika (IST)ya Dar es Salaam, waliohisiwa kuwa na ugonjwa wa malaria lakini vipimo vyao havikubaini uwepo wa ugonjwa huo.

Amefafanua kipindi cha kati ya Januari 2018 hadi sasa kati ya sampuli 13 zilizopokelewa kutoka IST 11 zilionesha uwepo wa virusi vya dangue na kuongeza ikumbukwe hiyo si mara ya kwanza kwa ugonjwa huo kuripotiwa hapa nchini kwani ulishawahi kuripotiwa miaka ya 2010,2013 na mwaka 2014.

"Taarifa ya uwepo wa homa hiyo ya Dangue si ya kushangaza kwani mbu anayeeneza virusi vya ugonjwa huu bado yupo katika mazingira yetu.Homa ya Dangue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa aina ya Aedes ambao ni weusi na wenye madoa meupe yenye kung'aa,"amesema Waziri Mwalimu.

Kuhusu dalili za ugonjwa huo, amesema ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa hasa sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchuvu.Dalili hizo huanza kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa ya Dangue.

Mwalimu amesema wakati mwingine dalili za ugonjwa huo zinaweza kufanana sana na dalili za Malaria,hivyo basi wananchi wahakikishe wakipata homa wapime ili kugundua kama wana vimelea vya malaria au dangue au sababu nyingine ili hatua stahiki zichukuliwe.

Pia amesema ni mara chache mgonjwa anaweza kutokwa na damu sehemu za fizi mdomoni, puani kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.Mbu wanao eneza homa ya dangue hupendelea kuzaliana kwenye maji yaliyotuama karibu na makazi ya watu, ndani ya nyumba na viluilui vya mbu hao huweza kuishi katika mazingira ya ndani ya nyumba mpaka wakawa mbu kamili na kuanza kusambaza ugonjwa huu kwa binadamu

"Tofauti na mbu wanaoeneza malaria, mbu wanaonezahoma ya dangue huwa na tabia ya kuuma binadamu nyakati za asubuhi na jioni.Tusisitize ugonjwa huu hauenezwi kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine bila ya kuwepo na kuumwa na mbu mwenye vimelea,"amesema.

Akizungumzia matibabu ya Dangue,Waziri Mwalimu amesema hadi sasa hakuna chanjo ya homa ya dangue inayotolewa hapa nchini,
hivyo mgonjwa mwenye homa ya dangue hutibiwa kutokana na dalili zitakazoambatana na ugonjwa huu kama vile homa na kupungukiwa na maji au damu.

Pia mgonjwa mwenye dalili za homa ya dangue anashauriwa kuwahi mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya ili kupata huduma stahiki

Kuhusu jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo, amesema unaweza kujikinga asipate maambukizi ya virusi vya dangue kwa kuchukua hatua mbalimbali na baadhi ya hatua hizo ni kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au kunyunyizia dawa ya kuua viluilui vya mbu kwenye dimbwi hayo

Amesema ni jukumu la mmoja wetu kuhakikisha kuwa mazalio ya mbu yanaangamiza na pia kujizuia na mbu na kwamba hatua ambazo zinachukuliwa na Wizara ni kutoa taarifa ya tahadhari ya uwepo wa ugonjwa kwa waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya chini kupitia ofisi ya Rais-Tamisemi.

Pia kutuma vipeperushi vya ugonjwa huo katika maeneo ya mipakani ili iwapo msafiri anayeondoka au kurudi nchini akiwa na dalili tajwa atoe taarifa kwa watumishi wa afya wa mpakani ili hatua stahiki zichukuliwe

"Tumeimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji taarifa ambao tunaendelea kupata taarifa za kila siku kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu.Wizara inashauri wananchi wasiwe na hofu,"amesema.

Pia amesema wizara inasisitiza hakuna vikwazo vyovyote vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka chini.Aidha wizara itaendelea kushirikiaa na wadau wa sekta mbalimbali katika kufuatila na kudhibiti ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad