HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 7, 2018

WAVURUGA ELIMU KONDOA WAMKERA MKUU WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mh. Sezaria Makota amesema hatowafumbia macho wale wote wenye nia ya kuishusha wilaya ya Kondoa kielimu kwa kuvuruga kwa makusudi mikakati ya kuinua elimu wilayani humu.

Aliyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa elimu wa Halmashauri ya Mji Kondoa kilichofanyika katika ukumbi wa Kondoa Irangi hivi karibuni na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu ili kujadili changamoto na  mikakati ya kuinua elimu ndani ya Wilaya ya Kondoa.

Alisema kuwa katika utawala wake hatoruhusu elimu kushuka kwani matokeo ya darasa la saba mwaka jana wilaya imeshuka kiwastani ukilinganisha na mwaka juzi ambapo wilaya ilikuwa na wastani wa asilimia 80 na mwaka jana imeshuka na kufikia asilimia 71 hivyo viongozi wajipange kusimamia elimu ili kuhakikisha ufaulu unapanda.

Aidha aliwaagiza maafisa elimu kumpelekea mipango yao ili kuona jinsi gani wanainua elimu na kutaka viongozi wa Halmashauri kuacha migogoro na kutekeleza mipango kwa vitendo ili kufikia mafanikio katika elimu.

Wakiongea wadau mbalimbali waliojitokeza walisema kuwa changamoto kubwa ya kushusha ufaulu katika wilaya ni upungufu wa walimu, wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu, kukosekana kwa mafunzo kwa walimu, kutolipa madai ya walimu mapema na utoro wa wanafunzi kutokana na kutoelewa masomo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kondoa Mh. Hamza Mafita alifafanua kuwa Halmashauri inaendelea kujipanga kuboresha sekta ya walimu kwa kuwapatia motisha walimu na kuwapatia gari Idara ya Elimu ili waweze kufanya ufuatiliaji wa elimu na kuwaagiza Waheshimiwa Madiwani kuweka elimu kuwa agenda ya kudumu katika vikao vya kata.

Akifunga kikao hicho Mbunge wa Kondoa Mjini Mh. Edwin Sannda alisema kuwa viongozi wanawajibu wa kuwabadilisha wazazi ili wawe na utamaduni wa kupenda elimu ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili kwa wanafunzi, walimu na watumishi kwani kwa kufanya hivyo elimu itapanda kwani changamoto zilizopo ni za nchi nzima.

Kikao cha wadau wa Elimu kilifanyika hivi karibuni wilayani Kondoa kwa ajili ya kubaini, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuinua elimu ambapo pia walimu mbalimbali wa Shule za Masingi waliofaulisha kwa alama A kwa somo walipewa zawadi ikiwemo shule tano zilizofanya vizuri na shule tano zilizofanya vibaya.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Kwapakacha Mwalimu Pantaleo akisoma barua katika kikao cha wadau wa elimu iliyoandikwa na mwanafunzi wa kidato cha pili akielezea sababu za kutaka kuacha shule.
  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kondoa akimwelekeza Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tungufu kupandisha ufaulu baada ya kupokea cheti cha shule yenye ufaulu duni Wilayani katika kikao cha wadau wa elimu kilichofanyika katika ukumbi wa Kondoa Irangi hivi karibuni.
 Katibu Tawala Wilaya ya Kondoa, Winnie Kijazi akimpa zawadi mmoja ya walimu waliofaulisha kwa alama A katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2017 kwenye kikao cha wadau wa elimu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad