HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 9 March 2018

DC MSHAMA AWAASA WANAWAKE KUACHA KURUDISHANA NYUMA KIMAENDELEO NA FITNA

Mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama.

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha.
MKUU wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama ,amewaasa wanawake kuacha tabia ya kurudishana nyuma kwenye maendeleo,fitna na kuwabeza wengine ambao wanakuwa na uwezo kiuchumi na uongozi .

Aidha amewataka wale wenye uwezo wa raslimali fedha kuthubutu kuanzisha viwanda vya kati na vikubwa ili kuikomboa jamii katika eneo la ajira.

Mshama amewasihi pia wanawake kuiunga mkono serikali ikiwa ni pamoja na kuisemea mazuri inayoyafanya ikiwemo kusimamia mafungu ya kuwezeshwa wanawake kupitia halmashauri nchini.

Mshama aliyasema hayo,Mwendapole katika maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyoadhimishwa na halmashauri ya Mji wa Kibaha.

Aliwaomba akinamama hao waungane mkono kwenye kila jambo ili kujiinua kimaisha.

"Unakuta tunabezana wenyewe ,mtu anauwezo mkubwa wa kufanya biashara ,anaongoza nyadhifa fulani lakini tunafanyiana fitna ,majungu na kukatishana tamaa" alisema Mshama.

Hata hivyo ,alielezea serikali ya awamu ya tano inaendelea kusimamia fedha zinazopaswa kuwezeshwa wanawake kwa asilimia nne ,vijana nne na wazee na walemavu asilimia mbili .

"Mjaribu kuwaelimisha wachache wasiotambua kazi kubwa inayofanywa na viongozi wetu waliopo madarakani " alisema Mshama.

Kuhusiana na changamoto wanayokabiliana nayo kundi hilo ikiwemo kukosa maeneo ya kuweka bidhaa na uhakika wa masoko,Mshama alisema atawasiliana na uongozi wa halmashauri ili iweze kutenga siku ya kuonyesha maonyesho ya bidhaa zao .

"Mfano kila mwisho wa mwezi tunapanga tupange biashara zetu pale Mailmoja ,lazima wateja watakuja kutoka ndani ya wilaya ,mkoa na nje ya Mkoa ,hii itaongeza tija kubwa kwenu"

"Sasa mnatakiwa mboreshe bidhaa zenu kwani kwenye ushindani wa soko ,kizuri chajiuza kibaya chajitembeza ," alibainisha Mshama.

Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Leah Lwanji alisema idara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wameweza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wajasiriamali 751 ambapo kati yao Wanawake ni 480 .#

"Huduma ya usajili wa biashara ilitolewa na Brela kwa washiriki 24,"; Pia kongano za biashara zimeundwa kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali kufanya kazi zinazofanana na kupata fursa ya kueleza changamoto zao kama kongano" alisema Leah.

Leah alieleza mwaka 2016-2017 halmashauri ilitoa fedha kiasi cha sh.mil .173 kwa ajili ya mikopo kwa Wanawake na vijana  ,2017-2018 ilitoa mil.368 na July -Sept 2017 walitoa mil.100 kwa vikundi 50 vyenye wanachama 320.

Kwa upande wake ,diwani wa viti maalum Mji wa Kibaha ambae pia ni katibu wa jukwaa la uwezeshaji mkoani Pwani,Elina Mgonja alisisitiza umoja kwa akinamama utakaowezesha kuwa na sauti moja kupigania fursa za ujasiriamali .

Elina alieleza ,wamejipanga kuthubutu kuanzisha miradi mikubwa na kuboresha bidhaaa kwa kushikana mikono ili kujikwamua kiuchumi .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad