HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 23, 2018

WATU WENYE MAHITAJI MAALUM NCHINI WAFANYIWE UTAFITI WA KINA

Wakati umefika wa kufanywa utafiti wa kina kujua mazingira halisi ya Watu wenye mahitaji Maalum Nchini ili kupata mwanga wa uhakika wa kuelewa pamoja na kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu mahitaji wanayopaswa kupatikana kwa kundi hilo katika Jamii.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Omar Seif Abeid alieleza hayo wakati akitoa Taarifa kwenye Kikao cha Majumuisho ya Ziara ya kamati hiyo hapo katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar.

Mh. Omar alisema ushirikishwaji wa Watu wenye Mahitahi maalum yaani Walemavu bado ni mdogo hasa katika maeneo ya Vijiji jambo ambalo husababishwa kukumbwa na changamoto nyingi likiwemo wimbi la udhalilishwaji wa Kijinsia ambalo kwa sasa limeshika kasi na kuendelea kuwaathiri kiakili.

Alisema ipo haja kwa Taasisi za Umma kuendelea kuwatumia Masheha pamoja na Makundi ya Kioraia katika maeneo husika kuliona tatizo hili na kutafuta mbinu ya pamoja na kulitatua.

Mheshimiwa Omar alisema suala hilo ni vyema likaenda sambamba kwa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar inayoratibu Idara inayoyohusika na Watu wenye Ulemavu kukaa pamoja na Wizara ya Elimu kufikiria njia ya kulitononosha Kundi hilo.

Alieleza kwamba Elimu Maalum kwa sasa inahitajika katika kuona Watu wenye Mahitaji Maalum wanazingatiwa ili kuwapa upeo na nguvu za kupambana na vitendi vya Udhalilishaji katika misingi ya kujiamini zaidi.

Wakichangia Taarifa hizo Baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa waliiomba Serikali kusingatia Vituo Maalum vya kupatia huduma za Afya Watu wenye mahitaji maalum ili kuwapunguzia gharama zinazowakabili hasa wale wanaohitajika kusafirishwa nje ya Zanzibar.

Walisema hatua hiyo itasaidia kuipunguzia gharama kubwa Serikali sambamba na kuzingatiwa mazingira rafiki ya Kundi hilo hasa kwenye Majengo ya Serikali wakati wanapokwenda kutaka kupata huduma za msingi.

Wajumbe hao pia walisisitiza suala la kuongezwa kwa Bajeti ya Kundi hilo waweze kujikimu kiutendaji pamoja na harakati zao za kila siku zinazowasaidia kuendesha maisha yao.

Wakichangia wimbi la Dawa za Kulevya Wajumbe hao waliiomba Serikali kufikiria nanma ya kukiongezea Ruzuku Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM} ili kuongeza Doria katika maeneo mengi ya Bandari yasiyo rasmi kwa kuingilia na kutokea.

Walisema hatua hiyo inaweza kuwatia hofu Watu wenye tabia ya kuiongiza Dawa za kulevya Nchini kwa kutumia Bandari bubu ambazo Pemba pekee zinakisiwa kuwa na Bandari zisizo rasmi zipatazo 162.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bibi Abeida Rashid Abdulla aliwaambia Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa kwamba jumla ya Vikundi 14 vya ujasiri Amali vimeshapatiwa Mikopo kwa ajili ya shughuli za ujasiri amali baada ya kupatiwa mafunzo mwaka 2017.

Mkurugenzi Abeida alisema hatua ya awamu ya Pili ya muelekeo wa kuviwezesha Vikundi hivyo vya Mahitaji Maalu imelenga kuvipatia Mikopop Vikundi Sita vya Ujasiri Amali Unguja na Pemba kwa lengo la kuendeleza miradi yao ya Kiuchumi.

Akitoa nasaha zake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimia Mohamed Aboud Mohamed alisema Kundi la Watu wenye Mahitaji Maalum ni eneo kubwa ambalo Serikali Kuu imelipa Kipaumbele na msukumo mkubwa.

Alisema upo Mpango Maalum unaotoa muelekeo wa jinsi gani Taasisi za Umma na hata Binafsi zinajiweka tayari katika kuzingatia mazingira Rafiki ya Kundi hilo hasa katika Miundombinu ya Majengo ya huduma.

Waziri Aboud aliihakikishia Kamati hiyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaangalia utaratibu wa kuweka mfuko wa Afya utakaoweza kuwasaidia Watu wenye Mahitaji Maalum zikiwemo zile Familia Duni kabisa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
23/3/2018.

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar chini ya Mwenyekjiti wake waliokaa kati kati Kulia Mheshimiwa Omar Seif Abeid wakiwa katika Kikao cha majumuisho ya ziara yao ndani ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kilichofanyika Vuga Mjini Zanzibar.
Baadhi ya watendaji Wakuu na Maafisa wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar walioshiriki katika Kikao hicho cha Majumuisho ya Kamati hiyo.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakiwa katika Kikao hicho cha Majumuisho ya ziara yao ndani ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad