HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 23, 2018

PANITA YATOA USHAURI KWA SERIKALI KUHUSU MUHIMU WA LISHE BORA

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
JUKWAA la Lishe Tanzania(Panita) limeishauri Serikali kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kuhusu lishe kwenye jamii ya Watazania ili kuwa na taifa lenye uwezo wa kujituma na kuleta maendeleo.

Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa Program wa Panita, Jane Msagati wakati anazungumza na Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhusu lishe bora.

Amesema kuna kila sababu ya kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele nchini kwa jamii kupata elimu itakayosaidia kutambua umuhimu wa lishe bora katika Taifa.

"Ukosefu wa lishe bora mwilini unasababisha udumavu na utapiamlo na matokeo yake husababisha magonjwa ambayo ni gharama kuyatibu na wakati mwingine husababisha ulemavu wa kudumu.

"Tatizo la lishe chini limesababisha kuongozeka kwa watoto wenye udumavu wa mwili na akili.Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia matibabu, na hiyo ni hasara kubwa,"amesema Msagati.
Akizungumza kuhusu lishe  amesema ni msingi wa maendeleo kwa wote na jamii ihakikishe watoto wote wanapata lishe sahihi hususani siku 1000 za kwanza.

Pia amesema wababa wahusike kwenye malezi ya watoto na jamii ihakikishe kaya zinauhakika wa chakula kwa kuzalisha vyakula vya kutosha na kutotumia vyakula vyote kutengeneza pombe.

Amezungumzia umuhimu wa jamii kutengeneza bustani ndogondogo kuzunguka nyumba, bustani makasha/viroba kwa ajili ya mboga za majani.Pia kufuga wanyama wadogo kama kuku na  sungura.

Amesema ukosefu wa virutubisho mwilini husababisha njaa iliyojificha ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa katika kusababisha magonjwa na vifo hususani kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na akina mama walio katika umri wa kuzaa

Kuhusu mafunzo ya lishe kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, Msagati amesema wanatambua nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha umma.

Msagati amesema wahariri wa vyombo vya habari ndio wenye jukumu la kupitisha habari kwenye vyombo vyao na hivyo kukutana kati ya Panita na wahariri hao kutatoa fursa ya kuelezea umuhimu wa kuzipa kipaumbele habari za lishe bora.

Mhariri wa Gazeti la Mtanzania, Bakari Kimwanga na Mgariri wa Jarida la Afya na Ajira kutoka Gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka wamezungumzia umuhimu wa mafunzo yaliyotolewa na Panita kuhusu lishe bora na kwamba watatumia vyombo vyao kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kuzingatia lishe bora.
Mtaalam wa masuala ya lishe kutoka Jukwaa la Lishe Tanzania(Panita), Deborah Esam akitoa mada kwa wahariri wa vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa jamii.
Meneja wa Program wa Jukwaa la Lishe Tanzania(Panita), Jane Msagati akitoa mada kwenye semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika leo Dar es Saalam leo Semina hiyo ilikuwa inangumzia umuhimu wa lishe bora kwa jamii.
Mwandishi Mwandamizi wa Mlimani TV, Annuary Mkama akitoa somo kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini.
Mhariri wa Jarida la Afya na Ajira kutoka gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka(katikati) akifafanua jambo kwenye semina iliyoandaliwa na Panita kuhusu lishe bora.
Mhariri wa gazeti la Mtanzania, Bakari Kimwanga (katikati) akifafanua jambo kwenye semina ya Lishe bora iliyoandaliwa na Jukwaa la Lishe Tanzania(Panita)leo jijini Dar es Salaam leo.
Mhariri wa Redio Clouds FM Joyce Shebe akizungumza kwenye semina ya lishe bora iliyoandaliwa na Panita leo jijini Dar es Salaam.
Mtangazaji wa TBC(wa kwanza kulia) akifafanua jambo kwenye semina hiyo ya lishe bora leo jijini Dar es Salaam leo.
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza mtoa mada katika semina la lishe bora kutoka kwa Meneja wa Programu wa Panita Jane Msagati(hayupo pichani).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad