HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 13, 2018

WAZIRI MKUU AZINDUA MPANGO MKAKATI AFYA MOJA

Na Said Mwishehe, Blogu ya jamii
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa mahala salama na penye afya bora huku akielezea jitihada zinazochukuliwa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na matukio hatarishi kwa wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam, wakati anazindua Mpango Mkakati wa Afya Moja na Dawati la Kuratibu Afya Moja nchini huku akisisitiza uzinduzi huo ni muhimu hasa kupindi hiki ambacho kumekuwepo na muingiliano mkubwa kati ya binadamu, wanyama na mazingira.

Amesema dhana ya dhana ya Afya Moja inafaa kutumika zaidi katika nchi zinazoendelea kwani inatoa fursa kwa wadau mbalimbali kushirikana katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

"Mpango huu wa Afya Moja ni ajenda ambayo ipo kwenye nchi mbalimbali duniani na kwa Tanzania ni mpango ambao tunaamini utasaidia kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yatokanayo na binadamu, wanyama na mazingira,"amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Ameongeza mkakati wa kukabiliana na maradhi yatokanayo na wanyama na mazingira ni muhimu kwa nchi nyingi za Afrika kwani zipo kwenye hatari zaidi.

Amesema katika Bara la Afrika kuna maeneo mengi yenye mapori makubwa ,hivyo ni rahisi kuwepo kwa magonjwa ya kuambukizwa yanayotokana na binadamu, wanyama na mazingira,hivyo Afya Moja imekuja wakati sahihi.

Ametoa mfano wa mapori makubwa yaliyopo kwenye Bonde la Mto Kongo, ambalo mazingira yake yamekuwa ni kitovu cha magonjwa ya mlipuko kama vile Ebola, Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Marburg na mengineyo.

"Wiraza husika kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar wakae na kuupitia muundo wa Afya Moja na kisha kuangalia namna watakavyoshirikiana kikamilifu kuutekeleza mpango huu.Lengo la Serikali yetu ni kuhakikisha wananchi wake kuwa salama na wenye afya bora.

"Tutakapokuwa na afya bora maana yake tutapiga hatua za kimaendeleo na hasa kipindi hiki cha kuelekea kwenye Tanzania ya Viwanda,"amesisitiza.

Majaliwa amesema kwa kutambua hilo, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na wadau wengine wa Maendeleo imeendelea kutekeleza agenda ya Afya Moja nchini tangu mwaka 2013 ilipozinduliwa kwa mara ya kwanza mjini Arusha na  Makamu wa Rais Mstaafu, Dk.Mohamed Gharib Bilal.

"Utekelezaji wa mpango huu unakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2015-2020) ya kujenga Taifa lenye watu wenye afya bora itakayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali ambayo ni muhimu katika kufikia azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda,"amesema Majaliwa.

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema uzinduzi wa mkakati huo ni ngao tosha kwa nchi katika kuzuia na kudhibiti magonjwa.

Amesema pamoja na kutekeleza kanuni za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ambazo zinahitaji ushirikiano  wa sekta mbalilmbali kwa kutumia dhana ya Afya Moja, mpango mkakati huo unaleta msukumo katika Ofisi ya Waziri Mkuu  kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali kudhibiti magonjwa.

Jenista amesema uratibu wa afya moja unakwenda sambamba na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika linaloshughulika na Afya ya Wanyama (IOE) na Shirika la Kimataifa la Chakula la Kilimo (FAO) ambayo yanashirikiana kudhibiti magonjwa yanayoambukiza na usugu wa dawa.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameeleza hatua mbalimbali ambazo wizara hiyo inachukua kukabiliana na magonjwa mbalimbali nchini.

Pia amesema mwaka 2016 walifanya utafiti kama sehemu ya kutathimini mpango huo na kubaini kuna changamoto ya usugu wa dawa umeongezeka kwa wanyama, matumizi holela ya dawa na chanjo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad