HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 14 March 2018

RC MWANRI: KUANZIA SASA KILA ZAO NI LAZIMA LILIME KITAAALAMU

SERIKALI  ya Mkoani Tabora imesema kuanzia msimu ujao mazao yote ni lazima yalimwe kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora kinachosisitiza matumizi ya mbolea na ujazaji wa mazao kitaaalamu ili kuhakikisha kunakuwa na mavuno mengi ambayo yatawawezesha wakulima kuzalisha ziada ambayo itawasaidia kuwaletea maendeleo yao binafsi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Wilayani Kaliua na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akiendelea na  kampeni zake za kuelimisha wakulima wa pamba juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu waharibifu katika pamba.

Alisema ulimaji wa hivi sasa kwa  wakulima walio wengi hauzingatii ujazaji wa miche(plant population) kitaalamu katika mashamba yao na matumizi ya mbolea jambo linalopelekea kuwepo na mavuno machache katika eneo kubwa shamba hatua ambayo inamfanya mkulima kuwa na mavuno machache.

Kufuatia hatua hiyo Mkuu huyo wa Mkoa alisema kilimo kijacho ni lazima wakulima wote waliopo  Mkoani Tabora walime kilimo kinachowasaidia kuzalisha ziada na kupata fedha kwa ajili ya kupanua kilimo chake na kuboresha maisha yao.

"Kuanzia sasa ni marufuku kwa wakulima kwa Mkoa huu kulima zao lolote iwe mchicha, viazi , mahindi na mazao ya biashara bila kufuata mistari na kujaza mazao katika shamba...siwezi kuendelea kuvumilia wakulima wanaendelea kulima kilimo ambacho hakiwasaidia kupiga hatua na kuondokana na umaskini kwa kuzalisha mazao mengi katika eneo dogo" alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema ili kufanikisha zoezi hilo Maafisa Ugani wote  wanatakiwa kuanza sasa  kwenda kwa wakulima wote ili kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao mbalimbali kinachozingatia kanuni bora na ujazaji wa miche kitaalamu katika shamba ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika ulimaji wao ambao ndio utakaowasaidia kuboresha maisha yao.

Mwanri alisema ni lazima wakulima waelimishwe kuwa kilimo bora na kinachozingatia kuzingatia kanuni bora sio tu kwa mazao ya tumbaku na pamba mkoani humo bali na kwa mazao yote yanayolimwa katika maeneo yao kama wanataka kuendelea.

Alisema kitendo cha kuwaacha wakulima kuendelea kulima kwa mazoea hakuwezi kuwasaidia kupiga hatua na kuondokana na umaskini.
 Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua Michael Nyahinga( wa pili kutoka kushoto) akitoa maelezo jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( wa pili kulia) wakati alipotembelea shamba la pamba la Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama ikiwa ni sehemu ya kuwaelimisha wakulima wa zao juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu. Wengine ni Mratibu wa Pamba wa Wilaya ya Kaliua Samwel Mushi(kushoto) na Mshauri wa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Modest Kaijage(kulia).
 Mshauri wa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Modest Kaijage(kulia)  akitoa maelezo jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( wa pili kulia) wakati alipotembelea shamba la pamba la Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama ikiwa ni sehemu ya kuwaelimisha wakulima wa zao juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu. Wengine ni Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua Michael Nyahinga(kushoto) na Afisa Tarafa ya Kaliua Bethod Mahenge (wa pili kulia)
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(wa pili kushoto) akizungumza jambo jana kwa Katibu Tawala Wilaya ya Kaliua Michael Nyahinga( kushoto) wakati alipotembelea shamba la pamba la Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama ikiwa ni sehemu ya kuwaelimisha wakulima wa zao juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu. Wengine ni Afisa Tarafa ya Kaliua Bethod Mahenge(wa pili kulia) na Mshauri wa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Modest Kaijage(kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( kushoto) akizungumza jambo jana kwa kwa viongozi mbalimbali kutoka Ofisi yake na Ofisi ya Wilaya na Halmashauri ya Kaliua wakati alipotembelea shamba la pamba la Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama ikiwa ni sehemu ya kuwaelimisha wakulima wa zao juu ya matumizi sahihi ya dawa za kuua wadudu. Picha na Tiganya Vincent

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad