HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 23, 2018

TAMISEMI KUBAINI WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM

KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo amefunga Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha wataalam watambuzi hao mjini Morogoro.

Akitoa hotuba yake, mbele ya walimu, maafisa ustawi wa Jamii na baadhi ya madaktari, Mkongo amesema ana imani kubwa na wataalamu hao ambao wamepatiwa mafunzo ya kubaini kwa kutumia vifaa maalum kuwa watafikia malengo ya kazi waliyoelekezwa na Serikali ili kuboresha huduma ya elimu bora kwa watoto wenye mahitaji maalum nchini.

“Ni matumaini yangu baada ya mafunzo haya kuwa kila mmoja wenu atakuwa na ujuzi wa
kutosha kutumia vifaa maalum kuwabaini watoto wenye changamoto za uoni hafifu, ujongeaji wa viungo vya mwili, usikivu, changamoto nyingine ambazo hutegemea hali ya afya na mazingira,”Amesema.

Amesema Watoto hao wanatarajiwa kutoka rika la miaka minne hadi sita na kwamba wataalam hao watatoa ushauri wa kitaalam na kitabibu kwa wazazi na walezi wa watoto hao, na walimu wa watoto watakaobainika hivyo ni vema wakaifanya kazi hiyo kwa umakini na weledi mkubwa ili malengo ya Serikali yatimie.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa Morogoro amesisitiza kuchukuliwa kwa hatua zinazostahili kwa watoto watakao bainika ili wapatiwe huduma kulingana na hali waliyonayo na mahitaji yao halisi.

“Ninasisitiza kuwa watoto watakaobainika kuwa na matatizo yanayohitaji matibabu, wazazi au walezi waelekezwe kuwapeleka katika vituo vya afya kwa matibabu au uchunguzi zaidi, baada ya uchunguzi mzazi au mlezi ashauriwe kumwaandikisha mtoto katika shule jumuishi, kitengo au shule maalum iliyokamilika kulingana na aina ya mahitaji maalum aliyonayo mtoto,”amesema.

Amesema Watoto wote wanahitaji kupatiwa elimu iliyo bora ili kujenga uhusiano unaokubalika katika jamii na kuandaa mazingira yanayotawala maisha yao ya kila siku ili kuirahisishia Serikali kuandaa, kupanga na kutekeleza mipango sahihi kulingana na aina ya mahitaji yao na kupata elimu iliyo bora.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu (Elimu ya Watu Wazima), Ofisi ya Rais TAMISEMI Kassim Kaoneka, akitoa maelezo ya awali kumkaribisha mgeni rasmi, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ya siku sita ni pamoja na kupata uelewa wa pamoja ili kupata vigezo vya kuwatambua watoto wenye uhitaji maalum katika kada mbalimbali kama watoto wasioona, wasio sikia, watoto wenye ulemavu wa viungo, watoto wenye changamoto za ufahamu, pamoja na ulemavu wa akili.

Zoezi la kuwabaini wototo wenye mahitaji maalum linakusudiwa kuanza nchini kote kwani vifaa vyote kwa ajili ya utambuzi tayari vimekwisha gawiwa katika ofisi za Mikoa yote ya Tanzania Bara.

Aidha, Kaoneka amesema Mpango wa kuwabaini wototo hao unaenda sambamba na Mpango wa kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ambao upo chini ya Programu ya LANES inayoratibiwa na kutekelezwa kwa pamoja kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wataalam hao, Salvatory Kitogwe amesema jumla ya washiriki wote ni 314 ambao wanatoka katika mikoa mbali mbali na wao kama wataalam
wanasisitiza kufika kwa taarifa mapema mikoani na wilayani ili kufanya zoezi la kuwabaini watoto wenye mahitaji maalum kuwa rahis na kulifanya kwa ufanisi.

Mapema kabla ya Mafunzo hayo Mhe.Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mpango huo sambamba na ugawaji wa vifaa maalum vitakavyotumika na pia aliagiza utekelezaji wake ufanyike mapema iwezekanavyo ili Serikali ipange mipango yake na kuitekeleza kwa wakati.
 Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo akifunga Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha wataalam watambuzi hao mjini Morogoro.
 Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu (Elimu ya Watu Wazima), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kassim Kaoneka akitoa neno la awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi. 
 Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Ernest Mkongo (kushoto) akiteta jambo na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimu (Elimu ya Watu Wazima), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kassim Kaoneka.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi ya kubaini watoto wenye mahitaji maalum yaliyowahusisha wataalam watambuzi hao mjini Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad