HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 14, 2018

AJALI ZAPUNGUA PWANI KWA ASILIMIA 57.9-RPC SHANNA

KAMANDA wa Polisi Mkoani Pwani (ACP)Jonathan Shanna ,akielezea hali ya usalama barabarani tangu mwaka huu uanze kwa waandishi wa habari Mkoani hapo,kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisini kwake .(picha na Mwamvua Mwinyi )

Na Mwamvua Mwinyi Kibaha
MKOA wa Pwani umeanza vizuri mwaka 2018, kwa kupunguza ajali kutoka ajali 19 kwa mwaka 2017 hadi ajali nane kwa mwaka huu sawa na asilimia 57.9.

Kadhalika ajali za vifo zimepungua kutoka ajali 16 mwaka 2017 hadi kufikia ajali sita mwaka huu ikiwa ni asilimia 62.5 ambapo watu waliokufa katika kipindi kama hiki walikuwa 18 na mwaka huu imepungua hadi kufikia watu nane sawa na asilimia 55.55.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, (ACP) Jonathan Shanna aliyasema hayo wakati akielezea hali ya usalama barabarani tangu mwaka huu uanze.

Aidha alisema pia ,idadi ya watu waliojeruhiwa kwa kipindi kama hicho ilikuwa 27 kwa mwaka 2017 na mwaka huu imepungua hadi kufikia 10 sawa na asilimia 62.96.;"

Pamoja na hayo ,Shanna alielezea kwa mwaka mzima wa 2017 Mkoa huo ulipunguza ajali kutoka ajali 396 zilizotokea 2016 hadi kufikia ajali 103 sawa na asilimia 73.98 .;"

"Ajali vifo kwa mwaka 2017 tulifanikiwa kupunguza ajali za vifo kutoka ajali 164 za mwaka 2016 hadi kufikia 82 mwaka uliopita sawa na asilimia 50.;"

"Idadi ya vifo kwa mwaka 2017 tumeweza kupunguza vifo kutoka 187 kwa mwaka 2016 hadi vifo 107 kwa mwaka 2017 sawa na asilimia 52.78":; alifafanua Shanna.

Hata hivyo Shanna alisema kuwa ,mwaka uliopita walifanikiwa kupunguza majeruhi wa ajali za barabarani kutoka majeruhi 391 kwa mwaka 2016 hadi kufikia majeruhi 154 kwa mwaka 2017 sawa na asilimia 60.61.

Kamanda huyo ,aliweka bayana kwamba kutokana na ukamataji wa makosa ya usalama barabarani mwaka 2017 yalikamatwa makosa 129,639 na kukusanya kiasi cha sh.bilioni 3.889.170/.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2016 yalikamatwa makosa 111,257 na kukusanya sh.bilioni 3.337.700 ikiwa ni ongezeko la sh.551.470.000./

Nae kamanda wa usalama barabarani Mkoani hapo ,Abdi Issango alieleza ,ipo mikakati waliyojiwekea kukabiliana na ajali za barabarani kwa mwaka 2018/2019.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha matumizi ya vipima ulevi kwa kuwapima madereva katika vituo vyote vya mabasi wakiwa safarini ili kuwabaini madereva wanaotumia kilevi na madawa ya kulevya .

Issango alitaja mkakati mingine kuwa ni kuimarisha matumizi ya speed radar kwa kufanya doria barabarani usiku na mchana ili kubaini wanaoendesha kwa mwendo kasi .

Mkakati mwingine ni kutoa mafunzo ya sheria za usalama barabarani kwa waendesha pikipiki.

Issango alibainisha wanaendelea kufanya oparesheni kwa magari aina ya Noah yanayobeba abiria kupita kiasi pamoja na magari yanayobeba wanafunzi ambayo hayana ubora .

Jeshi la Polisi Mkoani humo kupitia kitengo cha usalama barabarani limesema halitakuwa na mchezo kwa dereva atakaekiuka sheria zilizopo na wataendelea na misako ya kukagua magari mbalimbali ,na ni msako endelevu .

Kwa upande wake dereva wa hiace kutoka Kibaha-Mbezi aliyejitambulisha kwa jina la Abbas Juma ,alilipongeza jeshi hilo kwa kusimamia sheria za usalama barabarani .

Alisema madereva wamekuwa wakichukia endapo wakionewa ,lakini kwa wale wanaofanya makosa na kusababisha ajali kizembe alidai wachukuliwe hatua kali ili kupunguza vifo na majeruhi kwa abiria wasio na hatia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad