HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 7, 2018

ZAIDI YA BILIONI 25 KUTEKELEZA SHUGHULI MBALIMBALI MWAKA 2018/2019 KATIKA HALMASHAURI YA WILAYA NJOMBE.

Na: Lukelo Mshaura, Njombe.
Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Njombe limepitisha mapendekezo ya rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 wilayani hapa.
Katika mapendekezo hayo baraza hilo limepitisha kiasi cha zaidi ya bilioni 25.2  kutumika katika kutekeleza shughuli mbalimbali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019.
Akisoma mpango na rasimu ya  bajeti  kwenye kikao cha baraza la madiwani ,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi Monica Kwiluhya alivitaja vyanzo vya kufanikisha bajeti hiyo kuwa ni Serikali Kuu, wafadhili, mapato ya ndani, uchangiaji wa huduma za afya, uchangiaji wa ada kidato cha tano na sita pamoja na mchango wa jamii kwenye miradi ya maendeleo.
Akiainisha mchanganuo wa vyanzo hivyo  Bi Kwiluhya alibainisha kuwa Serikali kuu inatarajiwa kuchangia kiasi cha bilioni 20.179, wafadhili bilioni 2.965, mapato ya ndani halisi bilioni 1,439, uchangiaji huduma za afya  zaidi ya milioni 140, uchangiaji ada ya kidato cha tano na sita milioni 42 huku mchango wa jamii kwenye miradi ya maendeleo ukiwa ni kiasi cha milioni 520.
Bi kwiluhya alifafanua kuwa  mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya wilaya ya Njombe imekadiria kutumia zaidi ya bilioni tano ( 5) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri.
“Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe haina hospitali ya wilaya kutokana na Halmashauri hii kugawanyika katika halmashauri tatu hivyo tumeweka maombi maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali kiasi cha bilioni mbili  ambazo ni fedha za awamu ya kwanza” alisema Bi Kwiluhya.
Aliongeza kuwa katika kufanikisha hilo tayari Halmashauri imetenga bajeti ya milioni 180 kupitia mapato yake ya  ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya wilaya itakayojengwa katika Kata ya Matembwe wilayani Njombe.
Aliyataja maeneo ya kipaumbele kuwa ni miradi ya maendeleo itakayoleta matokeo ya haraka (Quick Wins) ambayo itasaidia kuinua uchumi, kurejesha asilimia 20 ya mapato ya ndani kwenye vijiji, pamoja na kuboresha huduma mbalimbali za jamii.
Maandalizi ya mpango na bajeti wa Halmashauri ya Wilaya Njombe umeanza katika ngazi za vijiji ambapo jamii imeshiriki katika kuibua miradi na kujadiliwa katika mikutano mbalimbali kuanzia ngazi ya kijiji.
Sambamba na hilo bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia  Utekelezaji wa Malengo Makubwa ya Dira ya Maendeleo ya taifa mwaka 2025, Malengo ya maendeleo endelevu kidunia 2016-2030, Mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017-2020/2021 pamoja na muongozo wa uandaaji wa bajeti ya mwaka 2018/2019.
Miongozo mingine iliyozingatiwa wakati wa uandaaji wa bajeti ni Hotuba ya Rais wa Jamhuri hya Muungano wa Tanzania wakati akilizindua bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20,  Novemba 2015, Mpango mkakati wa Halmashauri wa miaka mitano (2016/2017-2020/2021), mipango shirikishi ya jamii kwa kutumia dhana ya Fursa na vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) pamoja maelekezo  yaliyotolewa katika Ilani ya chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe, Bi Monica Kwiluhya akiwasilisha mapendekezo ya mpango na bajeti wa Halmshauri ya wilaya ya Njombe wa mwaka 2018/2019.
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe wakifuatilia mjadala wa mapendekezo ya  bajeti ya halmashauri hiyo ya mwaka wa fedha 2018/2019

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad