HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 12, 2018

WAZIRI MKUU AKUTANA NA WAKURUGENZI WA KAMPUNI YA NAMERA NA JOC

MKUUWAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa viwanda vikubwa viwili vya kuchakata pamba ambao wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu.

Viongozi hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi na Mkurugenzi Mtendaji wa JOC Bw. Qin Mengwei ambao kwa pamoja wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa.

Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao leo (Jumatatu, Februari 12, 2018) jijini Dar es Salaam na amesema kwamba wakulima waliitikia wito wa Serikali wa kufufua zao hilo, hivyo mwaka huu wanatarajia kupata mavuno mengi.

Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wajiandae kununua pamba nyingi kwa sababau mwaka huu wakulima wamelima pamba ya kutosha baada ya Serikali kuwahamasiha waongeze uzalishaji kwa kuwa kuna soko la uhakika.



Amesema hatua hiyo imekuja baada ya Rais Dkt. John Magufuli kutoa maelekezo ya uhamasishaji wa kilimo hasa mazao makuu ya biashara, tayari tija imeanza kuonekana ambapo zao la korosho limepata mafanikio makubwa na sasa linafuatia zao la pamba.


Waziri Mkuu amesema Serikali inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba kwa wakulima kuelekezwa kulima kitaalam, upatikanaji wa pembejeo hadi masoko, hivyo amewaalika viongozi hao kushiriki katika mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara wote wa zao hilo.


“Mimi mwenyewe mwezi huu nitakuwa na ziara ya kikazi mkoani Mwanza, kwa hiyo tarehe 21, Februari, nimeitisha mkutano wa wafanyabiashara wote wa pamba nchini iwe ni wanaosokota nyuzi, kuchambua pamba au kukamua mbegu za pamba, ili mradi wanajihusisha na pamba nanyi naomba muwepo”.


Waziri Mkuu amesema Serikali imefurahishwa na uamuzi wao wa kutaka kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu kwani ni faraja kwa Taifa kwa sababu wakulima walipunguza uzalishaji baada ya kukosa soko la uhakika.


Kwa upande wao, Bw. Pardesi na Bw. Qin wamemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba kampuni zao zinauwezo wa kununua pamba yote inayozalishwa nchini na kuichakata katika viwanda vyao na kutengeneza nyuzi na nguo zitakazouzwa nchini kwa bei nafuu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 12, 2018.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa viwanda vikubwa viwili vya kuchakata pamba cha Namera Group of Industries,na JOC. Wakurugenzi hao wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini kuanzia msimu huu.Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao leo, Februari 12, 2018 Ofisini kwake jijini Dar es Salaam. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa JOC Bw. Qin Mengwei (Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Namera Group of Industries Bw. Hamza Rafiq Pardesi (kushoto mwenye miwani nyeusi) . Wakurugenzi hao wameahidi kununua pamba yote itakayozalishwa nchini Tanzania. Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao leo, Februari 12, 2018 Ofisini kwake jijini Dar es Salaam. PICHA NA OFISI YA WAZIRI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad